Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

TAMKO LA UMOJA WA WADAU WA HAKI YA KODI TANZANIA (TTJC)

UKUSANYAJI WA MAPATO YATOKANAYO NA RASILIMALI ZA NDANI, MATUMIZI, CHANGAMOTO NA MAPENDEKEZO

Serikali inalo jukumu kubwa la kuwapatia wananchi huduma bora za umma. Ili Serikali iweze kutimiza wajibu wake kwa umma inahitaji rasilimali mbalimbali, zikiwemo fedha. Kushindwa kwa serikali kukusanya mapato ya kutosha kunadhoofisha uwezo wake wa kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba Tanzania inakabiliwa na tatizo la kupoteza kiwango cha juu cha mapato hasa yanayotokana na kodi.

Mnamo mwaka 2012 Kamati ya Viongozi wa Dini ya masuala ya Haki za Kiuchumi na Uadilifu katika Uumbaji walitoa ripoti iliyobainisha, Kiwango cha upotevu wa mapato kuwa Dola za Kimarekani kati ya Milioni 847 na bilioni 1.3. Upotevu huu wa mapato ni kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia misamaha ya kodi na utoroshwaji wa fedha kwenda nje ya nchi

Hali ya sasa inaonesha kuwa upotevu wa fedha za kodi umeongezeka hadi kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 1.83, sawa na fedha za Kitanzania takribani Shilingi trilioni 4. Fedha hizi zilizopotea zingeweza kufadhili kwa mara tatu ya bajeti ya Sekta ya Afya, au mara mbili ya bajeti ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2016/17.

Licha ya utafiti uliofanyika mwaka 2017 kuonesha kuongezeka kwa jitihada katika kukusanya mapato, bado serikali inakabiliwa na matatizo kama;

  Ukwepaji wa kodi

  upotevu kwenye misamaha ya kodi

  utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi.

  Na upotevu mwingine katika manunuzi ya umma

Kuhusu misamaha ya kodi: Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2015/16 inaonesha kuwa Serikali ilitoa misamaha ya kodi ya thamani ya Shilingi trilioni 1.10, sawa na asilimia 1.14 ya pato la ndani la taifa, wakati lengo la Serikali ni kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia chini ya asilimia 1 ya pato la ndani la taifa.

Mkaguzi Mkuu alibaini kuwa misamaha ya kodi imekuwa ikitumika kuwanufaisha watu au makampuni yasiyostahili. Mfano kwa kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, magari 238 kutoka nje ya nchi yaliingizwa nchini kwa kutumia majina ya walipa kodi wawili ambao hawakustahili. Kwa mwaka 2015/16 Serikali ilipoteza shilingi billioni 3.46 kwa kutoa misamaha ya kodi kwa watu wasiostahili.

Kuhusu utoroshwaji wa fedha: Viwango vipya vya upotevu wa mapato yatokanayo na utoroshwaji wa fedha nchini kwenda nje ya nchi ni Dola za Kimarekani milioni 464 kwa mwaka.

Kuhusu manunuzi ya umma: Mwaka 2015/16, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alibaini mapungufu katika utaratibu wa utoaji wa zabuni, na utekelezaji na usimamizi wa mikataba na manunuzi ambayo hayakufanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zake. Kutofuatwa kwa kanuni hizi ni kiashiria kikubwa cha upotevu wa fedha kwa njia badhilifu.

Kuhusu ukusanyaji wa kodi: Imebainika kwamba watu wachache sana, hasahasa walio kwenye sekta rasmi, ndio wanaolipa kodi, hivyo kubeba mzigo wa wale wasiolipa kodi, ambao bado wanafaidi bidhaa na huduma za umma sawasawa na wale wanaolipa kodi.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali 2015/16 inaonesha kuwa takriban Shilingi 588.8 bilioni hazikukusanywa kutoka kwa walipa kodi mbalimbali.

Pia, uchunguzi uliofanyika mwaka 2015 hadi 2016 ulibaini kuwa katika walipa kodi 9,743 waliosajiliwa kukusanya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ni walipa kodi 1,578 ambao ni asilimia 16 tu ndio wanatumia mashine za EFD. Kati ya walipa kodi 49,009 wanaostahili kutumia mashine za EFD ni walipa kodi 9,127, ambao ni asilimia 18.6 tu, wenye mashine hizo.

Mapendekezo: Kupitia kongamano la “Tanzania Extractive Indutries Conference 2017,”Wadau wa Haki ya Kodi Tanzania (TTJC) tunaamini mapendekezo yafuatayo kwa serikali yanaweza kuboresha ukusanyaji na matumizi ya mapato ya fedha za umma.

  Serikali ipunguze misamaha ya kodi

  Iboreshe uwazi katika utoaji wa misamaha ya kodi

  Iendelee kuelimisha wananchi na kuwajibisha wale wote wanaohusika na ubadhilifu, au wanaokiuka sheria zinazosimamia fedha za umma.

  Isambaze na kuonesha umuhimu wa mashine za EFD, na izidi kuwekeza katika mifumo ya kielektronki ya ukusanyaji kodi, hata katika ngazi ya halmashauri

  Na pia itekeleze kwa makini suala la mapitio ya sheria mbalimbali ili makampuni yote yalipe kodi stahiki

  Wananchi watambue kuwa ni wajibu wao kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao

Kwa kufanya haya, mapato mengi yataweza kukusanywa, na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kupata huduma muhimu na kwa ubora zaidi.

Tamko hili limeandaliwa na Umoja wa Wadau wa Haki ya Kodi Tanzania (TTJC)
Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana nasi: info@policyforum.or.tz