Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Midahalo ya umma iliyofanyika chini ya mradi wa Raia Makini imebainisha changamoto kubwa zinazowakabili wananchi katika upangaji na utekelezaji wa bajeti za serikali za mitaa, huku ikiongeza utayari wa wananchi kushirikiana na viongozi katika usimamizi wa rasilimali za umma. Midahalo hiyo imeonesha wazi kuwa wananchi wanapopewa taarifa sahihi na nafasi salama ya kujieleza, wako tayari kuuliza maswali, kudai uwajibikaji na kuchangia kwa njia chanya maendeleo ya maeneo yao.

Midahalo hiyo iliandaliwa na Policy Forum na Wajibu kwa kushirikiana na asasi za kiraia ilifanyika kati ya tarehe 17 na 28 Novemba 2025 katika maeneo ya mradi yaliyopo Katavi, Dodoma, Lindi na Zanzibar. Ilikutanisha wananchi, viongozi wa vijiji na Shehia, Vinara wa Uwajibikaji (CACs) wapatao 142 (57 wanawake na 85 wanaume), asasi za kiraia pamoja na viongozi wa serikali za mitaa kujadili kwa uwazi masuala ya usimamizi wa fedha za umma na changamoto za utoaji wa huduma.

Kwa jumla, midahalo kumi na nne ya ngazi ya kijiji na mjadala mmoja wa ngazi ya wilaya ilifanyika na kuwafikia takribani wananchi 1,755, ambapo wanawake walikuwa sehemu kubwa ya washiriki. Midahalo hiyo ilichagizwa na ngoma za asili, maigizo na nyimbo, jamii zilitafakari nafasi yao katika maendeleo, umuhimu wa kuhudhuria mikutano ya kijiji, kushiriki katika mchakato wa bajeti na miradi ya maendeleo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na serikali.

Katika Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi, wakazi wa vijiji vya Luchima na Ilalanguru walitumia midahalo hiyo kuuliza jinsi vipaumbele vya maendeleo ya maeneo yao vinavyojumuishwa katika bajeti za halmashauri na kudai uwazi zaidi katika matumizi ya fedha za umma. Washiriki walionesha uelewa kuhusu mzunguko wa bajeti na waliomba taarifa za bajeti zilizorahisishwa zitolewe mara kwa mara katika ngazi ya kijiji ili kuwezesha ushiriki wenye maana.

Washiriki pia walieleza wasiwasi mkubwa kuhusu ubora na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ikiwemo matengenezo ya barabara na ujenzi wa zahanati ya Luchima ambao haujakamilika.

Hoja kama hizo ziliibuliwa pia katika wilaya za Bahi na Mpwapwa mkoani Dodoma, ambako wananchi waliomba nakala rahisi na zinazosomeka za nyaraka za bajeti pamoja na utoaji wa taarifa za matumizi ya fedha za miradi kwa wakati. Maombi haya yalielekezwa kwa viongozi wa serikali za mitaa, wakihimizwa kutumia mbao za matangazo na njia nyingine za mawasiliano ya kijamii kuwafahamisha wananchi mara kwa mara.

Katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kupungua kwa mahudhurio ya mikutano ya vijiji kuliibuka kama changamoto kubwa. Wananchi walieleza kuwa kushindwa kuona mapendekezo yao yakijumuishwa kwenye mipango na bajeti kwa muda mrefu kumewakatisha tamaa na kupunguza ushiriki wao. Changamoto za muda mrefu kama migogoro ya mipaka na migongano kati ya wakulima na wafugaji nazo ziliibuliwa, hali iliyosababisha viongozi wa wilaya kuahidi kuzifuatilia na kushirikisha mamlaka husika.

Mijadala iliyofanyika katika vijiji vya Michenga na Likunja wilayani Ruangwa ilivutia idadi kubwa ya wananchi, ambao walihoji ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo na kuomba usimamizi madhubuti wa mapato ya vijiji. Viongozi wa halmashauri walitumia fursa hiyo kueleza kalenda ya upangaji na uidhinishaji wa bajeti na kuhimiza jamii kushiriki katika hatua zote za mchakato, badala ya kusubiri wakati wa utekelezaji pekee.

Zanzibar, mijadala iliyofanyika Bububu, Kama, Mkwajuni na Mkokotoni ilijikita katika uwajibikaji wa viongozi wa Shehia na umuhimu wa kutoa mrejesho wa wazi na wa mara kwa mara kuhusu mipango ya maendeleo. Maigizo yalichangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha dhana za utawala na kuhamasisha ushiriki mpana zaidi, hususan kwa wanawake na watu wenye ulemavu.

Katika ngazi ya wilaya, mdahalo wa umma uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika uliwakutanisha wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na vyombo vya habari kujadili ushiriki wa wananchi katika mipango na bajeti. Ingawa mijadala ya vijiji haikuweza kufanyika kutokana na vikwazo vya kiutawala, mdahalo huo ulionesha wazi shauku kubwa ya wananchi kushirikishwa zaidi katika maamuzi ya bajeti.

Kwa ujumla, uwazi na uwajibikaji vilijitokeza kama mada kuu katika maeneo yote. Wananchi walieleza wasiwasi kuhusu ukosefu wa taarifa za mapato na matumizi ya vijiji, madai ya usimamizi mbovu wa mikopo ya asilimia kumi ya halmashauri na mifumo dhaifu ya mrejesho kati ya viongozi na jamii.

Kwa jumla, midahalo ya Raia Makini imekusanya taarifa muhimu kuhusu vipaumbele na changamoto za wananchi ambazo zitatumika katika hatua za ufuatiliaji, uchechemuzi na ushirikiano na mamlaka husika. Ingawa midahalo hiyo imefichua changamoto zilizopo kwenye maeneo husika, pia imeonesha kwa uwazi kuwa wananchi wako tayari na wana uwezo wa kushiriki kikamilifu wanapopewa taarifa, majukwaa jumuishi na fursa halisi ya kusikilizwa.