Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Kabla ya uchaguzi mkuu  wa Oktoba 25, 2015, Asasi Za Kiraia (AZAKI) chini ya Kikundi Kazi  cha Bajeti cha  Policy Forum ziliandaa na kuwasilisha kijarida kinachoitwa“Vipaumbele  Vyetu Vikuu  kwa Serikali Ijayo”  kwa  vyama mbalimbali vya siasa  vilivyokuwa vinashiriki katika uchaguzi ili kutilia mkazo yaliyomo kwenye kijitabu hicho.  Kijarida hicho kilikuwa na masuala nyeti yaliyohitaji serikali ya awamu ya tano kuzingatia.  

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishinda uchaguzi na kuunda serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli;hivyo basi AZAKI  zinatumaini kwamba masuala waliyoibua wakati huo yatafanyiwa kazi na serikali ya awamu ya tano ambayo  siku za karibuni imetimiza siku 100 madarakani. Kutokana na yale  tuliyoyachunguza katika kipindi hiki kifupi lakini kizito, tunawasilisha tafakari na tathmini yetu kuhusu  ufanisi wa serikali mpya katika  kutekeleza  masuala ambayo tungependa yafanyiwe kazi:

Kuhusu Ukusanyaji wa Rasilimali za Ndani

Kwa kipindi kirefu, AZAKI zimekuwa na shauku ya kujua ni kwa jinsi gani Serikali inaweza kuboresha sera yake ya fedha ili kupambana na upotevu wa kodi kutokana na mfumo wa ukwepaji kodi, uepukaji kodi na uvushaji haramu unaokausha rasilimali za ndani.  Serikali mpya chini ya Rais Magufuli imeonyesha nia ya kupitia sera ya fedha. Tangu mwaka 2015 serikali imepunguza misamaha ya kodi iliyokuwa ikitolewa kwa makampuni ya madini toka  17.6% hadi 9% ya misamaha yote ya kodi inayotolewa kwa uwekezaji katika madini.  Serikali, kupitia  Waziri wa Fedha na Mipango ilitoa tamko Bungeni kwamba lengo la Serikali sasa ni kuimarisha biashara na mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji na siyo misamaha ya kodi. 

Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa mwaliko kwa wadau ikiwa ni pamoja na AZAKI kutoa maoni  yatakayosaidia katika mwenendo wa kikosi kazi cha mageuzi  katika mfumo wa  kodi, kwa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2016/17.  Mpango huu wa Serikali mpya unaonyesha utayari wake wa kuboresha sera ya fedha na hivyo kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani pamoja na kuwahusisha wadau wengine nje ya Serikali.

Ili kuboresha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji kodi, pamoja na kupunguza ukwepaji  na uepukaji kodi,   hatua za dhati zimechukuliwa  ambazo zinajumuisha kuboresha muundo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania hali iliyosababisha makampuni zaidi ya 200 ya utoaji na usambazaji bandarini kufutwa kwa kosa la kushindwa kuonyesha risiti za ulipaji kodi, na katika  miezi mitatu iliyopita TRA imeweza kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya makadirio ya mapato ya kodi.    

Hatua nyingine zinajumuisha kufukuzwa kazi mara moja kwa maafisa wa ngazi za juu wa TRA pamoja na Kamishna Mkuu, maafisa wengine kufunguliwa mashtaka mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabovu ya ofisi na kusababisha upotevu wa mapato ya umma na zaidi ya maafisa 100 wa TRA  kuhamishwa katika ofisi nyingine mikoani.

Zaidi ya hayo, katika kuhakikisha kwamba Serikali inatumia mapato ya kodi ipasavyo, tumeshuhudia hatua  za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa mfano; Serikali ilitoa mwongozo  kwa safari za nje ya nchi kwa maafisa wote wa Serikali. Kibali cha kusafiri lazima kiombwe kutoka Ikulu na safari yenyewe siyo tu iwe muhimu bali pia ithibitishwe kuwa ni ya lazima  na ya gharama stahiki. Inakisiwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni 4 zimeokolewa tangu tangazo hilo.

Hata hivyo, inapendekezwa kuwa Serikali iendelee kujenga taasisi imara zenye kanuni na taratibu thabiti kwa  hatua endelevu katika ukusanyaji wa kodi.  

Katika Afya

Sekta ya afya imeona uboreshaji mkubwa katika siku 100 za mwanzo za serikali ya sasa. Kwa hakika ni sekta mojawapo iliyopata kipaumbele kwa taasisi za afya zenye kutoa huduma muhimu kutembelewa mara kwa mara  na Rais pamoja na Mawaziri husika. Lengo lililotangazwa la ziara hizo lilikuwa kuchukua hatua dhidi ya mapungufu mengi katika mfumo – kuanzia vifaa hadi huduma kwa wagonjwa. Ziara hizo pia zilipelekea kuongeza uwajibikaji miongoni mwa watoa huduma za afya Serikalini. Hili limeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. 

Hata hivyo, hapajawa na hatua madhubuti zinazoonyesha mwelekeo au kipaumbele  cha Serikali katika utoaji wa fedha za afya, bidhaa na rasilimali watu  kwa huduma za afya. Pamoja na juhudi za Serikali za kupunguza matumizi ya umma na kuongeza ukusanyaji wa rasilimali, hakuna uhakika ni kwa kiwango gani sekta hii itapewa kipaumbele katika utolewaji wa fedha kwa mwaka wa fedha 2016/17.   Kipaumbele sasa hivi kinaelekea kuwa katika miundombinu badala ya mifumo, mipango ya  tiba  na kinga, upungufu wa rasilimali watu  na ufikiaji kati ya mambo mengine.

AZAKI pia zimepitia  Mpango wa Miaka Mitano  uliopendekezwa kuhusu  kukuza uchumi wa viwanda. Malengo  katika sekta hii ni kuhusu  MNCH (wakina mama, watoto wachanga, na afya ya watoto)  rasilimali watu na miundo mbinu, ufikiaji wa madawa na vifaa tiba  na  mipango ya bima. Mpango wa mwaka mmoja uliojadiliwa bungeni unaeleza wazi ni  huduma   zipi za afya zitapata kipaumbele katika mwaka wa fedha ujao, lakini pia unasisitiza msimamo wake kuhusu MNCH, madawa, rasilimali watu na mipango ya kuwafanya wabaki kazini.  Lakini, upatikanaji wa fedha haujachambuliwa vya kutosha, na haieleweki jinsi mipango hii itakavyogharamiwa.

Wakati wa uzinduzi wa  bunge la 11, mwaka 2015 Rais aliagiza kupunguzwa kwa bajeti iliyopangwa kwa sherehe na badala yake kutumia shilingi milioni 201 zilizopatikana kununua  vitanda kwa ajili ya hospitali ya Taifa ya Muhimbili.    

Utafiti kuhusu upatikanaji wa  madawa muhimu, vifaa tiba na  uwezo ki-vitanda uliofanywa na Sikika wa mwaka 2013 ulionyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa vitanda katika hospitali za Serikali hali iliyopelekea  wagonjwa ama kushirikiana vitanda au kulala sakafuni. Hali hii haikubaliki, hivyo  tunampongeza Rais kwa kuboresha upatikanaji wa vitanda katika hospitali za umma. 

Wana AZAKI wanapenda kumtia moyo Rais kuendelea kuhimiza ubora wa huduma za afya  kwa kuimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya bajeti ya sekta ya afya miongoni mwa wahudumu. 

Kuhusu Elimu

Mwaka  2016 ulianza vizuri kwa wazazi wenye watoto katika shule za Serikali  nchini kufuatia ahadi na agizo la serikali mpya kuhusu elimu  ya bure kama ilivyoainishwa katika Sera ya Elimu ya Mwaka 2014.  Kulikuwa na malalamishi kutoka kwa wananchi  kuhusu jinsi ilivyokuwa ghali kuweza kulipia michango yote ambayo wazazi wanatakiwa kutoa kwa ajili ya watoto wao walioko katika shule za Serikali ambazo kwa kawaida zinafikiriwa kuwa za gharama nafuu.

Tayari Serikali imetangaza wazi kuwa elimu ya bure lazima itolewe katika shule za umma kuanzia mwaka huu wa 2016.  Katika  shule ambazo agizo hili  halikuzingatiwa, tumesikia hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na Serikali. Kutokana na ongezeko la ukusanyaji wa mapato na mgao sahihi, tunaamini kuwa msimamo wa Serikali wa kutoa elimu ya bure na yenye ubora utafanikiwa.  

Ombi letu kwa Serikali ni kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu kwa kutoa kipaumbele katika bajeti ya maendeleo kuanzia Mwaka wa Fedha 2016/17. Ni kwa kuangalia mgaomga0o wa bajeti ya mwaka  2016/17   mtu anaweza kuona nia ya kweli  ya Serikali ya kutoa elimu bure pamoja na kuboresha utendaji wa sekta. Tungependa kuona walau asilimia 30 ya bajeti ya sekta ya elimu ikielekezwa katika matumizi ya maendeleo kutoka asilimia 15 ya sasa. Mgao tuliopendekeza unategemewa kusaidia katika kuondoa changamoto za sasa za miundombinu  na hivyo kusaidia kuboresha mazingira ya mafunzo.

Zaidi ya hayo, tunaisihi Serikali mpya kuhakikisha kuwa Tume ya Walimu inakuwepo kufuatia kupitishwa kwake na Bunge mwaka 2015. Hivyo ni muda muafaka sasa kwa Serikali kutimiza hitaji  hili kwani uwepo wake utasaidia katika kufanyia kazi baadhi ya changamoto za walimu nchini.

Kuhusu Haki ya Ardhi na Uhifadhi wa Misitu

Serikali mpya chini ya Rais Magufuli imeweza kutatua  migogoro ya ardhi na kurejesha ardhi kwa jamii. Mifano inajumuisha  Kapunga wilayani Mbarali pamoja na Vilima Vitatu wilayani Babati.

Baadhi ya migogoro inayohusu ardhi imetatuliwa. Hata hivyo bado kuna hitaji   la Serikali kubadilisha mbinu zake hasa wakati wa  kutafuta ufumbuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji; kwa kuangalia masuala  mapana ya kimfumo badala ya mtazamo finyu ili kuhakikisha ufumbuzi wa kudumu.   Mageuzi ya ardhi na mifumo iko tayari lakini juhudi zaidi zinahitajika katika utekelezaji wa sheria na uwajibikaji katika usimamizi wa ardhi na mgao wa bajeti kwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi (LUP).  

Katika muda huu mfupi wa mapitio haya, tumeona kuwa hakuna kilichofanyika kuonyesha msimamo thabiti kuhakikisha haki ya wanawake katika kumiliki  ardhi. Kuna sera kuhusu ardhi na usimamizi wa  ardhi lakini hakuna kitu kinachoonekana wazi kilichofanyika kuonyesha msimamo wa Serikali  kuhusu masuala ya wanawake hususan yanayohusiana na ardhi. Serikali katika siku zake 100 za awali imeweza kutatua  mgogoro wa Kapunga kule  Mbarali lakini hatuna uhakika kama kuna maagizo yoyote ya jinsi ardhi hii itakavyogawanywa na kama wanawake watapewa upendeleo.

Kuhusu Kilimo

Kimkakati, Serikali imewaita viongozi wote katika ngazi zote kuhamasisha jamii kujishughulisha na kilimo. Lakini mkakati wa wazi wa kuwezesha jamii vijijini na wanawake kushughulika kwa faida haujajionyesha kwenye kilimo. Pia  hatujaona jitihada za serikali za kutoa mikopo yenye riba nafuu  kwa masikini (wakulima wadogo na wafugaji)  na walioko pembezoni.

Pia, hatujaona mipango na misimamo yenye lengo la kushirikisha wanawake masikini na makundi mengine yaliyoko pembezoni, kadhalika hatujaona juhudi za kukuza biashara ya kilimo kwa usawa katika uwekezaji unaotegemea ardhi, pamoja na uhamasishaji ili kujenga uwezo wa wakulima wadogo  wadogo na wafugaji  kuhusu  mahitaji yanayoendana na thamani.

Hata hivyo, tunatambua na kukiri kauli ya Rais kwenye upande wa kilimo ambayo  inajali walio masikini, lakini pia ni muhimu Serikali  ihakikishe kuwa bajeti ya kilimo inafikia lengo la Azimio la Maputo  kwenye uwekezaji wa kilimo na usalama wa chakula la mwaka 2003  kwa kutenga walau asilimia 10 ya bajeti  ya nchi na kuielekeza kwenye kilimo.

Hitimisho

Ni wazi kuwa Serikali mpya chini ya utawala wa Rais  Magufuli imeonyesha utayari wa kisiasa  katika vyote viwili: hitaji la kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma, kama inavyojulikana wazi kuwa ni vigumu kuboresha utoaji wa huduma kwa umma wakati msisitizo ni katika ongezeko la rasilimali pekee bila taratibu thabiti za kuhakikisha  uwajibikaji. Siku 100 za Serikali mpya kwenye madaraka zimeonyesha kuwa inawezekana kukusanya rasilimali nyingi za ndani ambazo zinaweza kutumika kuboresha maisha ya wananchi.  Mbinu bora za kilimo zinawezekana pale tu ambapo kuna vifaa vinavyofaa; watu wana afya na  ujuzi unaohitajika kufanya kilimo cha kisasa katika ardhi ambayo haina migogoro. 

mwananchi.pdf (2.15 MB)