Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Mwaka 2018 Policy Forum (PF) mtandao wa asasi zaidi ya 70 zilizosajiliwa Tanzania ilichapisha utafiti unaohusu mikataba ya utozaji kodi mara mbili (Double Taxation Agreements - DTAs) kati ya Tanzania na Afrika Kusini na Tanzania na India. Makala hii ni tafsiri ya muhtasari wa utafiti huo ambao ulitumika kwenye kikao cha pamoja na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wapo kwenye Mtandao wa Kupambana na Rushwa (APNAC) mnamo Novemba 8, 2018 Jijini Dodoma.

Tanzania ina mikataba tisa ya utozaji kodi mara mbili na nchi zifuatazo: Zambia (1968), Italia (1973), Denmark (1976), Finland (1976), Norway (1976), Sweden (1976), India (1979), Canada (1995) na Afrika Kusini (2005). Tanzania hivi sasa inajadiliana kuhusu DTAs na Uholanzi, Uingereza, Falme za Kiarabu, Mauritius, Kuwait, Iran na China bila kuwa na sera ya majadiliano inayoeleweka kwa umma au iliyochunguzwa kwa makini kidemokrasia. Kwa nyongeza, Tanzania ina mikataba ya uwekezaji wa nchi mbili na nchi kumi na tisa na mikataba mingine saba ya uwekezaji na kanda za kiuchumi. 

Mkataba wa mwisho kati ya Tanzania na India wa utozaji kodi mara mbili ulitiwa sahihi tarehe 1 Januari 1979 Dar es Salaam. Mkataba huu unahusu kodi ya mapato inayotozwa kwa niaba ya nchi inayoingia kwenye mkataba au vitengo vyake vya kisiasa au mamlaka za mitaa, bila kujali jinsi kodi hizo zinavyotozwa.

Mkataba kati ya Tanzania na Afrika Kusini wa utozaji kodi mara mbili ulitiwa sahihi tarehe 15 Juni 2007.

Taarifa hii inaonesha matokeo ya utafiti  kwa vipengele vikuu vitatu: Mapitio makini ya  mikataba  ya utozaji kodi mara mbili (DTAs) iliyotiwa sahihi baina ya Tanzania na India pia kati ya Tanzania na   Afrika Kusini; uchambuzi kuhusu hatari  zinaletwa na mikataba hiyoi zinazohusu ugharimiaji wa maendeleo nchini Tanzania; na mapendekezo ya kisera na mambo muhimu ambayo Tanzania inahitaji kuyaingiza wakati wa majadiliano au marudio ya majadiliano ya mikataba hiyo. 

Utafiti huu ulifanyika kwa msaada wa taarifa zilizotokana na modeli za majadiliano ya DTAs ambazo kwa kawaida hutumika ulimwenguni kote ambazo ni pamoja na modeli ya OECD, modeli ya UN, na modeli ya mkataba wa ATAF.

Matokeo muhimu ya utafiti huu ni kama ifuatavyo:

 1. Umuhimu wa uwepo wa ubia wa kibiashara: Nchi zote mbili, Afrika Kusini na India ni wabia wakuu wa kibiashara na Tanzania kwa hiyo DTAs zilizopo zina vidokezi vya hatari kwa msingi wa kodi ya Tanzania;
 2. Pale ambapo nchi zilizo na nguvu za kiuchumi zinaingia katika DTAs na nchi iliyo dhaifu kiuchumi kuna uwiano usio sawa kifedha na upungufu wa nguvu ya majadiliano katika mvutano kuhusu kodi kwa upande wa nchi iliyo dhaifu kiuchumi.

Hatari zilizobainika katika mikataba ya kuepuka utozaji kodi marambili zinajumuisha:

 1. Vipengele vya mikataba ya kodi vinaweza kuwa kinyume na sheria za kodi za ndani ya nchi;
 2. Modeli ya OECD inapendelea nchi zinazopeleka mitaji nje ya nchi kuliko zile zinazotegemea mitaji kutoka nje;
 3. Chini ya Modeli ya OECD baadhi ya mapato na mitaji inaweza kukatwa kodi katika nchi ya makazi ya mlipa kodi pekee;
 4. Kipengele cha uhakika wa wawekezaji kuhusu haki za utozaji kodi baina ya wahusika wanaoingia kwenye mkataba hakijawekwa wazi;
 5. Mikataba ya kuepuka utozaji kodi marambili haiwasaidii wawekezaji kutathmini kwa urahisi kiasi cha kodi watakayohitajika kulipa kwa shughuli zao za uchumi;
 6. Mikataba ya kuepuka utozaji kodi marambili haina motisha ya ziada kwa kampuni za nje kufanya shughuli za biashara Tanzania au kwa kampuni za Tanzania kufanya shughuli za biashara nje ya nchi;
 7. Kanuni zisizo rafiki kuhusu kodi ya faida ya kimtaji na kanuni dhidi ya ukiukaji wa mikataba zinaweza kuingizwa ndani ya mikataba ya kuepuka utozaji kodi marambili.

Hatari kuu tatu  kwa mtazamo wa haki za ki-kodi  

 1. Kwanza, mikataba ya kimataifa ya kodi imeleta ulimwenguni kote hali ya kutotoza kodi mara mbili -  ambapo mapato hayalipiwi kodi popote hivyo kuleta mmomonyoko wa misingi ya kodi. 
 2. Pili, DTAs huunda hali ya sintofahamu kwamba ni mamlaka ipi kisheria ina haki ya kutoza kodi.  Je ni chanzo cha mapato (yaani yule ambaye ni mwenyeji wa uwekezaji wa ndani) au mamlaka ya kisheria ambapo mwekezaji anaishi: nchi iliyotoka mtaji? 
 3. Tatu, DTAs huunda changamoto kuhusu jinsi taarifa za kutosha zinavyoweza kutawanywa yaani wahusika kubadilishana taarifa ili kuruhusu mamlaka za kodi kupata taarifa wanazohitaji.
 •  Baadhi ya changamoto zilizoshuhudiwa katika utafiti wa DTAs:

-     Uhamishaji wa faida nje ya nchi zinazoendelea kunaweza kuwa na matokeo hasi katika  uwezekano wao wa kupata maendeleo endelevu. 

      -     Nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Tanzania mara nyingi hazijajizatiti kushughulikia mlolongo wa mbinu nyingi na ngumu za kuepuka kodi zinazotumiwa na       miji iliyoko ufukweni. Kadiri uwekezaji unavyopitia miji ya ufukweni ndivyo faida inayoweza kutozwa kodi inavyopungua.

      -     Kuna taarifa chache sana za kuthibitisha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya DTAs na utendaji wa kiuchumi wa mataifa husika. 

 • Ili kurekebisha maeneo ambayo hayakuwa sawa katika utafiti huu wa DTAs ajenda zifuatazo za kisera zinapendekezwa:
 1. Ajenda ya Kiutendaji ya Addis Ababa (AAAA) ya Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Fedha kwa ajili ya Maendeleo (Addis Ababa, 13 – 16 Julai 2015)  unatoa mfumo mpya wa kugharamia maendeleo endelevu kwa kupangilia mtiririko wa fedha na sera ili viende  sambamba na  vipaumbele vya kiuchumi, kijamii, na kimazingira. Kama ilivyoainishwa katika AAAA, nchi zinahitaji kuimarisha usimamizi wa kodi, kutekeleza sera za kuzalisha rasilimali zaidi, na kupiga vita rushwa na usafirishaji haramu wa fedha
 2. Ili kuhakikisha kwamba wawekezaji wananufaika na siyo serikali ya nyumbani, nchi nyingi zinazoendelea husisitiza kuwa na ibara ya “ubishani wa kodi” katika mikataba ya kodi na nchi zilizoendelea.
 3. Inapendekezwa kwamba modeli ya nchi yeyote inapaswa iingize mambo ya msingi yaliyomo katika modeli ya Umoja wa Mataifa (UN). Utafiti wa nchi za Afrika ya Mashariki unaonesha mikataba ya kuamini / tumaini, lakini baadhi ya mamlaka za kisheria zimeweza kubaki na haki zaidi katika utozaji kodi kuliko wengine kutokana na kutegemea zaidi katika mbinu zinazotumika katika modeli ya UN.

Ripoti ya Policy Forum inatoa mapendekezo yafuatayo:

1. Mikataba mingi ya utozaji kodi marambili iliyopo sasa imepitwa na wakati, hivyo inahitaji kufanyiwa marekebisho kwa manufaa ya Watanzania;

2. Epuka motisha za kikodi: Mwezi Juni 2012, taarifa ilikadiria kuwa Tanzania ni moja ya nchi maskini zaidi duniani na inapoteza karibu Dola za Marekani bilioni 1 ya mapato ya kodi kila mwaka kutokana hasa na ukwepaji kodi, utoroshaji wa fedha, na motisha za kodi;

3. Tanzania inapaswa kufanya uchambuzi wa viwango vya DTAs zote na kulinganisha na vile vya mwekezaji wa ndani. Uchambuzi wa kina utaonesha misingi ya hivyo viwango pamoja na matokeo na vidokezi vyake kwa Tanzania;

4. Majadiliano ya DTA yanapaswa yaendeshwe chini ya mwongozo wa  Mikataba Huru ya Kibiashara ya kikanda au ya kibara kama vile NAFTA, SADC, EAC, au  hati ya awali ya ASEAN  ambazo madhumuni yake ni kuimarisha  majadiliano  ya kikanda wakati wa majadiliano ya biashara za  kimataifa;  

5. Ingawa Afrika Kusini na India ni watia sahihi wa MLI (zana ya kimataifa inayotumika katika majadiliano ya mikataba ya kodi) ambayo wanatumia katika majadiliano ya mikataba ya kodi, Tanzania siyo mtia sahihi. Kwa kuwa mikataba mingine mipya bado inafikiriwa na MLI bado iko wazi kwa sahihi za ziada kuna hitaji la Tanzania kutia sahihi MLI ili iwe katika mlingano ulio sawa.