Sekta ya madini nchini Tanzania imepitia mageuzi makubwa ya kisheria na kisera tangu mwanzoni mwa mwaka 2000. Mabadiliko haya yalilenga zaidi kuhakikisha Tanzania kama nchi na hasa wananchi wake wanapata manufaa zaidi kutokana na maliasili waliyopewa na Mungu. Hata hivyo, manufaa hayo yanaweza kupatikana tu ikiwa utawala wa sekta ya madini kupitia ushiriki wa wananchi katika ukusanyaji na ugawaji wa mapato kutoka sekta hiyo utaboreshwa.
Nchini Tanzania, serikali ndio mmiliki halali wa madini yote (na maliasili nyingine) huku udhibiti wa maliasili hizo ukiwa chini ya Rais ambaye ndiye mdhamini pekee. Hii ina maana kwamba kuna wigo mdogo nchini wa kuruhusu kuweka sheria tofauti za kukusanya na kugawanya mapato ya madini kwa mamlaka za chini. Ili kuhakikisha mgawanyo sawa wa mapato ya madini kwa Watanzania wote, bajeti ya taifa hugawanya rasilimali zote za umma kwa kuzingatia vipaumbele vya serikali, ukubwa wa mapato yanayokusanywa na msongamano wa watu. Hivyo mamlaka za serikali za mitaa zina uwezo wa kuanzisha na kusimamia vyanzo mbalimbali vya mapato kama vile ushuru wa huduma na uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii (CSR) ili kuwezesha maendeleo ya jamii. Kutokana na usuli huu, muhtasari huu unalenga kutoa matokeo ya uchambuzi wa ushiriki wa wananchi katika ukusanyaji na ugawaji wa ushuru wa huduma ya madini kwa kutumia Geita na Mara kama kisa mafunzo