Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

WAJIBU na Policy Forum imezindua  Ripoti za Uwajibikaji kwa mwaka wa fedha 2023/24 katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha utawala bora, kuongeza uwazi na kupambana na rushwa, ubadhirifu na udanganyifu katika usimamizi wa fedha za umma. Tukio hili liliandaliwa kupitia mradi wa Kuwawezesha Wananchi kwa Ajili ya Kuimarisha Usimamizi wa Fedha za Umma na Ukuaji Endelevu wa Tanzania Kwa kifupi Raia Makini, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi, wakiwemo wawakilishi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, asasi za kiraia, mashirika ya maendeleo na waandishi wa habari.

Mgeni rasmi Ndugu John Kabale, Mkurugenzi Msaidizi ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Ndugu Ciprian Chalamila. Katika salamu zake, alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila kuwapo kwa uwajibikaji thabiti na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma. Alieleza kuwa ripoti kama hizi ni silaha muhimu kwa taasisi kama TAKUKURU katika kuzuia, kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka na fedha.

Katika hotuba yake kama mtoa mada mkuu wa tukio, Jaji Mstaafu Robert Makaramba alitoa mchango wenye uzito mkubwa kwa mjadala wa uwajibikaji wa kitaifa. Alisema kuwa demokrasia ya kweli haiwezi kustawi bila uwazi katika matumizi ya rasilimali na bila uwezo wa wananchi kuhoji matumizi hayo. Alisisitiza kuwa uhusiano kati ya ufanisi wa huduma za umma na nidhamu ya matumizi ya fedha ni jambo lisilohitaji mjadala, na kwamba ni wakati sasa kwa taasisi zote zianze kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi kwa vitendo.

Ripoti zilizoandaliwa na WAJIBU na Policy Forum ni zao la uchambuzi wa ripoti 21 za CAG zilizowasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 Machi 2025, na kisha kwa Bunge tarehe 16 Aprili 2025. Kati ya ripoti hizo, sita zilikuwa ripoti kuu za ukaguzi wa hesabu, zikiwemo taarifa za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, Miradi ya Maendeleo, TEHAMA, na Tathmini ya Utendaji, na nyingine 15 zilikuwa ripoti za Ukaguzi wa Thamani ya Fedha (Performance Audits).

Ripoti hizo zilionesha changamoto sugu zinazojirudia kila mwaka. Miradi mingi ya maendeleo haikukamilika kwa wakati, taratibu za ununuzi wa umma zilikiukwa au kupuuzwa, usimamizi wa mikataba ya ujenzi na manunuzi ulikuwa dhaifu, na ukusanyaji wa mapato ulikuwa duni huku fedha nyingi zikicheleweshwa kupelekwa benki. Pia ilibainika kuwa kuna ongezeko la mikopo kuliko kiwango kilichoidhinishwa na Bunge, jambo linalohatarisha uthabiti wa fedha za umma.

Katika jitihada za kuhakikisha taarifa hizi za kiukaguzi zinaeleweka kwa wananchi, WAJIBU na Policy Forum walizichambua na kuzitafsiri kwa lugha nyepesi na rafiki, na kisha kuandaa ripoti tatu za uchambuzi. Ripoti ya kwanza ilihusu Usimamizi wa Fedha za Umma, ikieleza viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu kama vile makusanyo kufanyika nje ya mifumo rasmi na kuchelewa kuwasilisha fedha benki. Ripoti ya pili ilihusu Uwekezaji katika Sekta ya Umma na Biashara, ikibainisha changamoto kama hasara za kudumu katika mashirika ya umma, ukosefu wa tathmini endelevu ya miradi, na utawala duni. Ripoti ya tatu ilichambua hali ya utoaji wa huduma za jamii katika sekta za afya, elimu na maji. Ilionesha upungufu mkubwa wa dawa, watumishi, miundombinu ya shule na vifaa vya msingi, huku baadhi ya fedha zilizotengwa kwa huduma hizo zikiwa hazikutumika kabisa.

Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU FCPA Ludovick Utouh alieleza kuwa kazi yao haijaishia kuzindua ripoti, bali ni mwanzo wa mchakato mpana wa kuifikisha taarifa kwa wananchi kupitia midahalo ya kijamii, warsha, vipindi vya redio na televisheni, na vikundi vya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha kama PETS. Alisisitiza kuwa wananchi wanahitaji kujengewa uwezo wa kutumia taarifa hizi ili kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao na taasisi za umma.

Tukio hili lilihitimishwa kwa uzinduzi rasmi wa ripoti hizo na mgeni rasmi, ambaye alieleza kuwa mafanikio ya kazi ya ukaguzi hayawezi kuonekana kwa macho hadi pale wadau wote ikiwemo wanasiasa, watendaji wa umma, wabunge, wanahabari, na wananchi, watakaposhiriki kikamilifu katika kutekeleza mapendekezo. Tanzania inaweza kufikia maendeleo endelevu iwapo itaweka msingi imara wa usimamizi wa rasilimali.

Ripoti hizi, kwa pamoja, zimewekwa kama dira ya kujenga taasisi za umma zenye uwajibikaji wa kweli, na taifa linalojenga mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho.