Skip to main content
Submitted by Web Master on 30 June 2015

Tarehe 25 Juni 2015, Policy Forum ilishiriki kwenye uzinduzi wa kampeni “Stop The Bleeding” inayolenga kupambana na utoroshwaji haramu wa rasilimali na fedha barani Afrika. Kampeni hii ambayo inaongozwa na asasi za kiraia za kiafrika kwa ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa, inaazimia kufanyia kazi matokeo ya utafiti na mapendekezo ya ripoti ya Thabo Mbeki ijulikanayo kama "the High Level Panel on Illicit Financial Flows from Africa" ambayo imechunguza tatizo la utoroshwaji wa fedha hizi. Kampeni hii pia inatarajia kuhamasisha ushirikiano baina ya asasi za kiafrika kupambana na tatizo hili katika ngazi ya kitaifa, ukanda na barani Afrika kwa ujumla.

Uzinduzi ulianza kwa mkutano wa asasi za kiafrika tarehe 24 Juni 2015 kwenye hoteli ya Sarova Panafric, Nairobi ambapo mada mbalimbali kuhusiana na tatizo linavyoathiri nchi za kiafrika ziliwasilishwa. Washiriki walielezwa juu ya  athari za utoroshwaji fedha kwa maendeleo, walitathmini kazi zao za uchechemuzi kwenye eneo hili hadi kipindi hiki, changamoto zake, na uzoefu wao katika kushirikisha makundi mbali mbali kama vile ya wanawake na vyama vya wafanyakazi. Asasi za kiraia jijini Nairobi walikubaliana kudai yafuatayo:

Kwa Jumuiya ya kimataifa:

- Jumuiya ya kimataifa isaidie nchi za barani Afrika kudai fedha zote zilizotoroshwa zirudishwe kama ilivyopendekezwa na Ripoti ya Thabo Mbeki.

- Jumuiya ya kimataifa iunge mkono jitihada za kuanzishwa kwa chombo cha kimataifa cha kodi ili kukabiliana na ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa. Chombo hiki kiwe chini ya Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Afrika na Taasisi zingine Afrika

- Serikali za Afrika, kupitia Umoja wa Afrika, zisukume uanzishwaji wa chombo cha kimataifa cha kodi ambacho kitapewa jukumu la kuweka sheria maalum za kukabiliana na ukwepaji kodi.

- Serikali za Afrika, kupitia Umoja wa Afrika na taasisi zake, zihamasishe ukuzwaji wa minyororo ya thamani barani Afrika ili kunufaika na mfumo wa sasa wa biashara na kodi duniani.

Ukanda

- Jumuiya za kiuchumi barani Afrika kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki waanzishe mifumo ya kupunguza ushindani wa kupata wawekezaji unaochangia nchi zetu kupata mapato madogo (Mbio za Kuelekea Chini).

Kitaifa

- Serikali za Afrika zitekeleze mapendekezo ya ripoti ya AU/UNECA "High Level Panel Report on IFFs"

- Serikali za Afrika zirekebishe mifumo yake ya kodi ili kupunguza kukosekana kwa usawa  na kuongeza fedha zitakazotumika kwenye kufadhili mipango ya maendeleo ya kitaifa.

- Serikali za Afrika zipunguze misamaha/motisha ya kodi.

- Serikali za Afrika zipitie upya makubaliano ya kodi na mataifa tajiri kuhakikisha wanapata mapato stahiki.

- Serikali za Afrika zitathmini mzigo wa kodi kwa wanawake na wanaume maskini ili kuhakikisha sera za fedha zinakuwa na mtazamo wa kijinsia.

- Serikali za Afrika zijengee uwezo wa ndani ili kukuza miundombinu wezeshi ya uzalishaji na biashara.

Uzinduzi wa tarehe 25 Juni ulihusisha mikutano na waandishi wa habari, risala mbalimbali zilizotolewa Uhuru Park, Nairobi na burudani ya muziki ikifuatiwa na maandamano. Uzinduzi huu uliandaliwa na kikundi kazi cha muda cha African IFF Campaign Platform kinachojumuisha mashiirika 6 yaani y Tax Justice Network-Africa (TJN-A), Third World Network-Africa (TWN-Af), Africa Forum and Network on Debt and Development (AFRODAD)African Women’s Development and Communication Network (FEMNET), the African Regional Organisation of the International Trade Union Confederation (ITUC-Africa), Trust Africa  na Global Alliance for Tax Justice (GATJ).

Kufuatia uzinduzi huu, kutakuwa na mkutano wa pembeni kwenye kongamano la 3rd Financing for Development Conference (FfD3)  Julai 2015 mjini Addis Ababa, Ethiopia ambao utatambulisha rasmi kampeni ya "Africa IFF campaign", utasisitiza umuhimu wa kutekeleza mapendekezo ya Ripoti ya Mbeki na kugusia mipango ya pamoja ya asasi za kiafrika ili kuhamasisha utekelezwaji wa Ripoti ya Mbeki. Mkutano huu utawalenga washiriki kutoka serikali za kiafrika, asasi za kiafrika, na taasisi zitakazowakilishwa kwenye kongamano la FfD3.