Policy Forum inasikitishwa na taarifa za vifo vya wananchi, ukiukwaji wa haki za binadamu na changamoto nyingine za utawala bora zilizojitokeza katika kipindi kilichofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Tunaungana na Watanzania wote kuomboleza wale waliopoteza maisha na tunatoa pole kwa familia zote zilizoathirika.
Tunasikitishwa na taarifa za kuaminika kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyofanywa na polisi na vyombo vya usalama dhidi ya raia. Matendo haya yanadhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma na yanapingana na wajibu wa vyombo vya dola kulinda wananchi na kudumisha utawala wa sheria.
Uwajibikaji na haki ni mambo muhimu katika kurejesha imani ya umma kwa taasisi za serikali. Tunatoa wito kufanyika kwa uchunguzi huru na wa wazi kuhusu matukio haya ya vurugu na kuwawajibisha kisheria wale wote waliohusika.
Kama mtandao unaojitolea kukuza uwazi, uwajibikaji na utawala bora, Policy Forum inatoa wito kwa serikali na wadau wote kuimarisha heshima kwa haki za binadamu, ushiriki wa wananchi, na maadili ya kidemokrasia kama msingi wa amani ya kudumu na umoja wa kitaifa.
Imetolewa na:
Policy Forum
Novemba 6, 2025, Dar es Salaam, Tanzania