Skip to main content
Mjue Diwani

Mjue Diwani

Nchi yetu imekuwa ikifanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali wakiwemo Rais, Wabunge na Madiwani kila baada ya miaka mitano au kwa mujibu wa sheria pale itakapo hitajika. Wananchi hupata nafasi ya kuelimishwa umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura au kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali. Haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya msingi inayotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maudhui ya kitabu hiki yanatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, na Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Madiwani (Tangazo la Serikali Na. 280 la mwaka 2000). Kitabu hiki kinaeleza maana ya Diwani, aina za madiwani, namna  Diwani anavyopatikana, sifa za kuwa Diwani, majukumu ya Diwani na maadili ya Diwani.

Diwani Ni Nani?

 1. Ni Mwakilishi wa wananchi kwenye Halmashauri
 2. Ni Mjumbe wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri ya Wilaya, Mji, , Manispaa au Jiji).
 3. Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata

Kuna Aina Ngapi Za Madiwani?

Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, zinataja aina nne za madiwani, ambao ni:

 1. Madiwani wa kuchaguliwa;
 2. Madiwani wa kuteuliwa;
 3. Madiwani wa viti maalum (wanawake); na
 4. Wabunge (wa kuchaguliwa, viti-maalumuau kuteuliwa).

Diwani Anapatikanaje?

 1. Kwa kuchaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano;
 2. Kwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi mdogo pindi nafasi ya Diwani inapokuwa wazi kwa sababu za: kifo cha Diwani; Diwani kukosa

Sifa za kuwa Diwani kwa mujibu wa sheria; kubatilishwa kwa uchaguzi wa Diwani; nafasi ya Diwani kuwa wazi kwa mujibu wa Sheria; na Diwani kukoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichomteua akiwakilishe; na

 1. Kwa kuteuliwa na chama chake (kwa madiwani wa kuteuliwa wa viti maalum).
 2. Kuteuliwa na Waziri mwenye dhamana pale inapobidi (kifungu cha sheria)

Sifa Za Kugombea Udiwani

Mtu anaweza kugombea na kuchaguliwa kuwa Diwani iwapo anakidhi sifa zifuatazo:

 1. Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 2. Awe ametimiza umri wa miaka  21 au zaidi;
 3. Awe na akili timamu;
 4. Awe ni mkazi wa eneo la Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika;
 5. Anaweza kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza;
 6. Awe ni mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 na chama chake kimemteua akiwakilishe kwenye uchaguzi husika;
 7. Awe na njia halali za kujipatia kipato;
 8. Asiwe amehukumiwa kwa kosa la ukwepaji kodi ndani ya kipindi cha miaka mitano kabla ya uchaguzi; na
 9. Asiwe amehukumiwa kifo au amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita jela.

Diwani Ana Majukumu Gani?

Majukumu ya Diwani yanatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288; na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Kwa ujumla Majukumu ya Diwani ni:

 1. Uwakilishi wa wananchi katika vikao na mikutano ya Halmashauri ;
 2. Kuongoza wananchi kwa umakini na uadilifu;
 3. Usimamizi wa rasilimali na sheria;
 4. Kupitisha mipango na bajeti za Halmashauri;
 5. Kushiriki Michakato ya Utungaji na upitishaji wa Sheria ndogo;
 6. Kuwawezesha wanajamii wa eneo lake kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo;
 7. Kuongoza na kufanikisha wananchi wake katika kutatua migogoro mbalimbali katika kata; na
 8. Kuhamasisha shughuli za maendeleo katika eneo lake la kazi.

Diwani Anamwakilisha Nani?

Kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinaeleza kuwa Diwani ni mwakilishi wa wananchi kwenye Kata aliyochaguliwa.

 Diwani kama Mwakilishi wa wananchi ana wajibu gani?

Diwani kama Mwakilishi wa wananchi ana wajibu ufuatao:

 1. Kuwakilisha wananchi wa Kata yake katika vikao vya Halmashauri;
 2. Kufuatilia maendeleo ya jitihada za jamii na usaidizi wa Halmashauri katika jitihada hizo;
 3. Kutafuta Rasilimali na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa;
 4. Kuhudhuria na kushiriki vikao na mikutano ya Halmashauri;
 5. Kuwa kiungo kati ya wananchi na Halmashauri husika;
 6. Kutetea maslahi ya watu wa eneo analoliwakilisha;
 7. Kukutana na wananchi katika eneo lake ili kusikiliza na kuchukua maoni, mapendekezo, kero na matatizo ya watu wa eneo analoliwakilisha;
 8. Kutoa taarifa kwa wapiga kura kuhusu maamuzi ya jumla   ya Halmashauri na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ili kuondoa matatizo yaliyowahi kuelezwa na wakazi wa eneo lake la uchaguzi; na
 9. Kusimamia na kudhibiti utumiaji wa rasilimali ya umma kupitia kamati za kudumu za madiwani.

Je! Diwani ni Mwajiriwa wa Halmashauri?

Diwani si mwajiriwa wa Halmashauri, bali ni “Mwakilishi wa watu”, na hivyo anawajibika kwa watu anaowawakilisha na wakazi wa eneo la Halmashauri yake.

Diwani Kama Kiongozi Ana Wajibu Gani?

 1. Kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo;
 2. Kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu vita dhidi ya umaskini, rushwa na janga la UKIMWI;
 3. Kuhamasisha ushirikiano kati ya jamii, wadau wa maendeleo, na AZAKI katika kuanzisha, kukuza na kuendeleza jitihada za jamii;
 4. Kushirikisha wananchi katika uandaaji,utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini wa mipango na bajeti za maendeleo;
 5. Kuitisha na kuendesha vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata (Ward Development Committee -WDC);
 6. Kushiriki katika kufikia maamuzi na kutoa maelekezo kupitia vikao na mikutano halali ya baraza la madiwani;
 7. Kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na kuhifadhi maliasili za nchi;
 8. Kuhakikisha kwamba watumishi wote waliopo katika eneo  la kata yake wanafanya kazi zao kwa uadilifu na ufanisi na endapo utendaji wao hauridhishi anapaswa kutoa taarifa kwenye kamati husika au kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri yake;
 9. Kuhamasisha na kuzingatia misingi ya utawala bora wakati wa utekelezaji wa majukumu yake; na
 10. Kuhamasisha wananchi kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri husika.

Je! Diwani ni Mtendaji?

Diwani si Mtendaji, bali ni Kiongozi na Mwakilishi wa wananchi, hivyo:

 1. Diwani hapaswi kuingilia utendaji wa idara yoyote katika Halmashauri kwa maslahi yake binafsi;
 2. Diwani hapaswi kutoa maelekezo, amri au maagizo kwa mwajiriwa au wakala yoyote wa Halmashauri; na
 3. Diwani hapaswi kuzuia au kujaribu kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la madiwani au kamati au mwajiriwa au wakala wa Halmashauri.

Diwani Kama Msimamizi Wa Rasilimali Za Umma Ana Wajibu Gani?

 1. Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani;
 2. Kufuatilia matumizi ya fedha za Halmashauri kwa lengo la kujiridhisha kuwa matumizi ya fedha hizo hayavuki bajeti iliyoidhinishwa na kwamba fedha zote zimetumika kwa madhumuni yaliyopangwa;
 3. Kusimamia matumizi bora ya rasilimali za umma kwenye Halmashauri yake;
 4. Kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata yake;
 5. Kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Taratibu, Kanuni, , Sheria ndogo na Miongozo ya Halmashauri;
 6. Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi, mipango na utoaji wa huduma katika kata yake na kutoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri au kamati za Halmashauri endapo kuna kasoro za msingi za utekelezaji;
 7. Kushiriki katika kufanya maazimio na maamuzi ya kuwawajibisha watendaji wazembe na wasio waadilifu; na
 8. Kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Diwani Kama Msimamizi Wa Ugawaji Wa Rasilimali Ana Wajibu Gani?

 1. Kuwashirikisha wananchi katika kuainisha vyanzo vya mapato, mahitaji, fursa na vipaumbele vyao;
 2. Kuhakikisha ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato kulingana na mahitaji na vipaumbele vya wananchi;
 3. Kusimamia mchakato mzima wa mipango na bajeti;
 4. Kuidhinisha makisio ya mapato na matumizi ya Halmashauri baada ya kuzingatia tathmini ya mahitaji na rasilimali zilizopo; na
 5. Kuhakikisha kuwa kazi zilizopangwa zimetengewa bajeti.

Diwani Kama Mtunga Sheria: Amepata Wapi Mamlaka Ya Kutunga Sheria?

Diwani amepewa mamlaka ya kusimamia na kutunga sheria ndogo na kifungu cha 153 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287, kifungu cha 89 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Mji), Sura 288 na Kifungu cha 122 (1) (d) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287. Mamlaka haya hutekelezwa kupitia vikao halali vya Baraza la Madiwani.

Uwezo huu wa kutunga Sheria ndogo unahusisha mambo mawili:

 1. Kutunga Sheria ndogo zitakazotumika katika eneo la mamlaka yao; na
 2. Kupitisha sheria ndogo zilizotungwa na Halmashauri za vijiji zilizopo katika eneo la mamlaka yao kwa kupitia Baraza la Madiwani.

Sheria ndogo ni Zipi?

Sheria ndogo (by-laws) ni kanuni zilizotungwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge kwa ajili ya kurahisisha au kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya mamlaka husika au kusaidia utekelezaji wa sheria mama.

Diwani Kama Mwezeshaji Ana Wajibu Gani?

 1. Kusikiliza matatizo ya wananchi, kujadiliana na kuwashauri hatua za kuchukua mfano kutafuta mtaalam wa kilimo katika eneo lake;
 2. Kuwezesha watu kupata taarifa muhimu kuhusu masuala ya maendeleo;
 3. Kuwasaidia wananchi waone fursa zinazowazunguka katika nyanja za sekta kuu kama uchumi, maji, afya, miundombinu na elimu ;
 4. Kuwawezesha wananchi kupata mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kama vile kilimo, ujasiriamali, afya borana makazi bora kwa kutumia wataalamu waliopo ndani na nje ya Kata yake
 5. Kuhamasisha wananchi  kujitegemea kwa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao;
 6. Kuondoa urasimu usio wa lazima  kwa kuzingatia kisheria;
 7. Kufanikisha ushirikishwaji wa wananchi katika mipango, utekelezaji, usimamizi na tathmini  ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao; na
 8. Kuhamasisha ulinzi na usalama,  demokrasia, utawala bora na uzingatiaji wa sheria katika maeneo yao.

Diwani Anatakiwa Kuwa Na Mwenendo Gani?

Diwani anapaswa kuwa na mwenendo wenye maadili mema kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Madiwani kwa mujibu wa matangazo yanayomuhusu diwani.

Kwa kifupi, Diwani anapaswa awe na mwenendo ufuatao:

Kuendesha shughuli zake kwa kujenga imani kwa wananchi;

Kuheshimu na kuzingatia sheria;

Kutojiweka katika hali ya mgongano  wakimaslahi ;

 1. Kutotumia nafasi yake kwa faida yake, au familia yake na marafiki zake;
 2. Kutoshiriki katika majadiliano au kupiga kura kuhusu jambo ambalo ana maslahi nalo;
 3. Kutoa taarifa kuhusu maslahi na mali zake pale inapobidi kufanya hivyo;
 4. Kutokuwa na uhusiano wa kimapenzi usiokubalika kati yake na Diwani mwenzake au watumishi wa Halmashauri;
 5. Kuwajibika kwa jamii na Halmashauri yake kutokana na matendo yake na maamuzi ya Halmashauri;
 6.  Kuwa muwazi, mkweli na muaminifu;
 7. Kufanya maamuzi bila upendeleo au ubaguzi na kwa kuzingatia sheria na haki;
 8. Kuhakikisha kuwa habari zote za siri za wananchi zinahifadhiwa kwa mujibu wa sheria na hazitumiki kwa maslahi au faida binafsi.
 9. Kuheshimu nafasi na hadhi ya madiwani wenzake na watumishi wa Halmashauri;
 10. Kutoomba wala kupokea rushwa/hongo au zawadi kutoka kwa mtu anayemhudumia; na
 11. Kutoingilia utendaji wa kazi wa idara yoyote katika halmashauri.

Kwa Nini Ni Muhimu Diwani Kutekeleza Majukumu Yake?

Ibara ya 29 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa kila mtu katika Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu na matokeo ya kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa jamii.

Hivyo basi, Diwani kutekeleza majukumu yake ni muhimu kwa sababu, kwa kufanya hivyoanatekeleza haki za msingi za binadamu na anatii utawala wa sheria.