
Taasisi ya WAJIBU – Institute of Public Accountability kwa kushirikiana na Policy Forum, imezindua rasmi mradi mpya unaolenga kuimarisha ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa fedha za umma, kupitia juhudi za kuongeza uwazi, uwajibikaji na kupambana na rushwa nchini Tanzania.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU, Ludovick Utouh, alieleza kuwa mradi huo unaoitwa “Empowering Citizenry Agency for Strengthened Public Financial Governance and Sustainable Growth in Tanzania” – kwa jina maarufu “Raia Makini Project”, umelenga kuwajengea wananchi uwezo wa kuwa washiriki mahiri na wachukua hatua katika kusimamia rasilimali za taifa.
“Mradi huu umeandaliwa kwa msingi kwamba ili tuwe na usimamizi bora wa fedha za umma, tunahitaji wananchi wenye taarifa, uelewa na uwezo wa kushirikiana na Serikali katika kusimamia matumizi ya fedha, kudai uwajibikaji na kupinga rushwa,” alisema Utouh.
Mradi wa Raia Makini unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (European Union Commission), kama sehemu ya jitihada zao za kuunga mkono utawala bora barani Afrika. Kupitia ufadhili huo, WAJIBU na Policy Forum wamejipanga kuandaa na kusambaza taarifa rahisi kuhusu usimamizi wa fedha za umma, kwa lengo la kuwapa wananchi na wadau maarifa yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika mijadala ya sera na midahalo ya umma.
Mradi huu, ambao umeanza kutekelezwa mwaka 2025 utakamilika mwaka 2027, utafanyika katika mamlaka za serikali za mitaa zifuatazo: Bahi DC, Mpwapwa DC, Lindi MC, Kilwa DC, Ruangwa DC, Mpimbwe DC, na Tanganyika DC.
Kwa jumla, mradi huu una bajeti ya TZS bilioni 2.64, na utafanyika kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo asasi za kiraia (AZAKI), mashujaa wa uwajibikaji ngazi ya jamii (Community Accountability Champions – CACs), vyombo vya habari, pamoja na taasisi za serikali katika ngazi tofauti.
Naye Semkae Kilonzo, Mkurugenzi Mtendaji wa Policy Forum, alieleza kuwa mafanikio ya mradi huu yanategemea sana mshikamano na mshirikiano baina ya wadau mbalimbali.
“Tunashukuru kwa uhusiano imara uliopo kati ya AZAKI, vyombo vya habari, na serikali. Mradi wa Raia Makini ni fursa muhimu ya kuchochea uwazi na uwajibikaji nchini – na tunatarajia kuona mabadiliko ya kweli kupitia ushiriki wa wananchi wenye uelewa,” alisema Kilonzo.
Malengo Mahususi Matatu ya Mradi:
- Elimu kwa Umma: Kuzalisha na kusambaza taarifa kwa lugha nyepesi kuhusu fedha za umma ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuhamasisha ushiriki wao kwenye majadiliano ya kisera.
- Uwezeshaji wa Wadau: Kuimarisha uwezo wa AZAKI, wanahabari, na makundi mengine ya uangalizi ili waweze kushiriki kwa ufanisi katika kudai uwajibikaji.
- Ushirikiano wa Kisekta: Kuleta pamoja asasi za kiraia, vyombo vya habari, na wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa maamuzi katika majukwaa ya kitaifa na ya wilaya.
Mradi huu utawanufaisha wananchi wa kawaida, Bunge na Baraza la Uwakilishi Zanzibar, vyombo vya habari, taasisi za serikali, mamlaka za serikali za mitaa, pamoja na vyombo vya ufuatiliaji kama TAKUKURU na ZAECA.
Katika ujumbe wake wa kuhitimisha, Utouh alisisitiza kuwa huu si mradi wa taasisi moja bali ni jukwaa la mabadiliko chanya kwa Tanzania nzima.
“Kwa ushirikiano kati ya AZAKI, Serikali, vyombo vya habari na wananchi, tunaweza kuleta mageuzi yenye tija na usawa. Rushwa ni adui wa haki, uwajibikaji ni kichocheo cha maendeleo yetu,” alihitimisha kwa msisitizo.