Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Wanachama wa mtandao wa Policy Forum wanaounda kikundi kazi cha bajeti (BWG) wameishauri serikali kuboresha sekta ya kilimo na ufugaji ili nchi iweze kufikia azimio lake la kuhakikisha inafikia uchumi wa kati wenye kuchagizwa na viwanda. Hayo yamesemwa tarehe 4 Mei 2019 Jijini Dodoma ambapo wanachama hao walikutana na wabunge wa kamati ya bajeti na mtandao wa kupambana na rushwa wa afrika tawi la Tanzania (APNAC-TANZANIA).

Akitoa wasilisho mbele ya wabunge, Ezekiel Semwa kutoka ANSAF (mwanachama wa PF na mjumbe wa BWG) alieleza kuwa sekta ya kilimo pekee huchangia pato la taifa kwa asilimia 30, ikiwa mifugo huchangia asilimia 6, huku asilimia 65 ya ajira nchini zikitengenezwa na sekta ya kilimo na sekta ya mifugo inategemewa na watu zaidi ya milioni 27. Alisisitiza kuwa sekta hizi huchangia zaidi ya asilimia 65 za malighafi ya viwandani nchini na hivyo ni muhimu sana katika kuifikisha Tanzania kwenye njozi ya Maendeleo 2025 ya kuwa na uchumi wa kati (Tanzania ya Viwanda).

Semwa alitanabaisha kuwa pamoja na umuhimu mkubwa wa sekta hizi, changamoto lukuki zimekua zikiathiri maendeleo yake. Changamoto hizo zikiwa kama ufinyu wa bajeti na kutopatikana fedha kwa wakati, ukosefu wa pembejeo zenye ubora, ukosefu wa uwekezaji katika utafiti na mafunzo, upungufu wa huduma za ugani, utitiri wa kodi, miondombinu duni na Kutokuwepo kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Akifafanua kuhusu changamoto za sekta ya kilimo, Semwa alisema kuwa kutoipa sekta ya kilimo kipaumbele kumeifanya sekta hii ikue kwa wastani wa chini ya asilimia 3 kwa mwaka huku takribani bilioni 413 zikitumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Alisisitiza kuwa uagizwaji wa maziwa kutoka nje ya nchi hupoteza fursa za ajira takribani 68,000 kwa mwaka, hii inatokana na uzalishaji hafifu wa viwanda vya maziwa chini ambavyo huzalisha asilimia 30 kutokana na kutopata malighafi za kutosha. Utafiti unaonesha kuwa kusipofanyika jitihada za makusudi za kuboresha sekta ya mifugo, ifikapo 2030 Tanzania itakuwa na upungufu mkubwa wa mazao ya mifugo.

Utekelezaji wa mwaka wa fedha 2018/2019 unaonesha kwamba halmashauri nyingi nchini hazitengi fedha kutoka mapato ya ndani, kwa mfano kiasi cha bilioni 8 zilikusanywa katika zoezi la kupiga chapa mifugo lakini haijulikanikani ni kiasi gani kilielekezwa katika kuendeleza mifugo. Semwa alisema serikali imekuwa ikiweka vipaumbele ambavyo ni muhimu sana kuendeleza sekta ya kilimo nchini lakini hukwamishwa na kiasi kidogo cha bajeti inayotengwa na inayotolewa kutekeleza vipaumbele hivyo.

Kikundi cha bajeti (BWG) kimeishauri serikali Kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi. Pia iongeze bajeti ya kuendeleza sekta ya kilimo kufikia asilimia 10 ya bajeti ya taifa na bajeti ya mifugo iwe walau asilimia 2.

Halikadhalika, wabunge wakiwa wajumbe wa mabaraza ya madiwani wahimize halmashauri kutenga fedha kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo na pia wahimize ushiriki na uratibu wa wadau wote katika halmashauli zao ikiwemo ushirikiswhaji wa sekta binafsi.

Serikali haina budi kulinda wafanyabiashara wa ndani wanaowekeza katika sekta ya kilimo kwa kuwajengea mazingira wezeshi ya kisera ikiwemo kutoza kodi kubwa kwa bidhaa kutoka nje. Serikali ipitie sera ya mifugo ya mwaka 2006 na kuirekebisha kwani haiendani na dhima ya nchi ya kuimarisha viwanda. Uboreshaji wa sera hiyo utawezesha uwepo wa mazingira wezeshi yanayohakikisha ulinzi na manufaa kwa wadau muhimu wakiwemo wazalishaji na wawekezaji wadogo.

Akihitimisha semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. George Simbachawene aliishukuru PF kwa kuratibu semina hiyo ambayo imekuja muda muafaka ikizingatiwa bado Serikali haijasoma bajeti ya kilimo na mifungo, hivyo, maudhui yaliyotolewa na kikundi kazi yameongezea ujuzi wabunge wa kutoa mapendekezo ya kuboresha sekta ya kilimo na ufugaji. Hata hivyo alisisitiza kuwa mara nyingine ukosefu wa fedha unaweza usiwe ni changamoto pekee inayofanya sekta hizo zisitoe mchango mkubwa kwenye uchumi bali ukosefu wa uratibu bora wa fedha zinazotolewa unaweza kudunisha sekta ya kilimo na ufugaji na hivyo kushindwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi yanayohitajika