Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Ile dhamira ya Policy Forum kushirikiana na Ofisi ya Bunge mwaka huu wa 2008 imeanza kutekelezwa kwa mfululizo wa vikao vya pamoja na wabunge, maafisa wa ofisi ya bunge na wana-ASASI.

Ikiwa moja ya njia ya kutimiza malengo yake ya kupata ushirikishi bora kakita michakato ya kitaifa ya sera, Policy Forum imeamua kuongeza mahusiano zaidi na wabunge. Harakati hizi ni katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana mwaka jana ambapo mtandao huu uliandaa semina kuhusu mchakato wa Bajeti na ilihudhuriwa kwa wingi na wabunge, wanahabari na asasi za kiraia. Wahudhuriaji walipata uelewa zaidi kuhusu jinsi mchakato wa bajeti Tanzania unavyotekelezwa.

Kwa mwaka 2008, PF imepanga kuandaa vikao saba kama hivi ikishirikiana na IDASA na Revenue Watch Institute. Kwa mwezi Mei, kulikuwa na kikao tarehe 12-16 ambapo maafisa wa Ofisi ya Bunge walialikwa kikifuatiwa na kingine na wabunge tarehe 19-20 Mei. Vikao hivi viwili viliongelea mapato yanayotokana na sekta ya madini. Kikao cha Mei 27-28 kilikutana kujadili

jinsi upangaji wa bajeti unavyosaidia au kuathiri malengo ya MKUKUTA (Mkakati wa Kukuza uchumi na Kupunguza Umaskini). Vikao kama hivi huwa vinaalika wazungumzaji ambao hutoa mada kuhusu mchakato wa bajeti; mitazamo ya ASASI za kiraia; uhusiano kati ya upangaji bajeti na UKIMWI na masuala ya kijinsia; na kama ilivyokuwa katika kikao cha madini, jinsi ya kuboresha mapato yatokanayo na madini. Vikao vyote hivi vilihudhuriwa pia na wana-ASASI.

Kama ilivyoelezwa katika mwelekeo wake mpya, PF itajihusisha katika michakato ya sera kwa njia ya ufanisi ambayo itaweza kuleta mabadiliko na ushawishi zaidi. Njia mojawapo ni kwa kuchagua kwa uangalifu maoneo ya kujihusisha nayo. Ushirikiano huu na Ofisi ya Bunge ni eneo ambalo PF inaweza kuleta mabadiliko na ushawishi katika michakato ya sera.