Kufuatia kutolewa na kujadiliwa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuhusu Independent Power Tanzania Limited (IPTL) Akaunti ya Tegeta ya Escrow (TEA) bungeni na kilio cha umma kilichofuatia kuhusu kufichuliwa kwa ufisadi ambao haujawahi kuwapo wa aina hiyo, Sisi, Asasi za Kiraia (AZAKI) tajwa hapo chini , tunapenda kuwasilisha msimamo wetu wa pamoja kuhusu utata wa suala hili.
Tumefanya mapitio ya taarifa ya Ofisi yaTaifa ya Ukaguzi (NAO) kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), pia taarifa ya PAC ya tarehe 26 Novemba 2014 Bungeni, pamoja na machapisho mengine mengi kuhusiana na suala hili, na TUMEBAINI yafuatayo kuhusu mapungufu ya taasisi zetu katika kuendesha shughuli zao kwa uwazi na uwajibikaji:
1. Ya kwamba jinsi Pan Africa Power Solutions Tanzania (PAP) ilivyochukua hisa za Mechmar ambazo ni asilimia 70 ya hisa za IPTL kwa uwizi wa ujanja na uhawilishaji wa fedha za TEA zisizopungua Dola za Kimarekani milioni 120 kwa IPTL/PAP uliofanywa ulikuwa kinyume cha sheria na ulihusisha njama baina ya maafisa wa serikali wa ngazi ya juu, Wakurugenzi wa Bodi ya Tanesco, Shirika la Uandikishaji na Utoaji Leseni za Biashara (BRELA) na Benki binafsi.
2.Ya kwamba utoaji wa fedha toka TEA mwaka 2013 ulikuwa ndiyo kilele cha miongo miwili ya utekwaji wa sera ya nishati kwa faida binafsi na rushwa iliyohusisha IPTL, Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini (MEM).
3. Ya kwamba mchakato wa usuluhishi kupitia Kituo cha Kimataifa cha Uamuzi wa Migogoro ya Kiuwekezaji (International Centre for the Settlement of Investment Disputes (ICSID) ulioanzishwa na TANESCO mwaka 2008 ili kupata suluhisho juu ya malipo yanayosemekana kupitiliza tozo la uwezo (capacity charges) kwa kipindi chote cha mkataba (mwaka 2002 hadi leo) ulihujumiwa na PAP pamoja na wamiliki wadogo wa zamani wa hisa za IPTL , VIP Engineering and Marketing (VIP) kwa kutumia kijanja mfumo wa kisheria wa Tanzania, na kuacha suala la gharama za umeme wa IPTL bila utatuzi.
4. Dhana ya kwamba “TEA siyo fedha za umma” ni hoja inayotolewa na watetezi wa IPTL/PAP/VIP ili kukanganya mjadala mweledi wa masuala ya msingi yaliyopo.
TUNAWAPONGEZA CAG na PAC kwa wajibu wao muhimu wa kufuatilia na kuwawajibisha maofisa wa serikali kwa vitendo na maamuzi yao kuhusu IPTL/TEA kujipatia fedha isivyo halali kwa kukagua taarifa husika za mahesabu ya fedha na kutaka maelezo na uhalali kutoka kwa wahusika. Katika mfumo wa kidemokrasia, hata hivyo, hii haitoshi. Wakati maelezo na uhalali kutoka kwa wenye wajibu huo yanapoonekana hayaridhishi, bunge linawajibu wa kuhakikisha hatua za marekebisho zinachukuliwa kwa kutumia uwezo wake wa kisheria na kikatiba .
TUNASIKITISHWA na jinsi ambavyo fedha za TEA zilihawilishwa (hamishwa) kirahisi kutoka Benki kuu ya Tanzania (BOT) kwenda benki binafsi, na hatimaye kwenda kwenye akaunti za watu binafsi. Vitendo hivi vinadhihirisha ukosefu wa uangalifu unaotakiwa kwa upande wa wahusika. Tunamashaka na mambo mengine yafuatayo yanayohusiana na hili:
· BRELA:Taarifa ya CAG inaonyesha wazi kuwa kulikuwa na nyakati ambapo ukosefu wa uangalifu unaotakiwa ulijitokeza katika michakato ya Mamlaka ya Uandikaji na Utoaji Leseni za Biashara (BRELA) kuhusu uhawilishaji wa kinachofikiriwa kuwa ni fedha zinazomilikiwa na Mechma ambazo ni 70 % za hisa za IPTL. Wamiliki wa chombo kisichofahamika cha Piper Link, PAP na mmliki hisa wake asiyefahamika, Simba Trust, wote wakiwa washiriki katika hujuma hii, walitakiwa wawe wamegundulika katika uchunguzi wa awali au kusita kufanya waliyoyafanya wangejua kuwa majina yao yanaweza wekwa wazi hadharani.
· Uangalifu unaotakiwa na mabenki na mashaka kuhusu utakatishaji fedha: Chini yaSheria ya Uzuiaji wa Utakatishaji Fedha (Anti-Money Laundering Act) ya mwaka 2006, benki zote na taasisi zote za fedha lazima zichukue hatua za uangalifu unaotakiwa za kuwatambua watu walio na nafasi kubwa kisiasa na kubaini vyanzo vya fedha zao na kuwafuatilia. Ukweli wa kwamba viongozi wa ngazi za juu kisiasa, baadhi yao wakiwa wamehusika dhahiri katika kashfa za rushwa katika kipindi kilichopita, walifungua akaunti katika Benki ya Mkombozi na kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kunaonyesha kwamba taratibu za kawaida za kuwafuatilia wateja ikijumuisha hatari ya utakatishaji fedha hazikuzingatiwa.
Muamala wa dola milioni 65 za Marekani kutoka Benki ya Mkombozi kwenda benki ya huko Uholanzi kunaonyesha ukiukaji wa taratibu za kawaida za “kumjua mteja wako”. Benki ya Stanbic kwa upande wake inatuhumika kwa kula njama katika ulipaji wa kiasi kikubwa cha fedha taslimu kwa wanufaika wa PAP/IPTL katka muda wa siku moja. Ukweli wa kwamba PAC haikuweza kuhakiki majina ya wengine ambao akaunti zao za benki zimeingiziwa kiasi kikubwa cha fedha kinacholeta mashaka na ya kwamba Kitengo cha Kiintelijensia cha Fedha (FIU) hakikujulishwa kuhusu miamala hiyo, pia kunaonyesha ukiukaji wa kanuni na taratibu za kibenki. Ingawaje Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua za kujisafisha dhidi ya changamoto za kisheria zinazoweza kujitokeza kuhusiana na TEA, ilishindwa kuchukua uangalifu wake binafsi juu ya kesi hii ikitegemea dhamana ya wahusika wakuu.
· Uwazi wa mikataba: Msukumo uliopo hivi sasa wa kufanya mikataba ya sekta zote za nishati kuwa wazi ni lazima ijumuishe mikataba kati ya serikali na wazalishaji binafsi wa nishati ikiwa ubia baina ya Serikali Na Wazalishaji Binafsi (PPP) hautafedheheshwa. Hivi sasa kuna ongezeko la sababu siyo tu za kuweka wazi mikataba bali ushiriki kamilifu wa bunge katika mchakato wa mikataba , kuanzia utoaji wa zabuni, utendaji na ukamilishaji pale panapokuwa na mikataba ya pamoja ya aina hii (joint venture agreements). Ushiriki kamili wa umma na bunge katika kuchunguza na kujadili mikataba ya PPP na utekelezaji wa mikataba hiyo kungelifanya hali iwe ngumu kwa PAP na VIP kutumia mwanya wa udhaifu wa kimfumo ndani ya BRELA, Tanesco na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujinufaisha.
· Utamaduni wa kuepuka adhabu: Ikiwa wale waliohusika katika kashfa hii hawatawajibishwa kwa kutumia mamlaka yao vibaya na kwa uwizi wa fedha za umma, itakuwa ni mwendelezo wa udhaifu wetu wa kimfumo kuhusiana na kuwafungulia mashitaka viongozi walioonekana kuhusika na vitendo vya rushwa, baadhi yao wakiwa wamerudia makosa hayo hayo. Umma unazidi kuumizwa na vitendo hivi vya rushwa ya viwango vikubwa, na jinsi ambavyo watuhumiwa wa rushwa wanavyojitetea pia na kile kinachojitokeza kama uwezo wao wa kuepuka adhabu.
Kuna hatari kwamba mwendelezo wa kuepuka adhabu kutawasilisha jumbe zisizo sahihi kwamba: 1) Hakuna hatari kutumia kiwango kikubwa cha fedha za umma kwa ubadhirifu, na 2) dola haina mamlaka ya kuwashughulikia watenda maovu.
Kwa mwanga wa hayo hapo juu, TUNATOA WITO kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika katika uporaji wa TEA kwa matumizi mabaya ya mamlaka na uwizi wa fedha za umma. Hasa, tunataka Serikali iagize mara moja na kwa uwazi urejeshaji wa fedha zote za escrow zilizolipwa kwa ulaghai kwa PAP, pamoja na faida na itekeleze mapendekezo ya Bunge na kutatua suala hili la IPTL kwa manufaa ya umma. Hatua hizo ni:
1. TAKUKURU, polisi na vyombo vingine vya usalama wachukue hatua dhidi ya wale wote waliotajwa na PAC kwenye taarifa yake na wengine watakaobainika kuhusika baada ya uchunguzi zaidi;
2. Wenyeviti na wajumbe wa Kamati za Bunge waliohusishwa katika sakata hilo waadhibiwe;
3. Benki ya Stanbic, Benki ya Mkombozi na taasisi nyingine za fedha zichunguzwe kwa kushindwa kuwa na uangalifu unaotakiwa na kwa utakatishaji fedha;
4. Mapitio ya Sheria ya TAKUKURU (PCCB Act) yafanyike ili kukabiliana na viwango vikubwa vya rushwa na uhujumu wa uchumi;
5. Serikali iangalie uwezekano wa kuumiliki mtambo wa IPTL;
6. Serikali ifanye mapitio ya mikataba yote ya uzalishaji wa umeme.
Kashfa hii ya IPTL inaleta hali ya wasiwasi kuhusu uadilifu wa Serikali ya Tanzania ambayo inaweza kutatuliwa tu kwa uongozi imara wenye maamuzi thabiti ili kumaliza kwa mara ya mwisho kashfa hii iliyodumu kwa muda mrefu.
Imetiwa sahihi na:
1. Policy Forum
2. Tanzania Coalition on Debt and Development
3. ACTIVISTA
4. Tanzania Youth Vision Association
5. SIKIKA
6. Action Aid Tanzania
7. HakiElimu
8. Youth Partnership Countrywide