Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Sisi, Kamati ya Viongozi wa Dini kwa Masuala ya Kijamii, Uchumi, Haki na Uhifadhi wa Mazingira na Maumbile na wanachama wa Policy Forum, tuliokutana katika Mkutano Mbadala wa masuala ya Madini mjini Arusha tarehe 20 Oktoba 2011, tumejadili kwa kina madhara yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa madini katika jamii zionazoishi karibu na migodi ya madini na kwa mazingira, na tunaiomba serikali na Bunge kuhakikisha kuwa zinatekeleza kwa dhati majukumu yao kwa kuhakikisha kuwa haki za wananchi ambao hawajanufaika na shughuli za uchimbaji wa madini licha ya shughuli hizo kuwadhulumu ardhi yao walioirithi kutoka kwa mababu zao, zinalindwa na kuheshimiwa.
Wajumbe wa mkutano huu pia waliazimia masuala yafuatayo:


• Ni muhimu utafiti na taarifa za madhara kwa mazingira na jamii kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini zinaandaliwa na taasisi au wataalamu wanaoaminika na kuheshimika ambao wako huru kufanya kazi zao bila kuingiliwa na serikali na wawekezaji binafsi. Utafiti huo ufanywe mara kwa mara wakati shughuli za uchimbaji zinaendelea na baada ya shughuli hizo kusitishwa. Ni muhimu shughuli hizo zikafanywa na taasisi zinazojitegemea ambazo hazitaegemea upande wowote ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wote;
• Ni dhahiri kuwa uharibifu wa mazingira kutokana na uchimbaji wa madini utaathiri pia vizazi vijavyo, na unaweza kuzisababishia jamii hizo kuishi maisha ya dhiki na mashaka. Kutokana na hilo, ni lazima kufanya utafiti kuhusu madhara yote ambayo yanaweza kutokea siku zijazo kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini na kuhakikisha kunakuwa na njia za kuwafidia ipasavyo watu wote watakaoathirika;
• Kwa hiyo tunapendekeza kuwe na utaratibu ambao ni endelevu na unaojitegemea ambao utahakikisha jamii maskini kwenye maeneo ya machimbo ya madini zinawezeshwa pia kujadiliana na kampuni za madini katika uwanda sawa;
• Pamoja na hilo, pia tunaihimiza serikali kuhakikisha inatekeleza kanuni za uchumi na haki za kijamii katika kukadiria mgawanyo na matumizi ya fedha kutokana na shughuli hizi;
• Tunaitaka serikali yetu kufanya mabadiliko kadhaa, kama vile kuanzisha sheria ya uwazi katika sekta ya Uziduaji (EITI) ili kuhimiza utawala bora katika sekta hii. Taratibu za kujadili mabadiliko haya yahusishe pia Asasi za Kiraia ambazo zinapaswa kupewa taarifa na nyaraka muhimu katika muda wa kutosha ili kuwawezesha kushiriki vema katika mijadala;
• Mfumo wa kisheria uliopo sasa katika sekta ya uziduaji ni dhaifu hasa kuhusiana na uwezo wake kusimamia sekta hii muhimu na mfano mzuri ni Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo, pamoja na mambo mengine, imetoa nguvu nyingi kwa Waziri. Bunge, kama taasisi ya kusimamia shughuli za serikali, pia liimarishwe na kuliwezesha kutunga sheria nzuri, na kuimarisha mahusiano baina ya kamati zake mbalimbali na wadau. Vile Vile, Bunge liwezeshwe kufuatilia kwa kina mapato yanayoingia katika bajeti ya taifa na ukaguzi wa matumizi yake. Hili linawezekana kupitia mafunzo ya kina na uwezeshaji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na Asasi za Kiraia.
• Jamii zinazoishi karibu na migodi ya madini, pamoja na wale ambao wameondolewa kwenye maeneo yao ya asili kupisha uchimbaji madini, mara nyingi wamekuwa wakisahaulika na kuna haja ya kuhakikisha kuwa nao wanafaidika na shughuli hizi kwa kuwezeshwa katika kujenga maisha yao. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa inazuia kila aina ya uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati watu wanapohamishwa kutoka katika maeneo yao ya asili kupisha uchumbaji wa madini. Uhamishaji huu wakati mwingine hauzingatii masuala ya kitamaduni za jamii husika. Tunaomba serikali kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha ulinzi wa haki za kimazingira, kiuchumi, kijamii na kitamaduni za jamii zilizoathirika na uchimbaji wa madini.
• Uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji madini unaathiri sana jamii katika maeneo ya uchimbaji na nchi nzima kwa jumla, lakini jukumu la kurekebisha mazingira haya linaachwa kwa serikali na si kwa wachimbaji. Kampuni za uchimbaji madini zinapaswa kuwa na jukumu la kurekebisha na kutengeneza mazingira bora baada ya kukamilika kwa shughuli zao. Sisi tupo tayari kusaidia kuhakikisha utekelezaji mzuri wa ‘Kanuni ya Mchafuaji Analipa' ambayo inapaswa kuwa na kipengele kinachowapa jukumu wachimbaji wa sasa na wa zamani kuhakikisha wanatengeneza mazingira yote yaliyoharibiwa kutokana na shughuli zao;
• Serikali pia itoe ufafanuzi wa kina na wa kueleweka katika suala la fidia, kwa kuainisha kiwango mahsusi cha fidia kwa watu na jamii ambazo zimeathirika na sumu zinazotokana na shughuli za uchimbaji wa madini na uharibifu wa mazingira yao;
• Serikali ihakikishe kuwa ni lazima jamii zinapewa taarifa muhimu na kuwezeshwa kushiriki kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuwa suala hilo liwekwe kwenye sheria na si hiari kutokana na matakwa ya makampuni au serikali.