Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Mchakato wa kuhalalisha mahusiano baina ya Serikali, wahisani, wafadhili na Asasi zizo za kiserikali AZAKI umekuwa na changamoto nyingi. Kumekew na juhudi nyingi ambazo zimekuwa zikitoa tumaini kwa AZAKI kwamba mahusiano rasmi na wadau wengine wa maendeleo ni jambo ambalo linawezekana kuwa rasmi na endelevu.

Kwa hiyo huu utajiri mkubwa wa uzoefu na uwezo wa aina mbalimbali wa AZAKI unaotokana na ushiriki wao katika nafasi nyingi kwa miaka mingi, utachangia sana katika kuwa na muundo unaokusudiwa. Mchakato huu unakusudia kuhakikisha AZAKI zinashiriki kikamilifu katika ngazi zote zinazofanya maamuzi kuhusu sera za maendeleo na matumizi bora ya rasilimali zetu. Ni muundo ambao una fursa ya kuzingatia tafauti za kimaslahi, kifikra na mbinu za utekekezaji kati ya serikali, AZAKI na wadau wao. Pia muundo huu ni ulingo wa AZAKI wa kuibua na kujadili baina yao na wadau wengine masuala ya maendeleo yenye maslahi ya kitaifa.

Hakuna asie jua kwamba AZAKI mbalimbali zimekuwa zikijadili na serikali, wafadhili na wadau wengine kwa miaka mingi; AZAKI zimekuwa zikijijengea uwezo na kutafuta ufadhili ama mmoja mmoja au katika makundi. Kwa hiyo thamani inayo ongezeka katika muundo huu unaopendekezwa ni kuongeza nguvu ya pamoja, kupaaza sauti za pamoja za AZAKIzifike kwa wafanya maamuzi na kuhalalisha juhudi mbalimbali kwa faida ya waTanzania. Lengo si kufinya juhudi za AZAKI mojamoja au mitandao yao na wala si kuwa mbadala. Bali ni Ulingo au Jukwaa la pamoja la kufanya maamuzi ya pamoja na kupeana taarifa ya kila kinachoendelea katika sekta mbalimbali.

Matarajio ni kwamba hatimae muundo huu utakuwa imara katika ngazi za Wilaya ili kuibua, kujadili na kufanya utafiti shirikishi katika masuala ya sera na maendeleo kwa mtazamo wa Mtanzania. Muundo huu utachochea AZAKI zijipange kushiriki, kuwajibika na kutumia ubunifu katika ushawishi na utetezi katika masuala yenye maslahi kwa taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Azma kubwa ni kutumia fursa hii halali ya demokrasia vitendo katika kutoa mchango wetu katika kujenga Tanzania tuitakayo katika miaka mia ijayo, Tanzania ya wajukuu zetu.

Mkataba wa Mapatano wa Cotonou wa 2000 kati ya Umoja wa nchi za Ulaya na zile za Afrika, Karibian na Pasifiki unazitambua AZAKI na umezipa uhalali wa kujipanga kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia katika nchi zao. Hapa Tanzania AZAKI zilikwisha anza kuunganisha nguvu zao kwa kuunda mitandao ya kisekta, ya kikanda, ya kinasaba. Mchakato wa kuwa na muundo huu ni hatua ya juu zaidi ya kuimarisha mshikamano katika masuala yanayotuunganisha kama AZAKI za kiTanzania ili:

  • Kuwa na majadiliano baina ya AZAKI kwa AZAKI, AZAKI na wadau wengine ilikufikia muafaka katika masuala sera na maendeleo kwa jumla.
  • Kuwajibika kwa pamoja katika kuhakikisha muundo unakidhi mahitaji, matakwa na matarajio ya AZAKI na wadau wake ili wawe na sababu ya kufadhili kwa hali na mali ili uwe endelevu.

Wizara ya Fedha na Uchumi  iliandaa kikao kwa ajili ya kuwapa taarifa AZAKI kuhusu Mkakati wa Pamoja wa Uratibu na Matumizi bora ya Misaada (JAST). Kikao hicho cha siku mbili kilifanyika KIbaha tarehe 22-23 Juni 2010 na kilifadhiliwa na Umoja wa nchi za Ulaya. Nia ilikuwa kutoa fursa kwa AZAKI kuuelewa mkakati huu na kujadili ni kwa jinsi gani AZAKI zitashiriki katika kujadili masuala ya sera, misaada na maendeleo kwa jumla na wadau wengine hasa serikali, wafadhili na wahisani. 

AZAKI 55 kutoka Bara na Visiwani zilishiriki katika awamu hii ya kwanza kwa kuzingatia sekta zao, uzoefu na ushiriki wao katika majadiliano ya sera na utekelezaji wa miradi. Walioteuliwa kuja walitarajiwa wawe na ujuzi wa kutosha katika sekta zao na waweze kutoa maamuzi kwa niaba ya asasi na mitandao wanayowakilisha na waweze kutoa mrejesho kwa wadau wao.

Lengo la kikao lilikuwa kuwakukutanisha AZAKI na Serikali ili wajadili kwa undani kuhusu muundo, mgawanyo wa majumu, vigezo na hadidu za rejea kwa AZAKI na wale watakao chaguliwa kuwakilisha; hususan katika suala la uratibu na matumizi bora ya misaada katika kuleta maendeleo. Serikali ilitoa pendekezo la muundo uliokubalika kati ya serikali na wafadhili na kutaka maoni ya AZAKI ili nao washiriki kikamilifu na waendelee kuchangia maendeleo ya nchi yetu. Muundo utahakikisha kwamba wote tunawajibika katika matumizi bora ya rasismali.

Lengo la Muundo wa JAST:

  • Kuboresha ushiriki wa AZAKI katika majadiliano ya kitaifa na wadau wengine
  • Kuimarisha ushiriki wa AZAKI na umilki wa kitaifa katika kuendesha nchi yetu,
  • Kuwezesha uwajibikaji wa pamoja kati ya AZAKI na wadau wengine kwa faida ya waTanzania,
  • Kuchabgia kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo na matumizi bora ya rasilimali watu, fedha na nyezo zingine.
  • Kuwa watetezi wa kitaifa na Kimataifa wa maendeleo, matumizi bora ya misaada na uratibu wa misaada,
  • Kuwa chachu ya mijadala ya kitaifa na kuelimisha umma kuhusu mchakato wa majadiliano ndani ya muundo wa JAST.