Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Kama ilivyo kwa nchi nyingi zinazoendelea, Tanzania imeathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi, madhara ambayo hayaishii tu kusababisha mafuriko na ukame lakini yanaharibu miundombinu na hata kuathiri maisha ya watanzania kwani kilimo, sekta inayoajiri watu wengi takriban asilimia 65.5 imeathiriwa sana na hali mbaya ya mvua. Aidha, athari za mabadiliko ya tabianchi pia zimeathiri sekta ya uziduaji hususan ufanisi katika shughuli za Uchimbaji mkubwa na mdogo wa madini (Large- & Small-scale mining operations).

Ni muhimu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu utafiti unaonesha kuwa Afrika ndilo bara lililoathiriwa zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi kwani uchumi wake bado unategemea hali ya hewa nzuri ili kukuza baadhi ya sekta muhimu za kiuchumi kama vile kilimo. Athari zinakithiri kutokana na bara kutokuwa na uwezo wa kupunguza au kuzoea (adopt) athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania inategemea zaidi vyanzo vya nje kufadhili hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, njia endelevu zaidi ya kukabiliana na changamoto hii ni kufadhili athari hizi kupitia mapato ya ndani ya nchi. Kwa bahati nzuri, mapato ya fedha nchini Tanzania yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na deni la Taifa likiwa ni himilivu. Hii imeendana na ongezeko la mapato katika sekta ya uziduaji kutoka asilimia 4.8 kwa mwaka wa fedha 2016/17 hadi asilimia 7.2 kwa mwaka wa fedha 2020/21, hivyo kutoa uwezekano mkubwa wa kukusanya mapato ya ndani ili kutumika kufadhili athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, kwa wingi wa madini ya kijani, sekta ya uziduaji nchini Tanzania inaweza kutumika kuchochea mapinduzi ya kijani na kwingineko.

Hata hivyo, uwezo wa kukusanya mapato ya ndani kikamilifu unaathiriwa na utoroshwaji wa fedha nchini. Ushahidi unaonesha kuwa nchi inapoteza takriban dola za kimarekani billion 1.5 kwa mwaka kutoka katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uziduaji kupitia njia tofauti tofautii za utoroshwaji fedha. Ni wakati muafaka Tanzania iungane na mataifa mengine ili kukabiliana na utoroshwaji wa fedha. Mfumo Jumuishi uliopendekezwa na OECD na G20 unaweza kuwa njia mojawapo ya kusaidia nchi kupambana na mikakati inayotumiwa na makampuni ya kimataifa ya kibiashara kucheza na mapungufu katika sheria za kodi ili kuepuka kulipa kodi (Base Erosion & Profit Shifting (BEPS).

Pamoja na changamoto hiyo, sekta ya uziduaji inaweza kutumika kufadhili hatua za mabadiliko ya tabianchi. Washiriki katika utafiti huu ambao unazinduliwa leo wanakubaliana na ukweli kwamba sekta ya uziduaji inapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kufadhili mabadiliko ya tabianchi. Lakini pia wahojiwa walieleza kuwa kwa sasa hakuna chombo cha kipekee cha kusimamia ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi Tanzania, wote wanaamini kuwa chombo kama hicho ni muhimu, lakini ni lazima utawala bora uzingatiwe ili kuepusha matumizi mabaya ya rasilimali fedha.

Mapendekezo:

1. Kuzingatia mapendekezo katika Mfumo Jumuishi wa kupambana na mikakati inayotumiwa na makampuni ya kimataifa ya kibiashara kucheza na mapungufu katika sheria za kodi ili kuepuka kulipa kodi (Base Erosion & Profit Shifting (BEPS).

2. Kuanzisha utaratibu wa kuweka gharama ya kaboni (carbon pricing mechanism) ili kufadhili hatua za mabadilko ya tabianchi.

3. Kuanzisha motisha inayolenga makampuni yanayotumia teknolojia inayoweza kurejeshwa na yenye ufanisi (Renewable and efficient technologies).

4. kuanzisha ushuru wa kijani kwa shughuli na bidhaa zinazotumia kaboni nyingi nchini.

5. Kutumia sehemu ya fedha za CSR kwa ajili ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

6. Kutumia kati ya asilimia 5 hadi 10 ya mrabaha kufadhili athari za mabadiliko ya tabianchi.