Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Mtandao wa Uwazi Katika usimamizi wa Fedha “The Financial Transparency Coalition (FTC)’ na asasi mwenyeji ya Policy Forum, wameandaa mkutano mahiri katika uwazi wa usimamizi wa fedha. Mada kuu ya mkutano huo wa siku mbili unaofanyika Jumanne  na Jumatano wiki hii katika Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam, ni “Kuleta Uwazi: Namna ya Kujenga Uwazi wa Matumizi ya Fedha Duniani kwa Ajili ya Maendeleo”.

Mkutano huo unaolenga kuleta uwazi katika mikataba ya uvunaji wa maliasili hususani, mafuta, gesi asilia, mbao na madini, utasaidia kuleta manufaa kwa pande zote mbili za mikataba hiyo. Mada zitakazowasilishwa ni pamoja na madhara ya utoroshaji wa pesa nje ya nchi, pia migogoro na hali tete ya kisiasa inayosababishwa na mikataba hiyo mibovu. Mada nyingine ni pamoja na utoroshaji wa wanyama na biashara haramu ya silaha ndogo ndogo. Wageni zaidi ya 30 wanatarajiwa kuziwakilisha nchi zao katika semina hiyo muhimu.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, mratibu wa Policy Forum Bw. Semkae Kilonzo alisema “katika kiwango kisichopungua trilioni moja zinazotoroshwa kutoka katika nchi zinazoendelea, nusu yake ikiwa ni zaidi ya dola bilioni 500 hutoka katika Bara la Afrika.  Kiwango hiki cha uhalifu, ufisadi, na ukwepaji kodi kinawakilisha hali isiyokubalika ya uyumbishaji wa uchumi wa nchi zinazoendelea, ambacho ni sawa na mara nane ya kiwango cha misaada ya fedha za kigeni”.

Tanzania imekuwa mlengwa wa Mtandao huu wa Uwazi katika usimamizi wa Fedha kwa sababu tayari gesi asilia imekwisha vumbuliwa nchini, ni hali inayoleta matumaini kwa wananchi wake katika muongo ujao.  Tanzania kwa sasa ni miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani ikiwa na viwango vidogo vya elimu kwa watu wake kwa kiwango cha asilimia 25 kwa watu wazima, makadirio ya uwezo wa kuishi kwa mtu ni miaka 58, ambapo ni asilimia 14 tu ya watu wake wanaopata huduma ya umeme, katika nchi yenye watu milioni 48.

“Watanzania wanaweza kujiondoa katika lindi la ufukara iwapo gesi asilia itatumika vizuri na kwa uwazi, lakini utoroshaji wa pesa unaweza kuzamisha jitihada zote hizo” alisema Kilonzo.

Aliongeza kwambautoroshaji wa fedha kutoka katika nchi zinazoendelea hupunguza makusanyo ya kodi, hupunguza uwazi unaotakiwa katika utawala bora, na hasa katika kipindi hiki muhimu ambacho maliasili nyingi zimekuwa zikivumbuliwa hapa Tanzania.

Kilonzo alisema, ushindani wa kupata wawekezaji umesababisha upunguzaji wa kodi na hivyo kuzipunguzia nchi hizi mapato makubwa. Nchi za Kiafrika zimekuwa zikipoteza mapato kutokana na mtindo huu ambayo yangesaidia katika kutoa ajira, kujenga barabara, hospitali na kliniki,  na shule.

“Haiwezakani kwamba bara lenye maliasili kama hizi linaweza kubakia katika lindi la umaskini na watu wake wakaishi katika maisha duni kwa kiwango hiki,” alisisitiza Kilonzo.

Policy Forum na FTC wanaamini kwamba Watanzania na Waafrika kwa ujumla wanaweza kunufaika kwa kufanya mabadiliko chanya na kushirikishana na mataifa mengine kwa kubadilisha taarifa za fedha, mauzo, faida, na taarifa za kodi zinazolipwa na makampuni ya wawekezaji ya kimataifa. Wanachi wanapaswa kufahamishwa kwa uwazi habari za mapato ya kodi, kutoka kwenye mashirika yote ili wajione kwamba na wao ni sehemu ya uchumi huo.

"Ili nchi zinazoendelea ziweze kunufaika kiuchumi ni lazima mfumo wa fedha utende haki kwa watu wote duniani. Wakati nchi za Kiafrika zinashukuru kwa misaada mbali mbali kutoka katika nchi zilizoendelea, lakini ni vyema kuwepo na mfumo mzuri unaotenda haki kwa pande zote, hicho ndicho kinachopiganiwa hapa. Jitihada za kupigania uwazi ni hatua mbele katika kufanikisha ndoto za usawa katika mapato” alihitimisha Kilonzo.

Kwa habari zaidi tafadhari wasiliana na wafuatao:

POLICY FORUM:

·         Alex Ruchyahinduru   +255 757716333, policy2@policyforum.or.tz

FINANCIAL TRANSPARENCY COALITION:

Dietlind Lerner: +1 202 577 3455 / dlerner@financialtransparency.org

Nick Mathiason: +44 77 99 348 619 / nmathiason@financialtransparency.org

Taarifa kwa wahariri:

1) Financial Transparency Coalition (FTC) ni Mtandao wa zaidi ya nchi asasi za kiraia 150 na serikali 12 katika sehemu mbali mbali duniani. Mtandao huu unazishirikisha taasisi zifuatazo;  Christian Aid, Eurodad, Global Financial Integrity, Global Witness, Tax Justice Network and Transparency International. Mtandao huu unafanya kazi ya kuhakikisha kwamba usiri wowote katika masula ya fedha ambao unawaathiri zaidi ya mabilioni ya watu unaondolewa.

2) Awali FTC ilifahamika kwa jina la Task Force on Financial Integrity and Economic Development.

3) Policy Forum, ni mtandao wa Asasi zaidi ya 100 za kiraia za Tanzania zilizoungana kwa pamoja kwa dhamira ya kushawishi michakato ya uundwaji sera ili kupunguza umaskini, kuleta usawa na demokrasia wakijikita zaidi katika uwajibikaji wa serikali kwa matumizi ya fedha za umma.