Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UZINDUZI WA RIPOTI YA HALI YA UTEKELEZAJI WA DIRA YA MADINI YA AFRIKA

Policy Forum kwa kushirikiana na Tax Justice Network – Africa (TNJ-A), Tanzania Tax Justice Coalition (TTJC) na HakiRasilimali wameandaa uzinduzi wa kitaifa wa Ripoti ya Hali ya Utekelezaji wa Dira ya Madini ya Afrika (AMV) utakaofanyika katika ukumbi wa Bunge (Old Dispensary Hall), Dodoma  tarehe 15 Mei, 2017.  Uzinduzi  huo utaanza saa 6:30 mchana.

Dira ya Madini Afrika iliasisiwa 2009 na wakuu wa nchi za kiafrika (ikiwemo Tanzania) zenye madini kwa lengo la kuboresha uwazi, usawa na matumizi bora ya madini kwa lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo. Dira ya Madini ya Afrika (AMV) inasisitiza mabadiliko katika usimamizi wa rasilimali za madini ili kuleta tija katika kukuza uchumi na viwanda barani Afrika. 

Kuasisiwa kwa AMV kulizua mijadala mbalimbali kutoka kwa wananchi wakihoji ni  kwa namna gani faida zitokanazo na madini zitaleta mageuzi ya kiuchumi  na madhara yatokanayo na shughuli za uchimbaji madini yanawezaje kutatuliwa. Mijadala ya aina hii ilianzia kwenye jamii ambazo shughuli za uchimbaji wa madini zilianza kati ya miaka ya 1980 na 1990.

Baada ya miaka saba ya kuasisiwa kwa AMV, Tax Justice Network-Africa (TJN-A) imefanya utafiti wa kisayansi katika nchi tatu - Ghana, Tanzania na Zambia kuangalia hali ya utekelezaji wa mojawapo ya nguzo saba muhimu za AMV ambayo ni Usimamizi wa Mapato na Mifumo ya Usimamizi wa Fedha.

Utafiti huo umelenga zaidi kupima maendeleo ya utekelezaji wa AMV katika nchi zilizoazimia dira hiyo ikiwemo Tanzania. Pia, utafiti umepima ulinganifu wa mifumo ya usimamizi wa fedha pamoja na mapato katika ngazi ya kitaifa na kikanda. Ripoti ya utafiti huo imetoa mapendekezo kwa lengo la kuboresha usimamizi wa fedha na mapato yatokanayo na madini.

Mojawapo ya mapendekezo, ni kuimarisha uwezo wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ili kukabiliana na tatizo la uhamishaji haramu wa fedha kutoka kwenye sekta ya madini.

Ripoti imependekeza kuanzishwa kwa sera ambayo itanufaisha jamii zilizoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini. Mapato yatokanayo na shughuli za madini yawezesha jamii hizo kupata maji safi na salama, huduma bora za afya, elimu bora na miundombinu madhubuti.

Ripoti hiyo itazinduliwa mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na wawakilishi mbalimbali kutoka taasisi za kiserikali na wanahabari na itapatikana mara baada ya kuzinduliwa. ________________________________________________________________________

Kwa taarifa zaidi, wasiliana nasi: info@policyforum.or.tz / 0782317434