Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Jumuiko la asasi za kiraia zinazoshawishi haki katika kodi Tanzania, zimeipongeza serikali kwa kuandaa rasimu ya Muswada wa Kodi ya Ongezeko la Thamani wa mwaka 2014 na Muswada wa Uendeshaji wa Kodi wa mwaka 2014 wenye madhumuni ya kuelekeza uendeshaji wa kodi ya  Ongezeko la Thamani na kuunda muundo wa kisasa na wenye ufanisi wa uendeshaji wa kodi. 

Miswada hiyo miwili, inayotegemewa kusomwa kwa mara ya pili katika kikao cha bunge kitakachokaa  Novemba 2014, imefanyiwa uchambuzi na muunganiko huo  unaoamini kuwa sheria hizo zitasaidia serikali kupunguza misamaha ya kodi Tanzania, pia kurahisisha na kuunganisha taratibu zinazotokana  na sheria mbalimbali  kwa madhumuni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari, usimamizi wa kodi ulio wa haki, na kuongeza mapato ya kodi. Muhtasari wa uchambuzi huo ni kama ifuatavyo:

Muswada wa Kodi ya Ongezeko la Thamani  wa Mwaka 2014

Stahiki: Kwa kulinganisha na utaratibu wa sasa, idadi na aina  ya wahusika wenye kustahili misamaha ya kodi wamepunguzwa chini ya Muswada wa Sheria ya VAT ya mwaka 2014 wakati ambapo wawekezajiwenye vyeti  vya misamaha kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), na wawekezaji katika  miradi ya Kanda za Usindikaji wa Bidhaa kwa Mauzo Nje ya Nchi (EPZs) na Kanda Maalum za Kiuchumi (SEZs)pia na wawekezaji wenye hadhi ya wawekezaji nyeti hawatanufaika tena na misamaha ya kodi. Muswada huo unakusudia kupunguza misamaha ya kodi.

Kigezo: Jumuiko linatambuavigezo vitakavyotumika katika misamaha ya kodi sehemu ya II ya Muswada  (wa Utozaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani)  unaainisha wale ambao wanastahiki kupata misamaha kama vile Ofisi za Kidiplomasia au za Kibalozi  za Nchi za Kigeni zilizoko  Tanzania Bara kwa kigezo kama  vile (miamala kwa ajili ya matumizi   rasmi  ya ofisi  hizo)”. Lakini, kwa misamaha ya mambo muhimu kama vile elimu, afya, na kilimo hakuna vigezo  vilivyoainishwa  kwa utoaji wa misamaha hiyo.  Huu unaweza kuwa mwanya ambapo kwa kupitia muswada huu mapato kutoka VAT yanaweza kupotea kwa kukosa vigezo maalum.

Uwazi:  Ingawa Muswada unaainisha wale ambao wanastahiki msamaha, hauonyeshi ni  kwa uwazi gani taratibu  na matokeo yanatakiwa kuwa. Katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/15, Waziri wa Fedha alisema kuwa kutakuwa na uwazi wa hali ya juu katika utoaji wa misamaha.  Miongoni mwa hatua  za uwazi zilizotamkwa katika hotuba ya bajeti  yalikuwa matangazo  kwa umma (kwa kupitia; kwa mfano tovuti ya Wizara na magazeti) kwa wale wote wanaonufaika kupata msamaha kwa kila robo mwaka. Muswada uko kimya katika eneo hili.   

Mipaka ya Mamlaka  ya Waziri Kutoa Misamaha: Chini ya  “Vitu na  Sababu”, Mswada unatoa pamoja na mambo mengine, mipaka ya mamlaka ya Waziri kutoa misamaha. Inasema kwamba”.....Muswada utafuta kuondokana  na mamlaka ya Waziri kutoa misamaha katika ulipaji wa kodi ya ongezeko  la thamani”.  Hii inaendana  na kile alichokisema Waziri katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/15. Sehemu ya II ya Mswada,  katika hali hiyo , “ Inapendekeza kuondoa mamlaka ya Waziri kutoa misamaha ya kodi. Hii, kama hatua nyinginezo ina lengo la kuwezesha utabiri wa mapato  na kuendeleza msingi wa kodi usioyumba.   

Uahirishaji wa Malipo: Hakuna muda maalum wa uahirishaji uliowekwa kwa uahirishaji  wa malipo katika Muswada. Hali hii inaweza kutoa mwanya kwa wafanyabiashara kuahirisha ulipaji kodi kwa muda mrefu hivyo kuonyesha wazi hatari kwa mapato kama hayo kupotea. Itaongeza thamani  zaidi na kupunguza uwezekano wa upotevu wa mapato ikiwa Muswada utaeleza muda na mara ngapi malipo ya VAT yanaweza kuahirishwa.

Uingizaji wa maoni ya wadau wa ndani kuhusu utaratibu mzuri wa kupunguza misamaha:

Kwa ujumla  muswada umeingiza maoni mengi kiasi kutoka kwa wadau wa ndani kuhusu misamaha ya kodi. Maoni hayo hayakujumuisha tu upunguzaji au uondoaji wa misamaha ya kodi isiyo na tija ,kama vile maoni dhidi ya ushindani wa kodi kati ya nchi za ukanda wa Afrika ya mashariki unaochochea hali inayojulikana kwa wengi kama “mbio za kuelekea chini”.  Vile vile yamejumuisha maoni kwa msamaha wa VAT kwa mambo muhimu kama vile  chakula, elimu, kilimo na nyumba za kuishi na maoni ya kupunguza mamlaka ya waziri kutoa msamaha. Hata hivyo,  haijajumuisha  maoni ya kufanya taratibu za misamaha na matokeo kwa uwazi kwa njia ya kuweka katika  maeneo ya umma (mfano mbao za matangazo)  majina ya wale waliopata na kunufaika na misamaha.

Muswada wa Uendeshaji wa Kodi wa Mwaka 2014

 

Sheria za kodi kwa mabadiliko yajayo

 

 

1

Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, CAP 399

2.

Sheria ya Matumiziya Mapato ya Kodi, CAP 408

3

Sheria ya Kodi ya Mapato CAP 332

4

Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta , CAP 220

5

Sheria ya Uandikishaji wa Magari ya Kigeni, CAP 84

6

Sheria ya  Makato ya Huduma za Ndege, CAP 365

7

Sheria ya Makato ya Huduma za Bandari,  CAP 274

8

Sheria ya Mafunzo ya Ufundi , CAP 82

9

Sheria ya Uandikishaji na Uhamishaji wa Magari, CAP. 124

10

Sheria ya Wanyama Pori, CAP 41

11

Sheria ya Tozo za Stempu, CAP. 189

12

Sheria ya ushuru na forodha (Excise (Manag’nt and Tariff Act), CAP. 147

Kama ikipita,  hii itakuwa sheria pekee ya kwanza iliyotungwa kwa uendeshaji wa  sheria mbalimbali za kodi zilizoko chini ya  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu ilipoundwa mwaka 1995.  Hivi sasa, uendeshaji wa kodi unatekelezwa chini ya vifungu mbalimbali vilivyotawanyika katika sheria 12 mbali mbali za kodi.  Ni lazima kutambua  kuwa  hali hii ina uwezekano mkubwa wa kuleta ugumu katika uendeshaji, inaweza kuongeza gharama  za utekelezaji na kuchanganya  walipa kodi, hasa  wale ambao shughuli zao  zina  maingiliano  mengi  na hivyo kuangukia chini ya sheria mbalimbali za kodi.

Misamaha ya kodi: Muswada uko kimya kuhusu vipengele vingi vya motisha ya kodi ambavyo ni muhimu sana  kwa uwazi wa mapato, uwajibikaji na haki. Usiri wa kiuendeshaji katika menejimenti ya motisha za kodi huongeza  kwa kiasi kikubwa  hatari ya rushwa na tabia ya kutaka bakshishi. Kama sehemu ya uendeshaji wa kodi, muswada ungeweza kuweka  vifungu kwa ajili ya uainishaji,  uwekaji kiasi  na utangazaji   gharama za mapato  ya kodi za upendeleo (misamaha ya kodi)  ambayo ni nguzo muhimu katika uwazi wa kifedha.

Hiari/Busara ya Mamlaka ya Kamishna: Muswada una vifungu kadhaa vinavyotoa mamlaka ya hiari / busara na /au yasiyoweza kuhojiwa kwa Kamishna Mkuu.   Bila  uhakiki wa kiufanisi  (ambayo ndiyo hali halisi)  kuna uwezekano wa mianya ya matumizi mabaya ya mamlaka kujitokeza.  Kwa mfano:

Mamlaka ya Kamishna Mkuu Kutoa  Notisi ya Kiutendaji

9.-(1) Kamishna Mkuu anaweza kutoa notisi ya kiutendaji  kwa madhumuni ya kuhakikisha  ulinganifu   katika uendeshaji wa sheria za kodi na kutoa mwongozo kwa watu wanaoathirika na sheria hizo.

Muswada hauelekezi  mazingira yanayoweza kupelekea  utoaji wa notisi ya kiutendaji  na kwa hiyo  kuweza kumpa Kamishna mamlaka  ya kutumia busara/hiari  yake kutoa notisi ya kiutendaji kwa sababu  zinazoweza kuhujumu uthibiti wa vifungu vingine vya sheria husika .  Itafaa kutoa maelezo mapana ya mazingira husika.

Mgongano wa kimaslahi: Vifungu vidogo vya 5-6 vinamwezesha mtu yeyote kutoa taarifa  kwa mamlaka kuhusu  uwezekano wa kutokea  mgongano wa kimaslahi  na hatua inayotegemewa kuchukuliwa na mamlaka ya kodi, hata hivyo iko kimya kuhusu  nini kifanyike endapo kweli kuna mgongano wa  kimaslahi. Kifungu kipya kinaweza kuingizwa  ili kuongezea sifa zinazostahili..

Ukadiriaji na ukadiriaji binafsi: Mfumo wa upimaji binafsi uliingizwa Tanzania mwaka 2004  kama sehemu ya mabadiliko / marekebisho ya kodi  na ni utambuzi wa ukweli ulimwenguni kote kwamba hakuna mamlaka yoyote ya uendeshaji kodi yenye au itakayoweza kuwa na rasilimali za kutosha kutathmini deni la kodi la kila mlipa kodi.  Kifungu 46.-(1),  kwa hiyo inatoa haki ya ukadiriaji binafsi  katika kujaza marejesho ya kodi. Wakati hili linaweza  kuwa rahisi  kwa walipa kodi inaweza pia  ikatoa mwanya kwa  wasio waaminifu, jambo ambalo siyo geni kwa Tanzania.  Zaidi ya hayo Muswada, unaelekea  kushauri kwamba  ukadiriaji binafsi hutumika kwa walipa kodi wote (bila kulenga makundi maalum ya walipa kodi). Wakati hili linaweza kukubalika kwa walipa kodi, inaweza kushindwa katika kuongeza mapato. Linaloleta utata zaidi, Kifungu cha 46 (2),  hakitoi mamlaka kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa Kamishna  Mkuu kufanya marekebisho ya ukadiriaji wowote.  Kuna masuala yanayojitokeza kuhusu kifungu hiki:

-          Hiki kifungu kinaweza kuleta  hali ya kutokueleweka katika utekelezaji wake kwani kinamzungumzia Kamishna Mkuu peke yake kama mtu mwenye mamlaka ya kufanya marekebisho yoyote kuhusu ukadiriaji  na kinaweza kupingana na yaliyomo katika kifungu cha 16 (1) kuhusu mamlaka ya  Kamishna Mkuu kukasimu mamlaka. Kifungu hiki kinaweza kuimarishwa  kwa kuingiza kifungu kidogo kinachomruhusu kukasimu mamlaka hayo kwa Afisa wa kodi.   

-          Haikidhi  utumiaji wa neno “marekebisho” ili kuonyesha kama inamaanisha kwenda juu, au chini au vyote, jambo ambalo linaweza kutoa mwanya utakaotumiwa vibaya  kwa walipa kodi wasio waaminifu. Kwa ajili ya kuongeza mapato kadiri iwezekanavyo, mamlaka hayo yatumike kwa marekebisho ya kwenda chini ili kuzuia maofisa wa kodi wasitafute marekebisho ya makato ya kwenda  chini yatakayopunguza madeni ya kodi  lakini kwa gharama ya kupunguza mapato ya kodi..

Kwa uchambuzi kamilifu wa miswada hiyo miwili itakayowasilishwa kwa wabunge Dodoma tafadhali tembelea tovuti yetu:http://www.policyforum-tz.org/tax-reforms-tanzania

Bofya hapa kuona tangazo la tamko lililotoka kwenye gazeti la Mwananchi:http://www.policyforum-tz.org/sites/default/files/TGA.pdf