Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Wanachama wa Policy Forum, tukiwa ni sehemu ya jumuiya za kiraia na sehemu ya wapiga kura wa wabunge wetu tumechukua jukumu katika jukwaa hili leo kutoa tahadhari kwa wabunge wetu kuhusu athari za kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya jimbo. Hii ni sehemu muhimu ya wajibu wetu kama raia waaminifu, wenye nia njema ya kuchangia mawazo bora yatakayotuletea maendeleo endelevu nchini kwetu. Bila mjadala mpana na mawazo chanya yaliyochambua maswala kwa undani kama msingi wa maamuzi, nchi itafanya maamuzi dhaifu yasiosimama kwenye misingi ya hoja na ukweli wa mambo. Na hatuwezi kutegemea maamuzi dhaifu yasiyo na hoja wala uchambuzi yakinifu kujiletea maendeleo endelevu nchini kwetu. Kukaa kimya au kutokuwa wa kweli kwenye jambo ambalo mnaliona kwamba halina maslahi kwa taifa letu na huenda likaturudisha nyuma maendeleo tuliokwisha piga, ni kukosa uwajibikaji kama asasi zilizopewa kujumu hilo. Kwani Uwajibikaji siyo kwa serikali tu, hata asasi za kiraia zinawajibika katika kushawishi na kutetea sera na mipango inayoweza kuwaletea raia maendeleo endelevu na siyo vinginevyo. Kwa sababu hizi mbili:

Kwanza ya uwajibikaji wa asasi kwa jamii katika kutetea sera bora na zenye kuleta maendeleo endelevu,

Na pili kwa sababu ya kupanua mjadala kuhusu uanzishwaji wa mfuko wa maendeleo ya jimbo, wanachama wa Policy Forum wanatoa;

Msimamo kuhusu Hoja zilizotolewa za kuanzisha mfuko wa maendeleo ya jimbo na la pili ni Athari zitakazotokana na kuanzisha mfuko huu.

La tatu na hitimisho, asasi zinatoa mapendekezo mbadala kwa Serikali nini kifanyike kuimarisha Majimbo ya Uchaguzi.

2.0 MSIMAMO KUHUSU HOJA YA KUANZISHWA KWA MFUKO WA MAJIMBO

2.1 Kujenga uwezo wa Kujitegemea katika Bajeti ya Serikali Kuna hoja kwamba nchi itajenga uwezo wa kujitegemea kwa kuanzishwa mfuko wa majimbo.

Hili si kweli kwani mfuko wa Maendeleo ya jimbo utatokana na bajeti ile ile ya serikali inayotegemea wafadhili kwa asilimia 40 hivi sasa. Kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya jimbo hakuiongezei serikali uwezo wa kupata mapato makubwa zaidi bali kunaongeza matumizi ya mapato yale yale ili kuweza kukidhi mahitaji ya mfuko wa maendeleo ya jimbo. Badala ya mapato ya serikali kwenda kwenye bajeti ya maendeleo ya Halmashauri zetu, sasa itabidi sehemu imegwe ili iweze kutengwa kama mfuko wa maendeleo ya jimbo. Ni mapato yale yale ambayo yangetengwa kwa miradi ya maendeleo katika Halmashauri yatakayobidi yamegwe kwenda kwenye mfuko wa jimbo. Maana yake ni kwamba tuko tayari kuifinya bajeti ya maendeleo ya Halmashari zetu ili tuanzishe mfuko wa majimbo ambao nao utafanya kazi ile ile inayofanywa na Halmashauri zetu hivi sasa kwasababu ambazo hazieleweki na huenda hazina msingi thabiti.

2.2 Mfuko utatoa fursa ya Jamii kupata raslimali fedha ya kuendeleza miradi iliobuniwa na jamii yenyewe.

Kuna hoja kwamba kwa kuwa na mfuko wa maendeleo ya jimbo, jamii itapata kianzio cha fedha za kuendeleza miradi inayobuniwa na jamii yenyewe. Hii si sahihi kwani tunaelewa kwamba Sera ya Serikali ya Maendeleo Vijiji – Rural Development Policy inatamka wazi kwamba maendeleo vijijini yataletwa kwa kushirikisha jamii katika mipango yote ya maendeleo. Fedha zote zinazotengwa kwenye bajeti ya serikali kwa ajili ya maendeleo zinaendeleza mipango shirikishi ya maendeleo katika Halmashauri. Mifano tunayo hai ya mipango ya maendeleo ya elimu ya msingi, mipango ya maendeleo ya elimu ya sekondari, mipango ya kundeleza kilimo yote ni mipango shirikishi inayojumisha jamii katika kubuni na kuitekeleza. Serikali ina mpango wa kuendeleza huduma ya afya ya msingi vijijini kwa kujenga zahanati katika kila kijiji na kuzipatia zahanati hizi wahudumu wa kutosha. Wananchi wanashirikishwa kwenye mkakati huu ambao unafadhiliwa na vianzo vya raslimami fedha kutoka bajeti ya serikali kupitia Halmashauri zetu. Hii si miradi ya maendeleo shirikishi?

Ingekuwa vyema zaidi kama wawakilishi wetu wangewahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye kupanga mipango ya serikali ya kutekeleza mikakati iliyopo ya kuboresha elimu, afya, maji na barabara badala ya kuunda mifuko iliyo nje ya mfumo mzima wa mipango na utekelezaji wa bajeti ya serikali. Serikali inayo mikakati mizuri ya kuboresha afya, barabara, kilimo, elimu, upatikananji wa nishati vijijini, tatizo ni uhamasishaji wananchi kushiriki kupanga mipango hii ili iweze kutumia rasilimali fedha inayotengwa kutoka kwenye bajeti kila mwaka kwenda kwenye Halmashauri zetu. Tatizo ni uwezo wa Halmashauri kuwashirikisha wananchi katika utekelezwaji, na sio vianzo vya fedha.

Fedha inatengwa na Serikali Kuu kwenda Halmashauri lakini haipangiliwi na kutumika ipasavyo kwa sababu ya ushirikishwaji finyu wa wananchi na usimamizi hafifu wa madiwani na wabunge wakiwa sehemu hiyo ya Halmashauri kama wajumbe wa Halmashauri 2.3 Mfuko utamuondolea Mbunge jukumu la kufadhili miradi ya maendeleo Jukumu la Mbunge la kufadhili miradi katika jimbo lake siyo jukumu alilopewa kikatiba. Jukumu la Mbunge alilopewa kikatiba ni kushirikiana na wananchi wa jimbo lake kuhakikisha kwamba serikali na halmashauri zinawajibika katika kutumia rasilimali fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya serikali ili maendeleo yaweze kupatikana kwa wananchi. Wabunge hawana wajibu wala hawalazimiki kufadhili miradi ya maendeleo katika majimbo yao kisheria. Hilo ni jukumu la serikali na suluhu ni kuielimisha jamii hivyo na siyo kuchukua majukumu ambayo hawawajibiki nayo. Elimu ya uraia ambayo imeainishwa kwenye Mpango wa Kuboresha utendaji wa Halmashauri zetu ni muhimu ukazingatiwa ili kutatuwa matatizo ya uelewa wa raia kuhusu majukumu ya Mbunge, Serikali Kuu, na Serikali za Mitaa.

2.4 Mfuko Utampa Mbunge Nguvu Za Kifedha za Kuanzisha Miradi katika Jimbo lake Sawa Na RC na DC ambao wana Bajeti HIZI

Uwezo wa DC na RC kuwa na fungu la kutumia kuleta maendeleo kwenye maeneo yao umetokana na mamlaka waliyopewa kikatiba kutekeleza miradi ya maendeleo kama sehemu ya Serikali Kuu. Mamlaka ya Mbunge yalioainishwa kikatiba ni kuishauri serikali na kuisimamia katika utekelezaji wa bajeti ili kuwaletea wananchi maendeleo yao. Kama RC na DC wanatumia bajeti hizi wanavyopenda wao kama inavyodaiwa na wabunge kosa hili haliwezi kusahihishwa kwa kuunda kosa jingine la kuanzisha mfuko wa maendeleo ya jimbo ambao wabunge watautumia wanavyoona wao. La msingi ni wabunge kuwawajibisha maRC na DC watekeleze bajeti ya serikali kwa kuhakikisha fedha zinatumika kwa maendeleo ya wananchi na siyo vinginevyo.

2.5 Mfuko wa TASAF hauendeshwi kidemokrasia

Kuna hoja kwamba mfuko wa TASAF hauendeshwi kidemokrasia na ndiyo maana mfuko wa maendeleo ya jimbo unahitajika ili kuboresha demokrasia katika kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo yao. Policy Forum ina maoni tofauti kuhusu hoja hii, kwani udhaifu wa TASAF hauwezi kurekebishwa? Ni lipi gharama zaidi kuanzisha mfuko mwingine au kuboresha mfuko uliyopo. Kwa mantiki ya kuangalia gharama za uendeshaji na uazishwaji wa mfuko mwingine ingekuwa busara zaidi kuimarisha mfuko uliyopo kuliko kuazisha kitu kipya kitakachofanya kazi sambamba na ile ile inayofanywa na mifuko iliyopo. Hii siyo kuongeza gharama ambayo haiongezi ufanisi wowote kwa vyombo vilivyopo, bali inaongeza mzigo kwa utendaji wa halmashauri.

2.6 Wafadhili hawana haja ya kuwa na wasiwasi na matumizi ya fedha za mfuko wa majimbo

Kuna hoja kwamba wafadhili hawana haja ya kuwa na wasiwasi wa matumizi ya fedha za mfuko huu kwani zitatokana na vianzo vya mapato ya ndani na siyo fedha ya wafadhili. Policy Forum inaona kwamba hoja siyo kwamba pesa itatoka wapi kwa wafadhili au kutoka mapato yetu wenyewe. Hoja yetu ni kwamba kweli dhana hii ya mfuko wa maendeleo ya jimbo itatuletea maendeleo endelevu au itatupotezea muda rasilimali watu na fedha ambayo ingeweza kutumika vizuri zaidi kutumia mifumo na taasisi za serikali zilizopo ili ziimarike katika majukumu yake ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa kuondoa jukumu la sehemu ya miradi ya maendeleo kutoka halmashauri kwenda kwenye mikono ya kamati za mifuko ya majimbo tunadhoofisha uwezo wa halmashauri kuboresha utendaji wake na kutoa madaraka kwa kamati ambayo haina uwezo. Wala nyenzo ya fedha ya mfuko huo haiwezi kuleta maendeleo endelevu na ya muda mrefu. Aslimia 2.5 ya bajeti ya matumuzi inayopendekezwa kutengwa kwa ajili ya mfuko wa majimbo ni kiasi kidogo sana cha kuweza kuleta maendeleo endelevu katika majimbo. Si zaidi ya kiasi cha Tshs milioni 600 kwa kila jimbo la uchaguzi lenye wastani wa watu laki 200-300. Ni wastani wa Tshs 2000 kwa kila mkazi wa jimbo. Hiki ni kiasi kidogo sana cha kutuletea maendeleo endelevu. Mpango wa Elimu ya Sekondari uliofanikishwa na Serikali hivi karibuni, wananchi kwa wastani wamechangia zaidi ya Tshs 2000 kwa mwaka kuifanikisha.

Pesa itakayotengwa haitatuletea maendeleo endelevu na yatakayoonekana. Bora ijumuishwe kwenye mipango ya serikali kama ya elimu ya msingi na elimu ya sekondari au mipango ya kuboresha upatikanaji wa maji na zahanati vijijini ambayo matunda yake yanaonekana. Miradi hii pia ni endelevu kwani inatengewa fedha za uendeshaji kwenye mipango ya bajeti ya serikali ya kila mwaka.

3.0 POLICY FORUM INATOA TAHADHARI ZIFUTAZO KUHUSU KUANZISHWA KWA MFUKO WA MAENDELEO YA JIMBO

3.1 Mfuko wa Maendeleo ya jimbo utadhoofisha nguvu ya wabunge

Policy Forum inatoa tahadhari kwamba Mfuko wa majimbo utadhoofisha nguvu ya wabunge bungeni kuisimamia serikali. Katiba ya Jamhuri wa Muungano kifungu cha 63(2) inasema kwamba Bunge litakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi kuishauri na kuisimamia serikali na vyombo vyake vyote katika kutekeleza majukumu yake. Kwa wabunge kujiingiza kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo wao wenyewe badala ya kuiachia serikali za halmashauri watakuwa wamedhoofisha uhuru na nguvu yao ya kuihoji serikali kwenye maswala ya utekelezaji wa bajeti.

Kwani nao walishiriki katika kutekeleza na ni sehemu ya matokeo hasa yakiwa matokeo hayo ni mabaya. Ndiyo maana kikatiba madaraka haya mawili ya utekelezaji na usimamizi wa utekelezaji yakatenganishwa- separation of powers between Legislature/Parliament and The Executive /Government. Hii litaathiri maendeleo na demokrasia siyo ya majimbo ya uchaguzi tu, bali maendeleo na demokrasia ya nchi nzima iwapo bunge litadhoofika.

3.2 Mfuko wa maendeleo ya jimbo unaongeza gharama bila ufanisi

Mfuko huu unalazimisha kuweka muundo mpya wa utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo utakaoendeshwa sambamba na muundo wa halmashauri. Muundo huu ni nyongeza ya gharama na mzigo wa ziada wa uendeshaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri zetu ambao tuna uhakika hautatuletea tija wala maendeleo endelevu kama hoja zilizotangulia zinavyotuonyesha. 3.3 Mfuko unadhoofisha dhana na mkakati mzima ya kupeleka madaraka kwenye halmashauri Mpango wa Serikali wa Kuboresha Utendaji na Usimamizi wa maendeleo katika Halmashauri – Local Government Reform Program ni mpango mzuri wa kuziimarisha halmashauri katika kuziongezea madaraka, na nyenzo za utendaji fedha na wafanyakazi.

Pia ni mpango wa kuimarisha utawala bora na uwajibikaji wa halmashauri kwa wananchi. Dhana ya kuanzisha mfuko wa maendeleo ya jimbo na hoja za kuuanzishwa hazitambui kabisa mpango huu wa kuimarisha halmashauri ili ziweze kutekeleza majukumu yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Kwa sababu Mfuko wa maendeleo ya jimbo utachukua rasilimali fedha ambazo zingekwenda kuimarisha uwezo wa utendaji wa halmashauri zetu na hauoneshi ni jinsi gani utaimarisha halmashauri na utendaji wake. La Hasha! Unazidhoofisha halmashauri kiutendaji na hata kiusimamizi. Kwani tunaelewa kwamba sehemu kubwa ya miradi ya maendeleo katika halmashauri zetu hutegemea fedha kutoka serikali kuu. Kwa kumega fedha hii iende kwenye mfuko wa majimbo kwa miradi ya maendeleo pamoja na uendeshaji wake tunapunguza uwezo wa halmashauri kutekeleza miradi mikubwa yenye kuweza kutuletea maendeleo katika nyanja pana zaidi kuliko maendeleo yanayoletwa na vimiradi vidogo vidogo kwenye maeneo kama dhana ya mfuko invyotuelekeza huko.

3.4 Mfuko wa majimbo utalazimu serikali kuongeza kodi

Iwapo Serikali itataka isizidhoofishe halmashauri kwa kumega fungu la pesa za maendeleo ziende kwenye mfuko wa maendeleo ya jimbo basi fedha za ziada kwenye bajeti zitahitajika kuendesha mfuko huu na vyanzo vya fedha ya ziada kwenye bajeti ni kodi mpya au kuongezwa kodi zilizopo.

3.5 Hatari ya matumizi mabaya ya mfuko

Kuna Hatari kubwa kwamba fedha za mfuko huu zikatumika vibaya kwa kukosa usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa wananchi kwani msimamizi wananchi waliomchagua kuwawakilisha naye ameingia kwenye utekelezaji. Upatikanaji wa taarifa za miradi utategemea sana utashi binafsi wa mbunge kuwa wazi na kuwajibika kwa wananchi.

4.0 HITIMISHO

Changamoto zinazoikabili CDF na dhana yake nzima ya utekelezaji wake inaiweka serikali katika mazingira magumu ya kuuendesha mfuko huu. Kutokana na uzoefu wetu na ushahidi mwingine unajionesha katika uchunguzi wa awali kama PEFAR ni kuwa kuna uduni wa huduma zinazotelewa katika ngazi za chini sio kwa kukosekana kwa misaada, bali ni kwa udhaifu wa utendaji, ukosefu wa mifumo thabiti, muingiliano wa siasa katika utekelezaji wa sera, uwezo mdogo wa wananchi kufuatilia na kutambua haki zao, n.k. Uanzishwaji wa CDF unaweza kuharibu zaidi hali hii badala ya kuiboresha. Ukijumlisha, uwepo wa misaada mingine ya kimaendeleo ambayo hutoa huduma sawa na CDF hapa nchini, inapendekezwa kuwa ujumla na mfumo wa kichangamoto unaoukabili uendeswaji na utekelezwaji wa misaada iliyotolewa huwa inahesabika, badala ya kuanzishwa kwa msaada mwingine ambao unaweza kuharibu changamoto iliyopo.

5.0 MAPENDEKEZO MBADALA YANAYOTOLEWA

1. Kutokana na matokeo ya CDF kuweza kuwa makubwa, wanachama wa Policy Forum wanashauri kuwa sheria ya CDF isipitishwe kwanza hadi pale kutakapokuwa na uelewa mkubwa wa mfuko wa aina hii miongoni mwa wadau mbali mbali kuhusu matokeo yake.

2. Badala ya kuanzisha jukumu lingine katika Bunge ambalo kimsingi sio la kwake na ambalo linaweza kudumaza utekelezaji wa jumla wa majukumu ya msingi ya Bunge, tunapendekeza hatua zichukuliwe katika mfumo uliopo wa sheria kwa ajili ya kuimarisha dhima ya Bunge ya usimamizi katika ngazi za chini na kitaifa. Baadhi ya mapendekezo juu ya namna hili linavyoweza kufanyika ni pamoja na haya yafuatayo:

  • a. Kuhakikisha kwamba wabunge wote wana ofisi. Wabunge wa majimbo ofisi zao zikiwa jimboni na wale wa viti maalum zao zikiwa Dar es Salaam au Dodoma.
  • b. Kuhakikisha kuwa ofisi zote za wabunge zina samani zote za muhimu na vifaa (ikiwa ni pamoja na vile vya TEKNOHAMA pale inapowezekana).
  • c. Kumwezesha kila Mbunge kwa kuwa na watumishi wanaoweza kufanya utafiti, kufuatilia masuala na kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya usimamizi.
  • d. Kutenga bajeti kwa ajili ya miradi maalumu ya utafiti kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Bunge
  • e. Kuweka mifumo ya uwajibikaji kwa ajili ya kuhakikisha kuwa rasilimali zilizotengwa katika vipengele a hadi d (hapo juu) zinatumiwa vizuri kwa mambo yaliyokusidiwa.