Skip to main content
Je, Unajya Kuhusu Mfumo wa Fursa na vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) Ulioboreshwa?

Je, Unajua Kuhusu Mfumo wa Fursa na vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) Ulioboreshwa?

Watanzania wamekuwa na desturi ya kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuboresha maisha yao. Desturi hii ilikuwepo na ilisimamiwa kwa kiasi kikubwa na Baba wa Taifa  Mwalimu Julius K. Nyerere. Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inaamini kwamba jamii itapata maendeleo makubwa kwa kuitumia na kuiendeleza.

Ili kutekeleza adhima ya Ugatuaji wa Madaraka kikamilifu, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilianzisha Mfumo wa Upangaji Mipango Shirikishi Jamii wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (Opportinities and Obstacles to Development - O&OD) wa mwaka 2001 (unaofahamika kama Mfumo wa O&OD wa awali) ambao ulirasimishwa na kutumiwa na MSM 105 kati ya 132 hadi kufikia mwaka 2010. Aidha Mfumo huo ulisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba mipango ya maendeleo inahusisha mahitaji halisi ya jamii katika ngazi za msingi (Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji).

Mchakato wa upangaji mipango kwa kutumia Mfumo wa O&OD wa awali ulijikita katika uibuaji wa vipaumbele vya jamii kwa kutegemea Serikali itekeleze vipaumbele hivyo. Kutokana na ufinyu wa bajeti sio vipaumbele vyote viliweza kutekelezwa, hivyo jamii kukosa hamasa ya kuendelea kushiriki kwenye zoezi la kuibua miradi na upangaji mipango.

Licha ya jamii kushiriki katika uibuaji wa vipaumbele vya miradi, umiliki wa mpango na bajeti ulibaki kuwa wa Halmashauri na kazi ya jamii iliishia katika uibuaji. Hivyo, Halmashauri ilikuwa na mamlaka ya kuamua nini kitekelezwe na kwa kiwango gani kulingana na bajeti au rasilimali zilizokuwepo.

Mchakato wa uibuaji wa vipaumbele vya miradi ya maendeleo ulifanya jamii kuamini kuwa baada ya kuibua miradi yao ya vipaumbele Serikali itatekeleza. Hali hii ilifanya jamii kujisahau na kuacha majukumu na wajibu wao kama watekelezaji wakuu wa maendeleo yao na kusubiri Serikali hata kwa mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wao. Aidha, utegemezi huu uliongezeka zaidi kutokana na baadhi ya wadau kutoa ahadi za kupeleka miradi mbalimbali katika jamii na hivyo jamii kusubiri pasipo kuchukua hatua yoyote.

Katika kutatua changamoto zilizoainishwa hapo juu, na kuliwezesha Taifa kufikia maendeleo endelevu, Serikali imefanya  maboresho katika Mfumo wa O&OD wa awali . Aidha mfumo huu unalenga kuboresha utoaji wa huduma na kusisitiza matumizi ya jitihada za jamii katika kufikia maendeleo. Msingi mkuu wa mfumo wa O&OD ulioboreshwa umejikita katika dhana ya kwamba wananchi ndio wahusika wakuu na wanufaika wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo yao bila kutegemea na kusubiri serikali ifanye kwa ajili yao.

Katika Mfumo wa O&OD Ulioboreshwa, wanajamii watapanga mipango yao kulingana na mahitaji halisi, uwezo wa ki-taasisi na rasilimali walizonazo kwa kushirikiana na MSM.

“Maendeleo katika ngazi za msingi” kwa muktadha wa Mfumo wa O&OD Ulioboreshwa yanatokana na utambuzi na matumizi bora ya rasilimali zilizopo ikijumuisha uwezo na uzoefu wa jamii yenyewe kutumia rasilimali hizo kwa maendeleo kulingana na sifa za kimazingira za eneo husika”.

Mfumo wa O&OD ulioboreshwa unahamasisha uibuaji na utekelezaji wa jitihada za jamii na ushirikiano baina ya Serikali na wanajamii ili kufikia utoaji huduma bora kwa maendeleo katika ngazi za msingi. Ikilinganishwa na Mfumo wa O&OD wa awali, Mfumo wa O&OD ulioboreshwa unatarajiwa kuleta faida ya moja kwa moja katika kuboresha utoaji huduma na maendeleo kama ifuatavyo:

 1. Kujenga Uwezo wa Jamii

Msingi wa Mfumo wa O&OD ulioboreshwa unatoa  hamasa kwa jamii kushiriki kutekeleza shughuli za maendeleo. Kutokana na ushiriki huo jamii inajenga uwezo wa kujiamini katika  kupanga na kutatua changamoto zinazowakabili. Uzoefu wa kutekeleza jitihada moja wanaoupata wanajamii, ndio unaosaidia kutekeleza jitihada nyingi na bora zaidi

 1. Uendelevu wa Miradi

Mfumo wa O&OD ulioboreshwa unasisitiza umuhimu wa kuijengea uwezo jamii ili iweze kuanzisha na kutekeleza miradi yao wenyewe. Dhana hii inawezesha kuwa na miradi endelevu hasa kutokana na jamii kuwa na umiliki wa miradi inayotokana na mahitaji yao halisi, uwezo walionao na rasilimali zilizopo, hivyo kuwa na uwezo wa kutekeleza, kufanya ufuatiliaji na tathmini wao wenyewe.

 1. Kupungua kwa Gharama za Utekelezaji wa Miradi

Kutokana na ushiriki wa jamii katika utekelezaji wa miradi, kunasaidia kupunguza gharama kwa Serikali na hivyo kuwezesha Serikali kujikita katika utekelezaji  miradi ya kimkakati ambayo iko juu ya uwezo wa jamii kuitekeleza.

 1. Kuimarisha Mahusiano na Ushirikiano baina ya Serikali na Jamii

Mfumo wa O&OD ulioboreshwa unaiwezesha Serikali kutoa usaidizi katika juhudi za jamii za kujiletea maendeleo kwa kuzingatia hali halisi. Kupitia Mfumo wa O&OD ulioboreshwa Serikali na jamii) zitatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na maendeleo endelevu katika ngazi za msingi.

 1. Utawala Bora katika Ngazi za Msingi

Mchakato wa uibuaji na utekelezaji wa jitihada za jamii, hufanyika kupitia vikao mbalimbali vya maamuzi katika ngazi za Vitongoji, Vijiji na Mitaa. Mchakato huu hufanyika kwa njia ya uwazi na hivyo kuimarisha uzingatiaji wa nguzo za utawala bora zinazojumuisha uwazi na uwajibikaji katika kufikia maamuzi ya kidemokrasia.

 1. Maendeleo ya Kiuchumi katika Ngazi za Msingi

Mfumo wa O&OD unachangia maendeleo ya kiuchumi katika ngazi za msingi kupitia uwezeshaji wa shughuli za vikundi zinazofanyika ndani ya jamii. Mipango bora ya maendeleo ya kiuchumi katika ngazi za msingi itahakikisha kuwa masuala ya vipaumbele yanashughulikiwa kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuwezesha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini katika ngazi za msingi. MSM zinatakiwa kutoa usaidizi kwa jamii ili kuwezesha ukuaji wa uchumi katika maeneo yao.

 

Mfumo wa O&OD una lengo la kujenga na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya jamii na MSM katika utoaji wa huduma na kuleta maendeleo ya jamii katika ngazi za msingi. Mfumo huu unalenga kuhakikisha kuwa jamii inajengewa uwezo wa kutekeleza mipango ya maendeleo kupitia jitihada za jamii.

Uhusiano na Ushirikiano ni njia muhimu inayoziwezesha jamii na MSM kufanya kazi kwa pamoja katika utoaji wa huduma na kuleta maendeleo katika ngazi za msingi, ambapo:

 1. Jamii huibua na kutekeleza jitihada zake kadri iwezekanavyo katika kukabiliana na   changamoto bila kusubiri msaada wa Serikali;
 2. Halmashauri za Vijiji/Kamati za Mitaa ni ngazi za utawala zenye wajibu wa kushirikiana na wana jamii (ambao ni watekelezaji wakuu wa mipango yao) ili kuboresha maisha ya jamii;
 3. Halmashauri zinapaswa kuzihimiza ngazi za utawala za Vijiji/Mitaa kuwa kitovu cha kuimarisha utekelezaji wa jitihada za jamii.

Maendeleo katika Ngazi za Msingi kwa Mfumo wa O&OD unahusisha kutambua matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo ndani ya jamii katika ngazi za msingi kwa kuzingatia tabia ya jamii na mazingira ya eneo husika. Ili kufikia malengo ya utoaji huduma bora na kuleta maendeleo katika ngazi za msingi msisitizo unapaswa kuwa katika kuimarisha jitihada za jamii na kuzijengea uwezo jamii kwa ushirikiano kati ya Serikali na jamii.

Jitihada za jamii ni shughuli za pamoja au miradi ambayo wanajamii kwa utashi wao wenyewe wanaipanga, wanaitekeleza, kuifanyia ufuatiliaji na tathmini ili kukabiliana na changamoto walizonazo. Wanajamii watachukua hatua kutatua matatizo yanayowakabili bila kusubiri usaidizi wa Serikali au wadau wengine wa maendeleo. Jamii huchukua hatua hii kwa kuwa inaona kuna umuhimu na ulazima wa kufanya hivyo.

Kuzijengea uwezo jamii inahusisha mchakato wa kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa jamii katika shughuli za maendeleo. Mchakato huu huziwezesha jamii kubaini changamoto na fursa zilizopo, kisha kwa pamoja huchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto walizozibaini.

Jamii inaweza kujenga uzoefu zaidi kutokana na kuendelea kutekeleza jitihada za jamii. Hii inamaanisha kwamba mafanikio ya jitihada moja huipa jamii ari ya kutekeleza jitihada nyingi zaidi na hatimaye jamii hujenga uzoefu na kujiamini katika kutekeleza shughuli za maendeleo.

Mchakato wa maendeleo ya jamii na usaidizi wa MSM katika kuzijengea uwezo jamii ni vipengele vinavyopaswa kuzingatiwa katika kufanikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali na jamii.

Mchakato wa maendeleo ya jamii kwa muktadha wa Mfumo wa O&OD ni dhana endelevu inayowezesha jamii kuungana pamoja ili kufanikisha jitihada zake na kujijengea uwezo wa kujiletea maendeleo. Mchakato huu hupitia hatua muhimu nne (4), ambazo ni:

 1. Maandalizi ya Jamii

Maandalizi ya jamii ni mchakato wa kuongeza uelewa ndani ya jamii ili iweze kutambua hali halisi ya jamii husika, changamoto zinazowakabili pamoja na fursa walizonazo katika kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja. Wakati wa maandalizi, jamii inapaswa kutambua mahitaji yake halisi pamoja na uwezo walionao katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa kuzingatia uzoefu katika kutekeleza jitihada za jamii. Viongozi wa Kijiji/Mtaa hupatiwa mafunzo katika hatua hii ili waweze kuwa chachu ya kujenga mwamko wa maendeleo ndani ya jamii.

 1. Upangaji wa Mipango ya Jamii

Upangaji wa mipango ya jamii ni mchakato unaofanywa na wanajamii kwa kujadiliana na kuweka vipaumbele kisha kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto walizonazo kwa kuanzisha miradi yao. Katika upangaji wa mipango, jamii inapaswa kuzingatia uwezo wao na rasilimali walizonazo pamoja na uendelevu wa miradi husika. Aidha, kwa miradi iliyo nje ya uwezo wao kuitekeleza, jamii inapaswa kutafuta usaidizi kutoka kwa wadau wengine kama vile; MSM, Taasisi binafsi, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo.

 1. Utekelezaji

Wanajamii ndio wahusika wakuu katika utekelezaji wa jitihada za jamii zilizopo katika mipango yao ya maendeleo. Aidha, MSM zinapaswa kuainisha aina ya usaidizi na wakati unaofaa kutoa usaidizi huo kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa jitihada za jamii.

 1. Ufuatiliaji na Tathmini

Ufuatiliaji ni mchakato endelevu unaofanywa na wanajamii ili kuangalia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa jitihada za jamii, kutambua changamoto na hatua za kurekebisha utekelezaji pale inapobidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Tathmini ni mchakato wa kutambua na kutafakari matokeo ya uhusiano kati ya shughuli zilizopangwa na zilizotekelezwa katika kufikia malengo yaliyokusudiwa. Matokeo ya ufuatiliaji na tathmini husaidia kuboresha upangaji na utekelezaji wa mipango ijayo. Pia, husaidia kuijengea uwezo jamii kujifunza kupitia changamoto walizokabiliana nazo katika utekelezaji wa mipango yao.

Jukumu la msingi la MSM katika Mfumo wa O&OD ni kuzijengea uwezo jamii ili kutekeleza jitihada zake kwa kutoa usaidizi katika hatua zote za mchakato wa maendeleo ya jamii. Jukumu hili hufanywa na MSM ili kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya Serikali na jamii. Hivyo, MSM zinapaswa kutoa usaidizi katika uwezeshaji wa jamii pamoja na kusaidia jitihada za jamii.

Uwezeshaji wa jamii ni muhimu katika kufanikisha mchakato wa maendeleo katika ngazi za msingi. Jamii hujifunza kutokana na uzoefu unaoimarishwa kwa uwepo wa wawezeshaji ambao huwa karibu na jamii wakati wa hatua zote za Mchakato wa maendeleo ya jamii. Hivyo, MSM zina jukumu la kuandaa wawezeshaji miongoni mwa maafisa ugani ambao watajengewa uwezo kuwa Wawezeshaji Kata.

Wawezeshaji Kata hupaswa kuwezesha jamii katika mchakato wa maendeleo ya jamii ili kuijengea Jamii uzoefu na uwezo wa kutosha. Hivyo, Wawezeshaji Kata wanapaswa kufanya kazi kama timu yenye angalau wawezeshaji watatu (3) ili kufanya kazi zao kwa ushirikiano na kushughulikia masuala ya sekta mbalimbali yatakayojitokeza.

Kupitia mchakato wa maendeleo ya ngazi za msingi, jamii huibua miradi na kupanga mipango ya maendeleo. Mipango hiyo huwasilishwa ofisi za MSM ili kujumuishwa katika mipango na bajeti ya Halmashauri. Usaidizi unaopaswa kutolewa na MSM upo wa aina tatu (3) kama ifuatavyo:

 1. Kutia Moyo

Kutia moyo ni matendo yote ya kutambua na kuipongeza jamii kwa jitihada zake. Matendo hayo yanahusisha kuwatembelea na kuzungumza nao pamoja na kuwasaidia shughuli wanazozifanya, kutuma barua ya pongezi, kutoa cheti, tuzo au ngao. Kutia moyo ni muhimu kwa kuwa husaidia jamii kuendelea kuongeza bidii katika kutekeleza jitihada zao. Inashauriwa wakati wowote MSM kuwatia moyo wanajamii ili kuendeleza ushiriki katika jitihada zao hata wanapokuwa katika wakati mgumu kiuchumi na kijamii.

     2. Usaidizi wa Kitaalam

Usaidizi wa kitaalam ni utoaji wa ujuzi na taarifa ambazo jamii inazihitaji ili kuwezesha jitihada kuendelea kutekelezwa. Usaidizi huu unahusu mambo kadhaa yakiwemo; utaalam, viwango vya Serikali vinavyotakiwa, taarifa za Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu. MSM zinapaswa kutoa usaidizi pale ambapo jitihada za jamii zinahitaji maarifa na ujuzi ambao haupatikani miongoni mwa wanajamii.

     3. Usaidizi wa Fedha

Usaidizi wa fedha ni utoaji wa fedha tasilimu au vifaa kwa jamii. MSM zinapaswa kuzitia moyo jamii kukamilisha jitihada zao isipokua kama jitihada inahitaji fedha au vifaa ambavyo vipo nje ya uwezo wa jamii ndipo MSM zitatoa fedha au vifaa. Baada ya uchambuzi wa jitihada za jamii na kuchagua aina ya usaidizi unaohitajika, matokeo ya uchambuzi huo yanapaswa kujumuishwa katika mipango na bajeti za Halmashauri. Iwapo Halmashauri zitashindwa kutoa aina ya usaidizi unaostahili kutokana na ufinyu wa bajeti, mamlaka hizo zinaweza kushirikiana na taasisi nyingine au wadau wenye uwezo wa kutoa usaidizi huu.