Uongozi wa Kidemokrasia katika Jamii: Ushiriki wa Wananchi na Viongozi katika Ngazi za Msingi za Serikali za Mitaa
Ushiriki wa wananchi ni suala muhimu na la msingi sana katika kujiletea maendeleo yao katika vijiji na mitaa. Mahali ambapo wananchi hawashiriki wala hawashirikishwi kunakuwa na lawama na mizozo mingi kwa viongozi hasa pale ambapo maamuzi yaliyopitishwa yanawaumiza wananchi ndipo tunaona umuhimu wa kushiriki unajitokeza zaidi.
Serikali za mitaa zimegawanyika katika makundi mawili; Mamlaka za Mijini na Mamlaka za Wilayani, kwa upande wa mijini ngazi ya msingi ya serikali za mitaa ni Mtaa, ikifwatiwa na halmashauri kisha ngazi ya juu ni halmashauri ya manispaa au jiji na kwa upande wa wilayani kitongoji ndiyo ngazi ya chini kabisa kisha inafuatiwa na kijiji na hatimaye ni halmashauri ya wilaya kama chombo cha juu kabisa.
Kitongoji
Mkutano wa Kitongoji huongozwa na Mwenyekiti wa Kitongoji ambaye huchaguliwa na wakazi wa Kitongoji hicho. Dhumuni la Mkutano huu ni kuwapa wananchi fursa ya kujadili kero na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
- Kitongoji ni sehemu ya kijiji
- Kitongoji sio ngazi ya utawala inayojitegemea
- Kuwepo kwa kitongoji ni kupeleka shughuli za Serikali ya Kijiji karibu na wakazi /wanakijiji
- Kila kijiji huwa na vitongoji visivyozidi vitano (5); Bali
- Mkutano Mkuu wa Kijiji una madaraka ya kuamua idadi ya vitongoji katika kijiji
- Kila Kitongoji kilichoundwa kitakuwa na Mwenyekiti ambaye atachaguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa.
Madaraka na Majukumu ya Mwenyekiti wa Kitongoji
- Ni mjumbe wa halmashauri ya kijiji kwa wadhifa wake
- Kuwa kiungo katika halmashauri ya kijiji na wakazi wa kitongoji
- Kuimarisha umoja na mshikano kati ya serikali ya kijiji na wanakijiji
- Kuwasilisha maoni, mapendekezo na mahitaji ya kitongoji kwa halmashauri ya kijiji
- Kuwasilisha taarifa za halmashauri ya kijiji kwa wakazi wa kitongoji
- Kuitisha mikutano ya wakazi wa kitongoji pale anapoona inafaa ili kuendeleza mijadala ya kuibua maoni na mapendekezo ya kupeleka halmashauri ya kijiji
- Kuhamasisha wakazi wa kitongoji kwenye shughuli za maendeleo
- Kutunza rejesta ya wakazi wa kitongoji
Mkutano Mkuu wa Kijiji
- Hiki ni chombo kikuu cha maamuzi katika kijiji
- Mkutano Mkuu upo kwa mujibu wa sheria
- Wajumbe ni wanakijiji wote waliofikia umri usiopungua miaka 18
- Hakuna akidi maalaum kila kijiji hujiwekea akidi yake inayofaa, ni kati ya 20% hadi 33% ya wanakijiji hukutana kila baada ya miezi mitatu, kikao cha dharura kinaweza kuitishwa na halmashauri ya kijiji kukiwa na haja ya kufanya hivyo
- Taarifa ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Kijiji hutolewa siku saba (7) kabla ya mkutano
- Kila baaada ya miaka mitano kunakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji
- Mkazi wa kijiji anayegombea nafasi ya uongozi kwenye halmashauri ya kijiji au uenyekiti wa kijiji lazima awe na umri usiopungua miaka 21
- Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu ni Mwenyekiti wa Kijiji akisaidiwa na Mtendaji wa Kijiji kama Katibu
- Mwenyekiti na Mtendaji wa Kijiji hupanga ratiba za mikutano, kuandaa na kuitisha Mikutano ya Kijiji.
Madaraka na Majukumu ya Mkutano Mkuu wa Kijiji
- Kusimamia na kuwajibisha watendaji
- Kuweka taratibu za namna ya kuitisha mikutano ya dharura
- Kupokea, kujadili na kufanyia maamuzi taarifa za utekelezaji wa shughuli za kijiji kutoka halmashauri ya kijiji
- Kupokea, kujadili na kufanyia maamuzi taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za kijiji
- Kupokea, kujadili na kufanyia maamuzi mapendekezo ya kodi, ushuru na vyanzo vingine vya mapato ya kijiji
- Kupokea na kujadili taarifa ya makusanyo ya fedha za kodi, ushuru na mapato mengine ya kijiji
- Kupokea, kujadili na kufanyia maamuzi juu ya mapendekezo ya halmashauri ya kijiji ya kutunga sheria ndogo
- Kupokea, kujadili na kufanyia maamuzi ya ugawaji wa ardhi usiozidi ekari 50 na matumizi ya rasilimali nyingine za kijiji
- Kuiondoa madarakani halmashauri ya kijiji au mjumbe yeyote kabla ya muda wake
- Kupitisha azimio la kukaripia rasmi mjumbe yeyote wa halmashauri au halmashauri kwa ujumla kwa utendaji mbovu
- Ni chombo cha maamuzi ya mwisho juu ya masuala ya kijiji
- Kuidhinisha mpango wa maendeleo ya kijiji
Majukumu na Kazi za Mwenyekiti wa Kijiji
- Ni msemaji Mkuu wa kisiasa na mwakilishi wa serikali ya kijiji
- Kuwakilisha kijiji katika vikao au mikutano ya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC)
- Kuitisha na kuongoza mikutano ya halmashauri ya kijiji na mikutano mikuu ya kijiji
- Kusimamia na kuhamasisha wakazi wa kijiji katika kutekeleza shughuli za maendeleo
- Kuwaongoza na kuwahamasisha wakazi wa kijiji washiriki katika mikutano ya hadhara inayoandaliwa na Serikali au halmashauri ya Kijiji
- Kuwasilisha maamuzi/maazimio ya vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata na ya Halmashauri ya Wilaya kwenye vikao au mikutano ya kijiji
- Kutunza rejesta ya wakazi wote wa kijiji
- Kusimamia na kuhamasisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao kushirikiana na Mtendaji wa Kijiji kukusanya mapato ya kijiji na ya halmashauri ya wilaya
- Kushughulikia migogoro midogo midogo isiyolazimika kushughulikiwa na mabaraza ya ardhi ya vijiji au kata au mahakama ya mwanzo
Halmashauri ya Kijiji
- Ni chombo kikuu cha utendaji katika utawala wa kijiji
- Hukutana mara moja kila mwezi, mikutano ya dharura inaweza kuitishwa
- Akidi ya vikao vya halmashauri ya kijiji ni nusu ya wajumbe wote wa halmashauri ya kijiji
- Wakati mkutano mkuu ni kama Bunge, halmashauri ya kijiji ni kama serikali tendaji
- Huchaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kila baada ya miaka mitano.Mkazi wa kijiji mwenye umri usiopungua miaka 21 ana sifa ya kuchaguliwa kwenye halmashauri ya kijiji
- Wajumbe wa halmashauri ya kijiji wanatakiwa wasizidi 25 na wasipungue 15. Mkutano Mkuu kwa kushauriana na msimamizi wa uchaguzi watakubaliana idadi ya wajumbe wanayotaka kutokana na mazingira yao kutegemea na wingi wa wakazi wa ukubwa wa eneo lao (idadi ya vitongoji)
- Wajumbe wa halmashauri ya kijiji ni mwenyekiti wa kijiji, wenyeviti wa vitongoji, wanawake wasiopungua theluthi moja (1/3) ya wajumbe wote na wajumbe wengine watakaochaguliwa kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa.
- Mwenyekiti wa kijiji ni mwenyekiti wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa Mkutano Mkuu
- Mtendaji wa Kijiji ndio katibu wa Halmashauri ya kijiji
Mamlaka na Majukumu ya Halmashauri ya Kijiji
- Kutafakari maamuzi, mapendekezo ya Mkutano Mkuu wa Kijiji na kubuni mbinu na njia za kutekeleza
- Halmashauri ya kijiji ni chombo ambacho kimepewa nguvu zote za kiserikali katika mambo yote ya uhusiano na kijiji
- Halmashauri ya kijiji inaweza kuanzisha kamati za kudumu na vile vile kuteua kamati maalum kama inaona ni muhimu
- Wajumbe wa halmashauri wenyewe wakiwa hawaridhiki na utendaji wa Mwenyekiti wa Kijiji wana haki ya kumuazimia kwa kura theluthi mbili (2/3) ya wajumbe wote na kuitisha Mkutano Mkuu wa kijiji ili kujadili na kutoa maamuzi juu ya utendaji wa Mwenyekiti..
- Kupokea taarifa za mikutano ya vitongoji na kamati zake kufanyia kazi na kupeleka kwenye mkutano mkuu wa kijiji
- Kupokea, kutafakari na kufanyia kazi maagizo na mapendekezo kutoka Kamati ya Maendeleo ya Kata ( WDC) na halmashauri ya wilaya
- Kubuni na kupendekeza sera na mwelekeo wa kijiji kwa mkutano mkuu wa kijiji
- Kuandaa na kupendekeza mipango ya maendeleo ya muda mrefu kwa Mkutano Mkuu wa kijiji
- Kutunga sheria ndogo kwa kushauriana na Mkutano Mkuu wa Kijiji
- Kuwaalika wataalamu panapokuwa na haja ya kufanya hivyo ila hawatakuwa na haki ya kupiga kura
- Kupokea, kutafakari na kupendekeza kwa Mkutano Mkuu wa Kijiji maombi ya ugawaji wa ardhi isiyozidi ekari 50 na rasilimali zingine kwa maamuzi
- Kumiliki mali na kuingia mikataba kwa niaba ya kijiji
Kamati za halmashauri ya kijiji
- Kuna kamati tatu za Halmashauri ya Kijiji
- Kamati ya Fedha, Mipango na Uchumi,
- Kamati ya huduma za Kijamii na Shughuli za kujitegemea na
- Kamati ya Ulinzi na Usalama
- Mkutano Mkuu wa Kijiji una uwezo wa kuagiza Halmashauri ya Kijiji kuunda kamati ya muda kwa shughuli maalum au halmashauri yenyewe inaweza kuunda kukiwa na haja ya kufanya hivyo
- Idadi ya wajumbe katika kamati inashauriwa wasipungue wajumbe watatu (3) na wasizidi wajumbe watano (5)
- Kamati za kisheria zinafaa ziongozwe na mjumbe wa halmashauri ya kijiji
- Inashauriwa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji wasiwe Wenyeviti wa kamati mbalimbali ili kutolimbikiza madaraka yote kwa halmashauri ya kijiji
- Wananchi wa kawaida wanaweza kuwa wajumbe wa kamati au wanaweza kuitwa kutoa ushauri kwenye vikao vya kamati
- Kazi na majukumu ya kamati ni kuishauri Halmashauri ya Kijiji juu ya masuala mbalimbali ya kijiji
- Kamati zinaweza kukutana mara kwa mara kuendesha vikao kwa kushauriwa na Mtendaji wa kijiji
Mkutano wa Wakazi wa Mtaa
- Hufanyika kila baada ya miezi miwili
- Kuna vikao sita(6) kwa mwaka
- Mtaa kama ilivyo kwa Kitongoji sio eneo la utawala bali ni eneo la uratibu tu ambapo mawazo yote hupelekwa kwenye kata(WDC) na hatimaye halmashauri ya wilaya ama ya mji/jiji kwa maamuzi
- Wajumbe ni wakazi wote wa mtaa ambao wamefikisha umri wa miaka 18
- Mtendaji wa Mtaa ndiye Mtendaji Mkuu wa Mtaa na katibu wa vikao vyote vya mtaa
- Taarifa ya kuitisha mkutano mkuu wa mtaa hutolewa ndani ya siku saba kabla ya mkutano
Kamati ya Mtaa
- Ina wajumbe sita
- Huchaguliwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mtaa toka miongoni mwa wakazi wa mtaa
- Hujadili na kupitisha taarifa zote muhimu za mtaa ikiwemo mapato na matumizi
- Hupanga na kuhakikisha upitishwaji wa ratiba za vikao vya mkutano wa wakazi na kamati ya mtaa
- Kamati ya mtaa kupitia mkutano wa wakazi wa mtaa inaweza kupendekeza kwa halmashauri ya wilaya ili Mtendaji wa Mtaa aondolewe au achukuliwe hatua na kuwajibishwa
Majukumu ya Kamati ya Mtaa
- Kutekeleza sera za halmashauri
- Kushauri kamati ya Maendeleo ya Kata kwa masuala yanayohusu ulinzi na usalama na shughuli na mipango ya maendeleo
- Kutunza taarifa za wakazi wa mtaa
- Kufanya jambo lolote kama litakavyoelekezwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata
Mtendaji wa Kijiji/Mtaa
Ni mwajiriwa wa Halmashauri ya mji/jiji/wilaya huwajibika kwa Halmashauri ya wilaya /mji/jiji na huwajibika pia kwa serikali ya kijiji/mtaa
- Ni Mtendaj na msimamizi wa shughuli zote za maendeleo za kijiji/mtaa
- Mtunzaji wa kumbukumbu zote za kijiji/mtaa za vikao vya kijiji/mtaa pamoja na hati ya kuandikishwa kijiji, mali za kijiji/mtaa, rejesta ya kijiji/mtaa na barua zote
- Mshauri mkuu wa wananchi na mhamasishaji wa utekelezaji wa shughuli zote za maendeleo ya kijiji/mtaa
- Mwasilishaji taarifa zote muhimu za kijiji/mtaa kwa Afisa Mtendaji wa Kata
- Mlinzi wa amani (anaweza kumkamata mtu yeyote anayeonekana kuhatarisha amani katika kijiji chake au mtaa wake)
- Msimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogo katika kijiji chake au mtaa wake
- Kupanga na kuhakikisha kupitishwa ratiba za vikao vya mkutano mkuu na halmashauri ya kijiji/mtaa
- Kwa kushirikiana na mwenyekiti kuandaa ajenda za vikao mbalimbali vya mtaa kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Kijiji au mkutano wa wakazi wa mtaa pamoja na makisio na hesabu za mapato na matumizi
- Kuwashauri wenyeviti wahusika juu ya taratibu za kuendesha vikao, kufanya maamuzi na kuandika muhtasari ya vikao na kuhifadhi katika daftari
- Kufanya mawasiliano na ngazi zingine za utawala kwa niaba ya kijiji/mtaa
- Msimamizi wa mapato na kodi za kijiji /mtaa
- Msambazaji wa habari na taarifa mbalimbali kijijini/kwenye mtaa
- Kuwa daraja kati ya kijiji/mtaa na asasi zingine kijijini/kwenye mtaa au nje ya kijiji/mtaa kama zahanati, shule, mashirika yasiyo ya kiserikali n.k
- Mfuatiliaji wa miradi ya kijiji /mtaa na kutoa taarifa kwenye halmashauri ya kijiji au kamati ya mtaa
- Mfuatiliaji wa utekelezaji wa maamuzi ya vikao mbalimbali vya kijiji/mtaa
- Muandaaji wa semina na warsha za wanakijiji/wakazi kwenye mtaa na viongozi wa kijiji/mtaa katika kijiji/mtaa
- Halmashauri ya kijiji au kamati ya mtaa kupitia Mkutano Mkuu wa kijiji au Mkutano wa Wakazi wa Mtaa inaweza kupendekeza kwa halmashauri ya mji au jiji ili Afisa Mtendaji wa kijiji au Afisa Mtendaji wa Mtaa aondolewe au achukuliwe hatua na kuwajibishwa
- Hufanya lolote linalofaa kuboresha utawala na utendaji wa serikali ya kijiji/mtaa
Majukumu ya Mwenyekiti wa Mtaa
- Ni Msemaji wa mtaa na kiongozi mkuu na kisiasa katika ngazi ya mtaa
- Ni Mwenyekiti wa mikutano yote ya Kamati ya Mtaa na Mkutano Mkuu wa Mtaa
- Kusuluhisha migogoro midogomidogo ambayo haistahili kuitisha mkutano wa Kamati ya Mtaa au kupelekwa kwenye Baraza la Kata au Mahakama.
- Kuwaongoza na kuwahimiza wakazi wa mtaa washiriki shughuli za maendeleo, sherehe za Taifa, mikutano ya hadhara itakayoandaliwa na mtaa, Halmashauri ya Mji, Manispaa au Jiji na Serikali.
- Kuwakilisha mtaa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata
- Kutekeleza kazi atakazopewa na Kamati ya Mtaa na Mkutano wa Mtaa na Kamati ya Maendeleo ya Kata.
- Kusimamia utekekelezaji wa kazi na majukumu ya Kamati ya Mtaa
- Kusimamia utunzaji wa rejesta ya wakazi wote wa mtaa
- Kuwakilisha maamuzi/maazimio ya vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata na ya Halmashauri ya Mji, Manispaa, au Jiji kwenye vikao au mikutano ya mtaa
- Kusimamia suala zima la afya katika eneo lake na kampeni za afya za kitaifa, kimkoa na kiwilaya dhidi ya magonjwa ya kuambukiza
- Kusimamia na kuhamasisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao kama vile polisi jamii
Wajibu Na Haki Ya Kila Mwananchi Katika Kijiji/Mtaa
- kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo
- Kuhudhuria mikutano yote katika Kitongoji, Kijiji na Mtaa na
- kuhakikisha kuwa mikutano yote inafanyika ndani ya muda uliopangwa
- Kulinda mali, rasilimali za umma na kupambana na kila aina ya uovu ikiwemo ubadhirifu, wizi rushwa na mengineyo kwa mujibu wa sheria
- Kumwondoa kiongozi au viongozi wasiowajibika kwa kumpigia kura ya hapana
- Kujenga na kuimarisha mshikamano uliopo katika jamii yake
- Kushiriki kupanga, kutekeleza, kusimamia na kutathmini pamoja na kuhoji utekelezaji wa miradi yote katika kitongoji, kijiji au mtaa
- Kushiriki katika kupiga au kupigiwa kura na kugombea nafasi za uongozi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa
- Kuwaheshimu viongozi wake
- Kupata taarifa za mapato na matumizi ya fedha za kitongoji, kijiji na mtaa
- Kushiriki katika shughuli zote za kisiasa katika kijiji, mtaa na kitongoji chake
- Kushirikishwa na kiongozi wake katika shughuli mbalimbali za maendeleo
- Kujua mipango mbalimbali ya maendeleo iliyopangwa katika kitongoji, kijiji na mtaa wake
- Kuhakikisha kuwa kiongozi wake aliyemchagua anatimiza wajibu wake ipasavyo
- Kudai haki zake za msingi kutoka kwa kiongozi wake
- Kuelewa sheria zote zilizopo katika kitongoji, kijiji na mtaa wake na kuishi kufuatana na sheria hizo
- Kutoa taarifa ya vitendo viovu kama rushwa, ubadhirifu na wizi katika ngazi husika kwa polisi na kwa Afisa Mtendaj wa kijiji/Mtaa
Ushiriki Na Ushirikishwaji Wa Wananchi
Huu ni mchakato unaohusu kuhusika na kuhusishwa kwa mwananchi katika Upangaji Utekelezaji, Usimamizi na Tathmini ya mipango mbalimbali ya maendeleo katika kijiji au mtaa. Vilevile kushiriki kutambua changamoto na kuweka vipaumbele ili kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuweka mikakati ya utekelezaji katika ngazi ya kijiji/mtaa. Ushiriki na Ushirikishwaji wa wananchi ni fursa ambayo mwananchi anapaswa kuitambua na kuifaidi ili kuleta tija kwenye maisha yake na jamii yake.
Fursa anazopata mwananchi zinaweza kuwa za kiraia ,kiuchumi ,kijamii na kiutendaji. Fursa ya kiraia ni kushiriki katika vikao rasmi vya maamuzi, kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi. Fursa za kiuchumi ni zile za kuinua kipato chake na cha familia yake na kuweza kuchangia pato la taifa ,fursa za kijamii ni namna ya kunufaika na huduma za jamii, ulinzi ,usalama na mahusano mema kwenye jamii yake na fursa za kiutendaji ni kushiriki kutekeleza maamuzi ya wananchi wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wao.
Suala la kushiriki na kushirikishwa katika vijiji/mitaa ni la lazima kwa sababu ni haki na wajibu wa Kikatiba wa kila mwananchi.
Umuhimu wa Ushiriki na Ushirikishwaji wa Wananchi
- Kuiwezesha Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kutoa huduma muhimu kwa watu wengi na kwa gharama nafuu kutokana na nguvukazi na michango ya wananchi
- Kuwawezesha wananchi kujua nafasi yao katika jamii na kutambua ushiriki na ushirikishwaji kama njia ya kuwapatia demokrasia
- Kuwawezesha wananchi kutambua changamoto walizonazo na kuzitatua kwa kutumia rasilimali walizonazo
- Kuwawezesha wananchi kumiliki na kujivunia maendeleo yao wenyewe kwa kushirikiana na Serikali
- Kuwajengea uwezo na uzoefu katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo
- Kuwawezesha wananchi kuwa na taarifa sahihi na za wakati zinazohusu maisha yao na hivyo kufanya maamuzi sahihi na kuchangia maendeleo ya jamii yao.
Usimamizi Na Udhibiti Wa Matumizi Ya Rasilimali Za Umma Katika Kijiji/Mtaa
Wananchi wanaweza kushiriki kusimamia na kudhibiti matumizi ya rasilimali za Umma katika Kijiji/Mtaa kupitia:
- Kufanya maamuzi katika vikao mbalimbali
- Kuhoji utendaji wa viongozi wao kupitia vikao mbalimbali
- Kuhamasisha uwazi katika mapato na matumizi ya rasilimali mbalimbali za Kijiji/Mtaa
- Kuhakikisha kuwa taarifa za mapato na matumizi zinasomwa kwa kila robo mwaka
Kusimamia Viongozi Wa Vijiji/Mitaa
Wananchi wanaweza kuwasimamia viongozi wao kupitia:
- Kuchagua viongozi waadilifu
- Kuhoji utendaji wa viongozi katika vikao mbalimbali vya kisheria.
- Kuhakikisha uwepo wa uwazi katika uendeshaji wa shughuli za serikali ya Kijiji/mtaa
- Kuwaondoa madarakani viongozi wasio waadilifu kwa njia ya vikao halali kabla ya uchaguzi