Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

‘Ushindi dhidi ya Corona kuanzia ngazi ya jamii’

UTANGULIZI

Sisi wanachama wa Policy Forum kupitia kikundi kazi cha Tawala za Serikali za Mitaa tumekuwa na jukumu la kushawishi sera za Kitaifa juu ya ugatuzi wa madaraka ki-utawala bora, maboresho ya Serikali za Mitaa na kuinua sauti za wananchi kwenye masuala na michakato ya umma,

Baada ya kufanya mapitio ya hali halisi ya kuenea kwa kasi kwa virusi vya Corona na kuongezeka kwa wagonjwa wa COVID -19 na baadhi yao kufariki,

Tukiwa na ufahamu juu ya madhara kwa binadamu na taathira kwa uchumi wa dunia na nchi yetu uliosababishwa na mlipuko wa COVID -19,

Pamoja na kutambua juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha udhibiti wa majanga chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dr John Pombe Magufuli kwa kuweka mpango, kuunda timu ya kitaifa na kutenga rasilimali kwa ajili ya mapambano dhidi ugonjwa wa COVID-19,

Tukiwa na uelewa   juu ya nafasi na  wajibu wa  Serikali za Mitaa kama ambavyo imefafanuliwa ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Ibara ya 145 na 146 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 287 na Sura 288 ya mwaka 1982 toleo la mwaka 2000 ambapo pamoja na kupeleka madaraka kwa wananchi, zinapaswa kuhakikisha utekelezaji wa sheria, kuimarisha ulinzi na demokrasia ili kuharakisha maendeleo katika maeneo yao.

Tumeona ni vema kutumia nafasi yetu kama wana AZAKI wenye wajibu na nafasi kwa mujibu wa sheria ya NGOs ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019 kuisaidia Serikali katika kuwafikia na kuwatetea wananchi hasa waliopo vijijini na pembezoni mwa mfumo mkuu wa uchumi ambao wengi wao wanaratibiwa na Serikali za Mitaa,

Tumeamua kwa pamoja kuandika tamko hili ambalo ni uchambuzi wa hali halisi ya COVID -19, juhudi zilizofanyika, changamoto zilizodhihirika na hatimaye mapendekezo yetu yatakayosaidia kuimarisha juhudi za Serikali za Mitaa kwenye mapambano dhidi ya covid-19.

UCHAMBUZI WA HALI HALISI YA COVID-19

Kwa takribani miezi sita sasa, Dunia imekumbwa na  janga la mlipuko na kusambaa kwa virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu. Virusi hivi vilianzia nchini China katika mji wa Wuhan mwezi wa 12, 2019 na kusambaa kwa kasi kubwa Duniani. Hadi kufikia Mei 15, 2020, Dunia nzima ilikua na maambukizi 4,643,825 na kuandika rekodi ya vifo 309,927 sawa na 6.8%. Hata hivyo, kuna habari njema kwamba kati ya waliombukizwa,wapo waliopona ambao idadi yao ni 1,631,955  sawa na 35% na wengine 58.2% waliendelea na huduma ya matibabu. Ikumbukwe kwamba tangu tarehe 11 Machi, 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza Covid 19 kuwa ni janga la Kimataifa. Sababu zilizopelekea ni pamoja na Covid 19 kuwa na asili ya maambukizi yenye mtapakao wa haraka/spidi na mpana katika sehemu mbalimbali duniani ndani ya wiki chache tu, vifo vya mapema na haraka, kulemewa kwa huduma za afya na hatari ya kupata maambukizi kwa wataalam wa afya, kufubaza uchumi kwa kila sekta ikiwemo usafiri wa anga, viwanda, huduma, kilimo usindikaji nk.

Ugonjwa wa Corona (COVID-19) ulitangazwa rasmi kuingia nchini Tanzania mnamo tarehe 16 Machi, 2020 kupitia wasafiri walioleta maambukizi kutoka  nje ya nchi (imported case). Hadi kufikia Aprili 9, 2020, Tanzania Iliingia hatua ya maambukizi ya ndani kwa ndani (local transmission phase). Ilipofika tarehe 7 Mei,2020, kulikua na jumla ya watu 509 waliombukizwa, vifo 21 na waliopona 178.

Japokuwa janga hili linaathiri zaidi afya na ustawi wa binadamu, pia limeathiri uchumi, sekta ya elimu, afya, ajira, uzalishaji, biashara pamoja na siasa. Kwa mfano, Kitaifa, janga hili limepelekea Serikali kusimamisha shughuli za michezo, safari za kimataifa na kufunga shule kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu. Kutokana na umuhimu wa tahadhari na kuenea kwa hofu, baadhi ya watu pia wamefunga maofisi yao binafsi na wengine kufunga maduka na shughuli nyingine za kibiashara.

Janga hili pia limedhoofisha  utekelezaji wa Mipango ya kimaendeleo Kimataifa, Kikanda na Kitaifa ikiwemo  Ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (hasa lengo namba 3 lililojikita kwenye Afya na Ustawi), Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025) kupitia Mpango wa Pili wa  miaka mitano ya Maendeleo ya Taifa (FYDP II ,2016/17-2020/21.)

Ni wazi kwamba mlipuko wa Ugonjwa wa Corona (COVID-19) umetikisa Mamlaka zote 185 za Serikali za Mitaa ambazo ndio ziko jirani zaidi na wananchi kwa maisha ya kila siku. Halmashauri hizi zimekuwa zikiweka jitihada za kupamabana na Janga la Corona kwenye maeneo yao kwa njia mbalimbali hususan usimamiaji wa utekelezaji wa maelekezo kutoka Serikali Kuu; hii imejidhihirisha katika kuweka vifaa kinga katika maeneo mbalimbali ya umma kama vile ndoo, sabuni na maji. Pamoja na jitihada hizo kufanyika, bado Halmashauri zimeonekana kuelemewa kutokana na sababu mbalimbali kama vile za ki muundo, upungufu wa rasilimali fedha na changamoto za miundombinu na upatikanaji wa vifaa kinga kwenye Hospitali, Vituo Vya Afya na Zahanati za maeneo yao.

JITIHADA ZA SERIKALI NA WADAU KATIKA KUPAMBANA NA COVID- 19.

Sisi kikundi kazi cha Tawala Serikali za Mitaa cha Policy Forum (LGWG) tunatambua  juhudi mbali mbali za Serikali na wadau wake katika kupambana na ugonjwa huu wa COVID 19 nchini, kama ifuatavyo,

 1. Kuundwa kwa kikosi kazi cha kukabiliana na mlipuko wa Corona (National Response Task Force) kinachojumuisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali nchini chini ya Mwenyekiti ambaye ni Mganga Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti Mwenza ambaye ni mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuratibu shughuli zote na kushauri juu ya mbinu za kutumia katika kukabiliana na janga hili la Covid -19
 2. Kusitishwa kwa mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii ili kuepuka ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona.
 3. Kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
 4. Wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi kutoa misaada ya kifedha na  vifaa vya usafi na kujikinga na maambukizi.
 5. Kufungwa kwa  shule zote kuanzia ngazi ya awali mpaka elimu ya juu (chuo kikuu)
 6. Kusitishwa kwa shughuli za kitaifa kama vile Mbio za Mwenge wa Uhuru na kusimamisha sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani na kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya jukumu hilo zitumike kusaidia hatua za kukabiliana na janga la virusi vya Corona.
 7. Kuendelea kuelimisha wananchi kwa kutoa matamko mbalimbali kupitia vyombo vya habari, na hata mitandao ya kijamii jambo ambalo limesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza hofu na kuwajengea wananchi ujasiri
 8. Kama ilivyo katika baadhi ya nchi duniani, Serikali (kupitia agizo la Mh. Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli, imeagiza uchunguzi wa vifaa vya kupima sampuli vilivyopokelewa na Maabara ya Taifa ili kuthibitisha uwepo wa virusi vya Covid 19 miongoni mwa washukiwa na wagonjwa.
 9. Wadau wa sekta ya elimu pamoja na serikali kwa kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, wameanzisha njia mbalimbali za kuwezesha wanafunzi walioko majumbani kuendelea kusoma na kujifunza kwa kutumia mitandano na vyombo vya habari (Radio na Runinga)
 10. Katika kupunguza athari za kiuchumi zitokanazo na Corona, Benki kuu ya Tanzania (BOT) imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushusha kiwango cha Amana kinachotakiwa kwenda Benki kuu kutoka benki za kawaida, kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki za kawaida kukopa benki kuu ya Tanzania kwa 2% kutoka 7% hadi 5% na kuagiza makampuni yanayotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka milioni 3 hadi milioni 5 ili kupunguza ulazima wa mteja kwenda benki.

CHANGAMOTO

Pamoja na juhudi kubwa za Serikali, Kikundi Kazi cha Policy Forum kimeona changamoto kadhaa katika mapambano dhidi ya Covid-19, kama itakavyoelezwa hapa;

 1. Utaratibu wa upatikanaji, utoaji na usambazaji wa taarifa juu ya janga hili kwa wananchi  haujitoshelezi na kupelekea sintofahamu kwa wananchi walioko vijijini na wasiokuwa na TV, Radio na simu janja.
 2. Uagizaji, uzalishaji na usambazaji hafifu wa vifaa kinga kama vile barakoa na vitakasa mikono katika ngazi ya jamii.
 3. Mazingira hatarishi kwa wataalam na watoa huduma kutokana na upungufu wa vifaa vya kujikinga (PPE).
 4. Wananchi kutomudu gharama kwa mfano kununua barakoa zenye ubora, na hatimae kukosa huduma wanapotembelea sehemu za huduma kwa umma kutokana na agizo la Serikali kwa kila mtu kuvaa barakoa anapoenda kupata huduma au katika usafiri wa umma.
 5. Kutokuwa na Ruzuku ya dharura kutoka Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa ili kuziwezesha serikali za mitaa kuwahudumia wananchi kiafya na kuwakimu baadhi yao walio kwenye mazingira magumu na hatarishi zaidi hususan watu wenye ulemavu, watoto yatima  na kaya maskini.
 6. Kukosekana kwa mkakati maalumu kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kutoa msaada au unafuu kwa Makundi ya jamii zilizolazimika kuacha au kufunga biashara au huduma kutokana na mazingira hatarishi ya Covid 19.
 7. Elimu juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona haijatolewa vya kutosha hasa katika ngazi ya Serikali za Mitaa katika kuhakikisha wananchi wanajikinga na maambukizi ya virusi na hivyo kuepuka kuugua ugonjwa wa Corona katika maeneo yao. 

MAPENDEKEZO

 1. Mamlaka za Serikali za Mitaa zitoe unafuu wa kulipa tozo kwa wafanya biashara wadogo ambao wameathirika kutokana na mlipuko wa COVID-19. 
 2. Mamlaka za Serikali za Mitaa zitunge sheria ndogondogo (By-laws) za kuwezesha usimamizi na ufuatiliaji wa njia na kanuni za usafi na za kujikinga badala ya suala la barakoa na kunawa mikono kubakia kuwa suala la utashi wa mtu binafsi.
 3. Mamlaka za Serikali za Mitaa ishirikiane na wadau walioko maeneo yao zikiwemo Asasi za Kiraia kutoa Elimu jamii juu ya uwelewa wa COVID -19 kwa Wananchi walioko chini ya mamlaka zao kwa njia ya matangazo ikiwemo mbao za matangazo lakini pia kuzunguka ndani ya mitaa kwa gari la kuelimisa jamii juu ya COVID 19.
 4. Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka taratibu maalumu na wazi kuwezesha wadau mbalimbali zikiwemo  Asasi za Kiraia, makampuni na mashirika katika kutoa  elimu, misaada ya kifedha, chakula na mahitaji mengine ya msingi kwa watu wenye mahitaji maalum, hususan Watu wenye ulemavu, wazee, watoto yatima na kaya maskini ili waweze kujikimu katika kipindi hichi cha COVID-19.
 5. Viongozi wa Serikali za Mitaa watoe elimu zaidi kwa wananchi wanaoendelea kufanya biashara katika kipindi hiki cha ugonjwa huu wa Covid -19 ili kuepuka kukuza tatizo na kurudisha nyuma juhudi za Serikali dhidi ya mapambano na Corona.
 6. Serikali za Mitaa zitilie mkazo utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na kuhakikisha wanawakataza watu kukaa vijiweni na maeneo ya masoko bila shughuli maalum na kuhakikisha taratibu za uuzaji na ununuzi wa kujihami zinazingatiwa hususan kusimama umbali wa mita angalau moja kati ya muuzaji na mnunuaji.
 7. Serikali Kuu ipeleke mafungu ya dharura ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona kwa mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuziimarisha kimiundo mbinu ya afya na kuharakisha kufikia lengo la kuifuta Corona Tanzania.
 8. Serikali iweke wazi misaada yote iliyopokea, itoe taarifa ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa mapambano ya Corona, ipate mrejesho toka kwa wanufaika wa misaada waliokusudiwa na kufuatilia kama misaada inawafikia wanufaika waliokusudiwa.

Imeandaliwa na kutolewa na;

Wanachama wa Policy Forum – Kikundi Kazi cha Tawala Serikali za Mitaa

Na Kusomwa na;

Israel  Ilunde – Kwa niaba ya Mwenyekiti  wa Mtandao wa Policy Forum      

20, Mei 2020