Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Ubalozi wa Uswisi hapa nchini kupitia Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi SDC umezindua awamu ya tatu ya programu ya uwajibikaji wa kijamii (Social Accountability Programme - SAP) ambayo inachangia kuziwezesha asasi za kiraia (AZAKI) zinazofanya kazi ili kuboresha uwajibikaji nchini Tanzania.

Uswisi ina nia ya kuchangia zaidi katika kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji wa mamlaka za umma ili zitoe huduma bora kwa wananchi. SDC itachangia shilingi bilioni 18 kwa kipindi cha miaka minne ijayo kwa asasi kadhaa za kiraia ikiwa ni pamoja na Foundation for Civil Society (FCS), Policy Forum, na Twaweza.

Ubalozi wa Uswisi unashirikiana na asasi hizi ambazo zinahusika na uanzishwaji na usimamizi wa sera za maendeleo ili kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida. Uswisi inaamini kwamba asasi za kiraia ni moja ya wadau muhimu kwa nchi ya Tanzania ili kufikia malengo yake ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Programu hii ya SAP ni sehemu ya michango kadhaa ya Uswisi kwa Tanzania katika kuimarisha masuala ya uwajibikaji. Uswisi tayari ina ushirikiano wa muda mrefu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kuimarisha uwezo wake wa uchunguzi. Uswisi pia inachangia mpango wa Utawala bora wa Fedha (Good Financial Governance GFG programme) unaotekelezwa na shirika la Kijerumani la GIZ. Programu hii inafanya kazi ya kuzijengea uwezo na kutoa msaada wa kiufundi kwa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani na halmashauri za wilaya ili kuwezesha utawala bora wa fedha na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Uswisi imekuwa ikichangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania tangu miaka ya 1960 na inaendelea kutoa karibu shilingi bilioni 51 kila mwaka kusaidia sekta za afya, ajira na mapato, na utawala bora.

Kuhusu FCS

FCS ni taasisi inayotoa ruzuku na kuzijengea uwezo asasi za kiraia  nchini. FCS inatoa ruzuku na kuzijengea uwezo kwa wastani Azaki 150 kila mwaka katika maeneo muhimu yaliyopewa kipaumbele. Kwa habari zaidi: http://thefoundation.or.tz/

Kuhusu Policy Forum

Policy Forum ni mtandao wa kitaifa wa utetezi wa sera ulio na wanachama kutoka Azaki 79 unaofuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika sekta mbalimbali. Kwa habari zaidi: https://www.policyforum-tz.org/

Kuhusu Twaweza

Twaweza ni asasi ya Afrika Mashariki inayohusika na kuimarisha ‘utashi wa wananchi’. Twaweza inafanya kazi ili kuwezesha sauti za wananchi kuchukuliwa kwa uzito katika kufanya maamuzi na kuonyesha kuwa wananchi wana uwezo wa kutatua matatizo yao wenyewe. Kwa habari zaidi: https://www.twaweza.org/