Vinara wa Uwajibikaji (Community Accountability Champions – CACs) kutoka wilaya za Tanganyika mkoani Katavi na Mpwapwa mkoani Dodoma wamejengewa uwezo kupitia mafunzo maalum yaliyoratibiwa chini ya mradi wa Raia Makini, unaotekelezwa na Wajibu – Institute of Public Accountability kwa kushirikiana na Policy Forum, kwa ufadhili wa pamoja kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Mafunzo haya yalilenga kuwawezesha vinara kuelewa kwa undani mfumo wa O&OD (Opportunities and Obstacles to Development), pamoja na nafasi yake katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo yao. Washiriki walijifunza kuhusu chimbuko la mfumo wa O&OD, changamoto za mfumo wa awali, maboresho yaliyofanyika, na faida za mfumo ulioboreshwa, ambao kwa sasa unasisitiza zaidi ushirikishwaji wa wananchi na matumizi ya takwimu katika kupanga maendeleo.
mfumo wa O&OD ambao chimbuko lake ni ibara ya 145 na 146 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya waka 1977 ulianzishwa mwaka kwa lengo la kuweka utaratibu wa kuandaa mipango ya maendeleo unaotoka kwa wananchi wenyewe. Hata hivyo, utekelezaji wa awali ulikumbwa na changamoto kadhaa kama vile upungufu wa rasilimali, ushiriki mdogo wa wananchi, na ukosefu wa uratibu mzuri kati ya jamii na viongozi wa vijiji au kata. Ndiyo maana serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, iliboresha mfumo huo na kuanza kutumia rasmi mwaka 2019 ili kuongeza uwazi, ushirikiano na uwajibikaji katika kupanga maendeleo.
Hadi sasa, ushiriki wa wananchi katika michakato ya mipango na bajeti nchini Tanzania, hasa katika ngazi za msingi, bado unakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo kuhusu majukumu yao, upatikanaji hafifu wa taarifa za bajeti, pamoja na ukosefu wa mifumo thabiti ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma. Ripoti mbalimbali za uwajibikaji wa kijamii zinaonyesha kuwa bado kuna mwanya mkubwa kati ya viongozi wa serikali za mitaa na wananchi, jambo linalochangia baadhi ya miradi ya maendeleo kutotekelezwa kwa ufanisi au kukosa uwazi katika matumizi ya fedha.
Ni katika muktadha huu ambapo mradi wa Raia Makini umeendelea kujenga uwezo wa wananchi kupitia vinara wa uwajibikaji, ili waweze kushiriki kwa uelewa mpana katika michakato ya mipango na bajeti, na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Katika mafunzo haya, vinara pia walipewa uelewa kuhusu muktadha wa kisheria wa Mipango na Bajeti nchini Tanzania, ikiwemo mfumo wa Serikali za Mitaa na mpangilio wake, ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa namna michakato hiyo inavyotekelezwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za kitaifa.
Baada ya mafunzo, vinara wametakiwa kutekeleza maazimio matatu muhimu: kushiriki kikamilifu katika mikutano ya vijiji, kushiriki katika michakato ya uandaaji wa mipango na bajeti, na kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kupima kiwango cha uwajibikaji katika utekelezaji wake.
Kupitia hatua hii, mradi wa Raia Makini unalenga kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji wa kijamii, kuongeza ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya maendeleo, na kuhakikisha matumizi ya rasilimali za umma yanaendana na vipaumbele vya jamii husika. Hatua hii ni sehemu ya juhudi endelevu za kujenga Tanzania yenye wananchi wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo endelevu.
Kupitia mradi huu, vinara wengine kutoka Kilwa, Ruangwa, Bahi, Mpimbwe, Unguja Kaskazini, na Mjini Magharibi walijengewa uwezo kwa nyakati tofauti.