Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Juma lililopita, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aliwasilisha Bungeni taarifa yake ya  mwaka kuhusu mahesabu ya serikali kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2012 kufuatana na ibara ya 143  ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 34 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na: 11 ya mwaka 2008.  Taarifa inaonyesha baadhi ya masuala ambayo yanazuia ufanisi wa Serikali kuu, Serikali za mitaa, Mamlaka za umma na vyombo vingine kufikia malengo yao. Lengo kuu ni kuvuta hisia za vyombo vya  Serikali,  Watunga Sheria, Mahakama na Washirika wa Maendeleo na Umma kwa ujumla  kuhusu hali ya fedha, pia kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuondokana na mapungufu yoyote yaliyopo.

Kwa miaka sasa, Bunge limejenga utaratibu usio na dosari wa jinsi wabunge wanavyojadili  na kutoa kauli zao kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali  baada ya kuwasilishwa bungeni kufuatana na vifungu vya 34(2), 35(2), 37(3) na cha  38(1) na (2)  ya sheria ya Ukaguzi wa Umma Na: 11 ya 2008. Moja kati ya tukio muhimu ambalo litakumbukwa na vizazi vijavyo ni lile la mwezi Aprili 2012  ambapo wabunge  kutoka vyama mbali mbali walisema imetosha na kudai mawaziri wasiopungua wanane wajiuzulu kutokana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuweka wazi  suala la rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma. Hili lilikuwa ni tukio la kihistoria katika juhudi zetu za kutaka uwajibikaji na lilijenga imani na heshima  kwa bunge letu katika macho ya umma.

Kwa bahati mbaya, wakati umma unatoa pongezi na kujenga imani kwa wawakilishi wao,  Bunge halioneshi kupendezwa  na jambo hili wala kujali na kuchukulia kama jambo la kawaida  imani tuliyoipa ili itekeleze kazi kwa niaba yetu,  Bunge iko mbioni kuondoa wajibu wa walipa kodi kuamua masuala yanayohusu nchi yao. Jaribio la hivi karibuni la kurekebisha sheria ya Ukaguzi wa Umma (Hansard –Taarifa ya kikao cha Bunge cha tarehe 8 Februari, 2013), na kufutwa kwa Kamati ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma ni kati ya vitendo vya Bunge vinavyopasa kututahadharisha kuwa Bunge halipo ili kukidhi haja zetu bali haja zake binafsi. Kikundi Kazi cha Bajeti cha Policy Forum kinapenda kuwatahadharisha umma kuwa kufuatana na marekebisho  (kama yalivyopitishwa  tarehe 8 Februari 2013) kifungu cha 38 (3) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma inatakiwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali  iwasilishwe Bungeni ikiambatana na majibu ya jumla na mipango ya marekebisho yatakayoandaliwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali.  Matokeo yake, Bunge linazuiwa kujadili taarifa ya CAG hadi hapo Mlipaji Mkuu wa Serikali atakapopokea na kuunganisha pamoja majibu na mipango marekebisho ya taarifa za taasisi zote zilizofanyiwa ukaguzi. Sasa tunaona kuwa Bunge linajadili makisio ya bajeti bila kuzingatia taarifa ya Mkaguzi Mkuu wala majibu ya Mlipaji Mkuu na mipango ya utekelezaji. Lakini ni muhimu Bunge lizingatie hayo majibu na mipango ya utekelezaji kabla ya kupitisha bajeti za wizara ili kuhakiki utunzaji na usalama wa fedha za umma. 

Kwa mshangao, kana kwamba jaribio la Februari 2013 halikutosha, baada ya CAG kukamilisha matakwa ya vifungu mbalimbali vya sheria kwa kutoa taarifa yake ya ukaguzi ya mwaka 2011/2012, Bunge wakati wa kutoa taarifa fupi kwa vyombo  vya habari tarehe 4 Aprili 2013, kwa kupitia kwa Mkurugenzi Msaidizi  wa Habari, Bw. Deogratius Egidio liliwaambia waandishi wa habari kuwa “Kutokana na ufinyu wa muda na mabadiliko ya ratiba, halitajadili taarifa ya CAG katika kikao kinachoendelea cha Bunge.” (Chanzo: Alvar Mkakyusa. “Tanzania: Bunge Session Kicks Off on Tuesday in Dodoma” tarehe 9, Aprili  2013.Tovuti; www.AllAfrica.com

Sisi Wajumbe wa Kikundi Kazi cha Bajeti kutoka Asasi za Kiraia (AZAKI) tunasikitika kutaarifu umma kuwa, tumefanya kazi yetu na kwamba kutoka vyanzo vinavyoaminika taarifa ya Jumatatu ya tarehe 4 Aprili 2013 kwa vyombo vya habari haikuwa ya mzaa, taarifa ya mwaka huu ya CAG ambayo ingawa iliwasilishwa bungeni haitajadiliwa ndani ya bunge. Ingawa ulazima wa mjadala haujawekwa wazi, Kikundi Kazi cha Bajeti kinachukulia jambo hili kama ukiukwaji mkubwa wa utaratibu uliojengeka kwa miaka na ambao umekuwa ukifafanua yaliyomo katika Sheria ya Fedha za Umma, Sheria ya Ukaguzi wa Fedha za Umma na Katiba  ya kwamba BUNGE baada ya kupokea taarifa ya CAG inapaswa kujadili taarifa hiyo,  kutaka maelezo na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa. Bunge lazima lielewe kwamba huu ufafanuzi  na utaratibu umezoeleka na kukubaliwa na umma kwa mujibu wa katiba na sheria na kwamba wananchi wanahaki ya  kusikia matokeo ya Ukaguzi wa CAG.   

Ikiwa Bunge litasisitiza kutokujadili taarifa  hiyo kwa sababu zozote  zile litakalokuwa nazo, Kikundi Kazi cha Bajeti kitachukulia hali hiyo kama  usaliti kwa watu wao kitendo ambacho kitamaanisha kuondoa thamani na umuhimu  wa CAG kufanya ukaguzi wa fedha za umma kwa sababu kisheria  hana madaraka ya kuagiza hatua za kuchukuliwa kwa wanaokiuka, bunge lina madaraka na linapaswa kuwajibika kwa umma kwa hatua zinazochukuliwa.  

Uamuzi wa Kufuta Kamati ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma na Jaribio la Kurekebisha Sheria ya Fedha za Umma Na: 11 ya 2008.

Sheria ya Mahesabu ya Umma, kifungu cha 38(1) kinatoa mwongozo kwa Kamati ya Mahesabu ya Fedha za Umma, Kamati ya Mahesabu ya Serikali za Mitaa, na Kamati ya Mahesabu za Mashirika ya Umma kwamba “Lazima” zijadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  wa Serikali baada ya kuwasilishwa katika kikao cha  Bunge. Kifungu 38(2) kinasema “ baada ya kukamilika kwa mjadala” Kamati za Usimamizi wa Shughuli za  Bunge   lazima ziandae na kupeleka kwenye Mkutano wa  Bunge taarifa  ambazo zinaweza kuwa ni pamoja na maoni na mapendekezo. Kwa kusoma maelekezo haya kwa makini na kuyaoanisha na kile ambacho Bunge limefanya mwaka huu, ni wazi kifungu cha 38 cha sheria Na 11 ya mwaka  2008  kimekiukwa. Sasa, kutokana na mabadiliko hayo , hakuna atakayejadili taarifa hiyo, si Kamati ya Usimamizi wa Shughuli za Bunge wala Bunge lenyewe. 

Hata hivyo, uamuzi wa hivi karibuni wa Spika wa Bunge, Mh. Anne Makinda kutangaza kufutwa kwa Kamati ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha shughuli zake na zile za Kamati ya Mahesabu ya Umma (PAC), ni wazi kuwa ni ukiukwaji wa kifungu cha 38 cha sheria ya  msingi ya Ukaguzi ambayo inatambua na kutoa madaraka kwa POAC. Hali hii itapelekea haki isitendeke na Kikundi Kazi cha Bajeti kinaongezea mashaka ya CAG ya kwamba PAC haitaweza kutekeleza hata nusu ya shughuli zake kutokana na haya mabadiliko. Kwa mujibu wa  CAG, Bw. Ludovic Uttouh, kuunganisha shughuli za kamati za bunge za POAC na PAC kunamaanisha kwamba PAC haitaweza kutekeleza shughuli zake za usimamizi kwa ufanisi kwa kuwa italemewa na mzigo wa kazi. Alisema kuwa kuunganisha PAC na POAC haukuwa uamuzi mzuri kwa sababu hata kabla ya kuziunganisha PAC tayari ilikuwa ina kazi nyingi. “Hali ya huko nyuma hadi sasa inaonesha kuwa PAC ilikuwa na wakati mgumu kukamilisha majukumu yake  kila mwaka sasa tunapoongeza mashirika ya umma juu yake, nadhani itahitaji miujiza iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi,” taarifa zinasema.

Kikundi Kazi cha Bajeti (BWG) kinapendekeza kuwa POAC irejeshwe na kwamba Bunge sharti litafute muda wa kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali  (CAG).  Tunaelewa kuwa madaraka ya CAG yanaishia katika kutoa maoni na mapendekezo. Bunge ndiyo chombo pekee kilicho huru na chenye madaraka siyo tu ya kujadili na kuchambua bali ya kuagiza na kuchukua hatua dhidi ya serikali. Ni budi kutokukimbia wajibu wake.