Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Imeendikwa na Emmanuel Kavula (EOL Project Champion) kuelekea Mkutano wa Tano wa Vijana wa Afrika kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 14 -18 August, 2023

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua kubwa na inaendelea kufanya mageuzi muhimu katika sekta ya elimu, na hivyo kuleta mabadiliko chanya ndani na nje ya nchi, kwa faida ya Tanzania na raia wake. Taifa hili limetokea kuwa kielelezo bora ambacho wengine wanaweza kujifunza, kwa jinsi inavyowahudumia raia wake kwa uwaminifu, uadilifu, na mafanikio makubwa, hasa katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Kati ya mageuzi muhimu yanayotekelezwa na Serikali ya Tanzania katika kufuatilia na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni:

  1. Utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila Malipo

Kwa kutekeleza sera ya elimu bila malipo kutoka kidato cha kwanza hadi kidato cha sita, Serikali ya Tanzania imejizatiti kuwawezesha watoto wote kupata elimu bila ada. Hatua hii inaonyesha dhamira ya Tanzania katika kuboresha viwango na upatikanaji wa elimu na mafunzo. Sasa hivi, kila mtoto anaweza kwenda shuleni na kusoma bila kizuizi cha ada, badala ya kukosa fursa ya elimu kwa sababu ya kukosa fedha.

  1. Kuwarudisha Wanafunzi wote wa kike waliokuwa wamekatishwa masomo kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo Ujauzito

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza, na kusimamia Malengo ya Maendeleo Endelevu ( SDGs  ) ikiwemo kuwaruhusu wanafunzi wote wa kike waliokuwa wamekatishwa masomo kutokana na kubeba ujauzito kuendelea na shule. Hii ni kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa elimu.

  1. Kutoa huduma ya chakula na lishe mashuleni

Serikali ya Tanzania imejitahidi kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha watoto na wanafunzi wanapata huduma muhimu kama chakula bora, maji safi, na huduma za afya wanapokuwa shuleni. Hii ni hatua inayojenga imani na kuongeza matumaini katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inaeleza wazi umuhimu wa kutoa huduma muhimu kama chakula bora, maji safi, na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni. Kwa hiyo, kupitia viongozi wa elimu wa kata (WEOs) na maafisa elimu wa kata (MEKs) katika maeneo yao, kuhakikisha kila shule inatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi ni kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

  1. Kuongeza na kuboresha Miundombinu ya Shule

Katika kuhakikisha kuwa elimu bora inafikishwa karibu na jamii, Serikali ya Tanzania imejitahidi sana kwa kutoa fedha na kusimamia miradi ya ujenzi wa miundombinu katika sekta ya elimu. Miradi hii inajumuisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, maktaba, maabara za sayansi, vyumba vya TEHAMA, mabweni, na nyumba za walimu. Kupitia programu ya BOOST, jumla ya kiasi cha fedha cha bilioni 1.6 kitatumika kufanikisha ujenzi wa majengo mapya, ikiwa ni pamoja na kujenga shule mpya mbili. Pia, vyumba vya madarasa takribani 55 na matundu 50 ya vyoo vitajengwa katika Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.

Aidha, kupitia mradi wa SEQUIP, fedha kiasi cha TZS 48 bilioni zimetolewa kwa mikoa 16 kwa ajili ya kujenga shule mpya za wasichana zinazojikita katika masomo ya sayansi. Mkoa wa Geita pekee umepokea ufadhili wa TZS bilioni 3, jambo linaloonesha jitihada kubwa za kuhakikisha utoaji endelevu na imara wa elimu na mafunzo katika ngazi ya elimu ya msingi.

  1. Kuimarisha mfumo wa TEHAMA kwa Wanafunzi wa elimu ya msingi na mikopo kwa Wanafunzi wa elimu ya juu.

Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuleta mageuzi katika mfumo wa elimu. Hatua hizi ni pamoja na kuanzisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Programu ya Maktaba Mtandao imekuwa msaada katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vitabu vya kiada shuleni. Hii imepunguza gharama kubwa za kununua vitabu na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kusomea.

Kuanzishwa kwa mfumo wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imekuwa hatua muhimu. Mwongozo wa uombaji wa mikopo kwa mwaka 2023/2024 umefanyiwa maboresho, ambapo sasa waombaji wanaweza kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao badala ya kutumia nakala ngumu au kwenda kwenye Bodi ya Mikopo. Maboresho haya yametokana na ufadhili wa mradi wa Elimu ya Juu "Higher Education for Economics Transformations" (HEET) uliotekelezwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2026.

Serikali imeongeza bajeti ya mikopo na kuwezesha wanafunzi kupata ufadhili wa masomo. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendeleza jitihada hizi kwa kuanzisha ufadhili maalumu unaojulikana kama "Samia Scholarship" kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi katika kidato cha sita. Kupitia ufadhili huu, wanafunzi 640 wamenufaika na jumla ya shilingi bilioni 3. Hatua hizi zinaonyesha dhamira ya serikali katika kuboresha upatikanaji na ubora wa elimu nchini.

  1. Kufanya mabadiliko ya Sera na mtaala wa Elimu ili kuendana na mabadiliko ya Dunia ya sasa

Kupitia mapendekezo yaliyotolewa katika Rasimu ya Ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Maboresho ya Mitaala, kuna mpango wa kubadilisha mfumo wa elimu nchini Tanzania. Baadhi ya mapendekezo hayo ni kuondoa mtihani wa darasa la saba, kuhakikisha kwamba mwanafunzi anapoanza darasa la kwanza anamaliza kidato cha nne. Aidha, lugha ya kufundishia na kujifunzia itakuwa Kiswahili, na Kiingereza kitafundishwa kama somo katika shule zinazotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia, na Kiswahili kitakuwa somo katika shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Hatua hii inaonyesha wazi juhudi za Tanzania katika kutekeleza na kusimamia Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Hatua ya kutekeleza mabadiliko haya katika mfumo wa elimu, ikiwa ni pamoja na kufanya Kiswahili kuwa lugha kuu ya kufundishia, inaonesha jitihada za Tanzania katika kuendeleza lugha na utamaduni wake, na hivyo kuchangia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.

Nini kifanyike ili kuboresha zaidi sekta ya Elimu Tanzania

Ingawa Serikali imejitahidi kwa jitihada kubwa, bado kuna changamoto za upungufu wa bajeti katika kugharamia miundombinu ya shule, malipo ya mishahara ya walimu, ununuzi wa vitabu vya kiada, na kununua vifaa vya kufundishia. Ili kufanikisha mabadiliko ya mtaala na sera ya elimu, Serikali ya Tanzania inahitaji upatikanaji wa ufadhili wa kutosha. Hii ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu na watekelezaji wengine wa mtaala mpya, kama vile walimu wa kozi na masomo mapya. Hii itasaidia kuwajengea uwezo ili waweze kufundisha kwa ufanisi na kuhakikisha mabadiliko yanafikiwa.

Utekelezaji wa mtaala mpya na Sera ya Elimu ya mwaka 2023 unatarajiwa kufanyika kwa awamu. Hii inalenga kusawazisha gharama na bajeti, kwani kuanza kwa mtaala mpya katika madarasa yote na ngazi zote kwa pamoja ingekuwa na gharama kubwa sana. Utekelezaji kamili wa mtaala mpya unatarajiwa kuanza mwaka 2024 ikiwa sera na mtaala husika zitapitishwa kama ilivyopangwa.

Hatua hizi za kuhakikisha kuanza kwa awamu zitawezesha Serikali kujipanga kwa ufanisi zaidi katika utekelezaji wa mabadiliko ya elimu, huku ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa bajeti inakidhi mahitaji ya kutekeleza mabadiliko hayo kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika mfumo wa elimu nchini.

Changamoto zinazokabili Tanzania na kuathiri ubora wa Elimu
Mapato kutokana na rasilimali kama madini ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Hata hivyo, ukosefu wa uwazi katika mikataba na utaratibu wa kugawanya mapato kwa serikali unaweza kusababisha kutokuwepo kwa uwiano mzuri katika upatikanaji wa mapato hayo. Hii inaweza kuathiri uwezo wa serikali kuboresha sekta muhimu kama elimu na kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini nayo yanapata fursa za maendeleo.

Ni muhimu kwa serikali kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika mikataba na makubaliano yoyote yanayohusiana na rasilimali za nchi. Hii itasaidia kuhakikisha kuwa mapato yanayopatikana yanatumika kwa manufaa ya wananchi wote na kwa ajili ya kuboresha huduma za umma kama elimu. Kwa kuweka mifumo madhubuti ya kutoa taarifa na kufuatilia matumizi ya mapato haya, serikali inaweza kuleta usawa zaidi katika ugawaji wa rasilimali na kuhakikisha kuwa maendeleo yanawanufaisha wananchi wote

Mikopo na misaada inayotolewa na nchi za nje mara nyingi huja na masharti magumu. Kuwepo kwa "Structural Adjustment Programs" (SAPs) au mipango ya kurekebisha miundo ya uchumi, kunaweza kuwa na matokeo ya kubana matumizi na kufuata masharti fulani yanayowekwa na wakopeshaji. Hii inaweza kusababisha taifa kuwa na mzigo mkubwa wa kulipa madeni ya nje badala ya kuwekeza kikamilifu katika sekta muhimu kama elimu.

Masharti haya ya kifedha yanaweza kuwa na athari hasi kwa maendeleo ya nchi. Kwa mfano, kulazimishwa kubana matumizi katika sekta ya elimu kunaweza kusababisha upungufu wa fedha za kuendesha shule na kuboresha miundombinu, na hivyo kusababisha kukwama kwa maendeleo ya elimu. Hii inaweza kuchangia ukosefu wa usawa katika ugawaji wa rasilimali za umma, hususan katika sekta ya elimu.

Ni muhimu kwa serikali kuangalia kwa kina athari za masharti haya ya mikopo na misaada kutoka nje na kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa yanaleta manufaa halisi kwa wananchi. Kipaumbele kinapaswa kuwekwa katika kuendeleza sekta muhimu kama elimu ili kuhakikisha kuwa maendeleo yanafikiwa na kuwa na athari chanya kwa jamii nzima.

Nchi yetu inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa ya ujinga. Mojawapo ya vikwazo ni utayari mdogo wa wazazi kuchangia maendeleo ya elimu. Hii imekuwa kikwazo kwa utekelezaji wa mipango na sera nzuri za serikali zinazolenga kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundisha. Aidha, uelewa mdogo wa jamii kuhusu masuala ya elimu na taaluma umesababisha kukosekana kwa ushirikiano mzuri kati ya serikali na wazazi, hususani katika maeneo ya vijijini.

Ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wazazi ni muhimu katika kuboresha elimu. Wazazi wanahitaji kuelimishwa kuhusu umuhimu wa elimu na jukumu lao katika kuchangia maendeleo ya elimu. Kwa kushirikiana na serikali, wanaweza kuchangia kuboresha miundombinu ya shule, kutoa motisha kwa walimu, na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza.

Ushirikiano huu unaweza kujengwa kupitia mikutano na mazungumzo kati ya serikali, wazazi, na jamii nzima. Elimu na uelewa juu ya umuhimu wa elimu unapaswa kusambazwa ili kuhamasisha ushiriki wa wazazi katika masuala ya elimu. Serikali inaweza kuchukua hatua za kuhamasisha na kutoa motisha kwa wazazi kushiriki kikamilifu katika kuboresha elimu, na hivyo kuleta mabadiliko chanya katika mazingira ya kujifunza na ufundishaji.

Nini kinapaswa kupewa kipaumbele na wafanya waamuzi?

Kutoa elimu kwa wazazi ni hatua muhimu katika kuboresha hali ya elimu nchini. Kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ni wazo zuri kuanzisha warsha na mikutano katika maeneo ya vijijini ili kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu. Kwa kuongezea, matumizi ya zana za mawasiliano kama vile video, sinema, na maigizo yanaweza kuwa njia bora za kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia inayovutia na inayoeleweka.

Kupitia video, sinema, na maigizo, jamii inaweza kuona kwa njia jinsi elimu inavyoleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu. Hii inaweza kujumuisha mifano halisi ya watu wanaofanikiwa kupitia elimu, na jinsi elimu inavyowezesha fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi. Pia, inaweza kuelezea jinsi elimu inavyochangia katika kujenga jamii yenye uelewa, afya bora, na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.

Kuandaa warsha na matamasha ya elimu katika maeneo ya vijijini ni njia nzuri ya kuwashirikisha wazazi na jamii nzima. Inawawezesha kujifunza na kubadilishana uzoefu, na pia inatoa fursa ya kuuliza maswali na kushiriki katika majadiliano. Kwa kufanya hivi, jamii itakuwa na ufahamu mzuri zaidi wa umuhimu wa elimu na jinsi inavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao na ya watoto wao.

Upatikanaji wa huduma muhimu kama chakula cha ubora, maji safi, na huduma za afya kwa wanafunzi shuleni ni suala la umuhimu mkubwa. Inafahamika kuwa watoto wengi wa shule hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu kurudi nyumbani kwao wakati wa mchana ili kupata chakula cha mchana. Kurudi nyumbani hutumia muda mwingi hivyo kuathiri uwezo wao wa kuhudhuria vipindi vya mchana darasani.

Hali hii inaweza kuwaathiri wanafunzi kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuhatarisha afya zao na uwezo wao wa kujifunza. Baadhi yao wanaweza kujikuta wakipata njaa na hivyo kuwa na uwezo mdogo wa kujielekeza katika masomo. Wengine wanaweza kukosa hata rasilimali ndogo kama vile shilingi mia mbili kwa ajili ya kununua chakula.

Kwa hiyo, kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora, maji safi, na huduma za afya shuleni ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo bora ya wanafunzi. Hii inaweza kufanikiwa kwa kushirikiana na wadau wa elimu na jamii kwa ujumla, ili kuhakikisha kuwa mazingira ya shule yanakuwa salama na yanayosaidia wanafunzi kujifunza kwa ufanisi na kuendelea vizuri katika masomo yao.

Hakika, upatikanaji wa chakula shuleni unaweza kuwa na athari Chanya katika mafanikio ya elimu. Inaonekana kuwa watoto wanapopata chakula shuleni, ufaulu huongezeka na tatizo la utoro wa wanafunzi hupungua. Pia, kuongezeka kwa muda wa kufundisha hadi jioni kunaweza kuleta faida kubwa kwa wanafunzi. Hii inawapa fursa ya kujifunza zaidi na kufanya mazoezi ya ziada. Wanafunzi pia wanapata muda wa kutosha wa kujisomea na kufanya majadiliano, ambayo yanaweza kuimarisha ufahamu wao na uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika masomo.

Kula chakula shuleni kunaweza kusaidia kupunguza tatizo la udumavu wa akili na utapiamlo miongoni mwa wanafunzi, hasa katika maeneo ya vijijini. Lishe bora inachangia katika maendeleo ya akili na mwili wa wanafunzi, na hivyo kuwa na athari chanya kwa uwezo wao wa kujifunza na kufanikiwa shuleni.

Kwa kuzingatia manufaa haya, kuendelea kuwekeza katika mipango ya kutoa chakula shuleni, kuongeza muda wa kufundisha, na kuwezesha wanafunzi kujisomea na kufanya majadiliano kunaweza kusaidia kuimarisha mazingira ya elimu na kuchangia katika kuboresha matokeo ya wanafunzi na maendeleo ya elimu nchini.

Jambo lingine linalopewa kipaumbele ni kuhakikisha usawa katika uhusiano kati ya teknolojia na elimu. Ni muhimu kuhakikisha kuwa faida za teknolojia zinapatikana kwa kila mwanafunzi, na hakuna anayeachwa nyuma. Kuimarisha uelewa wa wanafunzi kuhusu masuala ya usalama wa kidigitali pamoja na kujenga uwezo wao ni jambo muhimu. Hii inahusu kuwafundisha jinsi ya kutumia teknolojia kwa njia salama na yenye faida, pamoja na kuhakikisha kuwa wanapokuwa mtandaoni, wanapata ulinzi na usalama unaostahili.