Semkae Kilonzo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Policy Forum, mtandao wa mashirika 62 ya asasi za kiraia za Tanzania unaolenga kuimarisha utawala bora na matumizi yenye uwajibikaji ya rasilimali za umma kwa kujenga uwezo wa wadau wa kiraia kushawishi na kufuatilia utekelezaji wa sera, pamoja na kuimarisha mwitikio wa serikali kwa ajenda ya utetezi ya asasi za kiraia inayohusu matumizi yenye uwajibikaji ya rasilimali za umma.
Semkae ana uzoefu mkubwa katika kazi za utetezi wa sera akiwa na asasi za kiraia nchini Tanzania, na ana shauku ya kupambana na mtiririko haramu wa fedha hususan katika sekta ya uziduaji, pamoja na kuhakikisha usimamizi wa mapato yatokanayo na rasilimali asilia unawanufaisha wananchi kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali, sekta binafsi na jamii.
Semkae ana shahada ya uzamili (Masters) katika Uandishi wa Habari na Masomo ya Vyombo vya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Cardiff, Uingereza, na alipata mafunzo yake ya awali ya uandishi wa habari nchini Ireland (Dublin) na katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Tanzania. Pia ni mhitimu wa kozi ya Misingi ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Huduma za Umma (Fundamentals of Social Accountability Monitoring Course) ya Public Service Accountability Monitor (PSAM) katika Chuo Kikuu cha Rhodes, Afrika Kusini.
Aidha, Semkae ni mwanzilishi mwenza na mjumbe wa Bodi ya Hakirasilimali, jukwaa la asasi za kiraia linalofanya kazi kwenye masuala ya kimkakati yanayohusu uchimbaji wa madini, mafuta na gesi nchini Tanzania