Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Mtandao wa Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TACCEO) na Jukwaa la Sera (Policy Forum) tumeendelea kufuatilia mchakato wa utayarishaji wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,2019 nchini Tanzania kwa kutoa maoni kwenye rasimu ya kanuni husika ambapo maoni na mapendekezo yetu yaliwasilishwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI mnamo mwezi Aprili, 2019. Baada ya kuchapishwa na kutangazwa kwa kanuni husika na waziri mwenye dhamana, tumefanya uchambuzi wa kina wa kanuni hizo ili kubaini kuzingatiwa kwa maoni na mapendekezo tuliyowasilisha.

Imekua desturi kwa mashirika na mitandao ya AZAKI kufanya uchambuzi kuhusu masuala ya Sera, Kanuni, Sheria na Miongozo mbalimbali inayohusu michakato ya maendeleo nchini. Uchambuzi huu wa kanuni umelenga kubaini mambo mazuri, mapungufu na changamoto zake kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tukiamini kuwa uchaguzi huo ni sehemu muhimu na msingi wa demokrasia shirikishi na mfumo wa uwakilishi hapa nchini.

Tukiwa Asasi za Kiraia ambazo haziungi mkono mgombea yeyote wala chama chochote cha kisiasa, tunatimiza wajibu wetu kama raia wazalendo kwa mujibu wa ibara ya 8 ya Katiba ya Tanzania.

Kutokana na uchambuzi wetu, Policy Forum na TACCEO tumebaini mambo kadhaa katika maeneo makuu mawili ya kimchakato na kimaudhui.  Kwanza, Mchakato umekua wa uwazi na shirikishi kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo ni zuri na la kuipongeza serikali ya awamu ya tano.

Pili, masuala mengi katika kanuni yamezingatiwa na kufanyiwa maboresho kama tulivyopendekeza. Policy Forum, TACCEO na wadau wengine tunaipongeza serikali kwa kuzingatia takribani asilimia 70 ya maoni na mapendekezo yetu kama tulivyowasilisha. Hata hivyo, pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika kanuni hizo, bado tumeona kuna masuala ya msingi ambayo hayakuzingatiwa katika utungaji wa kanuni hizo. Hivyo basi, tumeona ni muhimu umma na mamlaka husika kujua na kuangalia namna ya kuyazingatia wakati wa uchaguzi.

  1. Masuala Ambayo Hayakuzingatiwa
    1.  Masuala ya Jumla
      1. Ushiriki wa Watu Wenye Ulemavu na Mwenye Mahitaji maalum

Kwa mujibu wa Kanuni za Mamlaka za Miji na mamlaka ya wilaya (vijiji) kifungu cha 32(1) na mamlaka za wilaya (vitongoji) Kifungu cha 31(1) kinasema kutakuwa na sanduku maalumu la kupiga kura lililotengenezwa kwa namna itakavyomwezesha mpiga kura kutumbukiza karatasi ya kura kwa urahisi, pia kifungu cha 36(1) (Mamlaka za miji na Wilaya-vijiji) na kifungu cha 35 (1) cha Mamlaka za wilaya-vitongoji) kinaelezea juu ya usaidizi kwa wenye mahitaji maalumu kusaidiwa kupiga kura. Maoni yamezingatiwa ingawa kanuni hizo hazibainishi namna ambavyo watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum watafikia sanduku la kupigia kura kwa urahisi.

1.1.2   Sababu za Kuahirisha Uchaguzi

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, kifungu cha 37 (Mtaa na Kijiji) na 36 (Kitongoji) vinasema kwamba endapo siku ya kupiga kura kutatokea jambo lolote litakalozuia upigaji kura kuendelea kufanyika,msimamizi msaidizi wa uchaguzi baada ya kuwasiliana na msimamizi wa uchaguzi atahairisha uchaguzi. Hivyo basi, ni vyema kanuni hizo ziwe bayana juu ya sababu za msingi ambazo zitapelekea kuhairisha zoezi la uchaguzi. Kwa mfano, kufariki kwa mgombea, kutokea kwa janga la asilia na kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

      1. Sifa za Msimamizi wa Uchaguzi

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, tafsiri ya msimamizi wa uchaguzi ni mtumishi wa umma tu, jambo ambalo linamnyima nafasi raia mwingine asie mtumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

      1. Mkanganyiko wa Majina ya Kanuni

Katika Kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa (mamlaka za Miji) Sura 288, inaonesha jina ni Kanuni za Uchaguzi kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauiri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji. Ambapo kwenye Mamlaka za Miji hakuna Kitongoji, badala yake ingesomeka Kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika Mamlaka Ya Miji Midogo Za Mwaka 2019(sura ya 288).

      1. Kinga kwa Msimamizi wa Uchaguzi

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, kifungu cha 49(Mtaa na Vijiji) na 46 (kitongoji) vimempa kinga msimamizi wa uchanguzi, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Msimamizi wa Kituo, Wajumbe wa Kamati ya Rufaa au Mtumishi yeyote wa Umma aliyehusika na Usimamizi wa Uchaguzi hatowajibika kwa jinai au madai au kuchukuliwa hatua za kinadhamu au kiutawala kwa jambo lolote alilolifanya au kuacha kufanya kwa nia njema wakati wa kutekeleza majukumu yake chini ya kanuni hizi.

Changamoto ya kifungu hiki ni uwezekano wa mhusika kutumia vibaya madaraka yake kwa kisingizio cha “nia njema”. Kwa kuwawekea kinga wasimamizi wa uchaguzi, kunazuia vyombo vya kutoa haki kutimiza wajibu wake na raia yoyote kukosa haki ya kudai katika vyombo hivyo.

      1. Kibali cha Waangalizi wa ndani wa Uchaguzi

Kwa mujibu wa kifungu cha 50 (1) (2) cha mamlaka za wilaya -vijiji na mamlaka za miji,  na kifungu cha 47(1) cha mamlaka za wilaya – vitongoji, waangalizi wa ndani wa uchaguzi wataweza kuangalia uchaguzi baada ya kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya Serikali za Mitaa tu. Kifungu hiki kinaleta urasimu usiowalazima wa kupata vibali hasa kwa vikundi amabavo viko mbali na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara.

 

      1. Tafsiri ya Mkazi

Kwa mujibu wa kanuni hizi tafsiri ya mkazi ni raia wa Tanzania anayeishi kwenye eneo la mtaa, Kijiji au kitongoji ambaye ana kaya au anaishi katika kaya au taasisi iliyopo katika eneo la kijiji,mtaa au kitongoji. Kifungu hiki hakikutamka bayana muda wa mtu kutambuliwa kuwa mkazi wa kijiji, mtaa ama kitongoji. Hivyo kinaweza kutoa mwanya kwa raia yeyote mwenye nia ovu au wahamiaji haramu kujiandikisha na kupiga kura.

      1. Mapungufu ya kiuchapaji kwenye Majedwali na Fomu

Tumebaini mapungufu ya kiuchapaji kwenye majina ya kanuni ambayo pia yameathiri fomu zilizoambatanishwa, tunatambua kwamba baadhi ya fomu zitarekebishwa katika Halmashauri husika;

  • Fomu za matokeo hazina nafasi ya kutaja jina la kituo cha kupigia kura.
  • Fomu za uteuzi hazibainishi /kutambua watu wenye ulemavu  walioonesha nia ya  kugombea nafasi za uongozi.
  • Fomu za Mpiga kura hazina picha ya Mgombea, hali hii inaweza kuleta ugumu wa utambuzi wa mpiga kura kuchagua mgombea anaemtaka hasa kwa mpiga kura asiejua kusoma na kuandika.

Mapendekezo

  1. Tunapendekeza Waziri mwenye dhamana kuzielekeza mamlaka husika kufanya maboresho katika fomu za uteuzi, upigaji kura, na matokeo ya uchaguzi. Hususan Fomu ya matokeo ya uchaguzi kutaja jina la kituo la kupiga kura.
  2. Wadau wa uchaguzi wa serikali za mitaa watoe msaada na ushirikiano ili kuhahikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi.
  3.  Mamlaka ya uchaguzi, Msimamizi wa uchaguzi, Msimamizi msaidizi wa uchaguzi na Msimamizi wa kituo watoe msaada na ushirikiano ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi.
  4. Katibu Mkuu ofisi ya Rais TAMISEMI akasimu mamlaka ya kutoa vibali ya kuangalia uchaguzi na kuendesha elimu ya mpiga kura kwa Msimamizi wa uchaguzi ngazi ya Halmashauri.
  5. Baada ya uchaguzi, Waziri mwenye dhamana azielekeze Halmashauri zote nchini kuandaa na kutoa taarifa ya uchaguzi ya serikali za mitaa kwa umma ikiainisha pamoja na masuala mengine upigaji kura, matokeo, ushiriki wa makundi maalum (vijana, wanawake na walemavu).
  6. Sanduku la kupigia kura liwekwe mahali ambapo watu wenye mahitaji maalum wanaweza kulifikia kwa urahisi.