Sisi, Asasi za kiraia awali ya yote tunapenda kwanza kuipongeza serikali yetu ya Tanzania kwa kufikia hatua ya kutengeneza rasimu ya sera ya Gesi Asilia iliyotolewa hivi karibuni. Hii imedhihirishwa kwetu kuwa serikali yetu inadhamira ya dhati katika kuhakikisha kuwa rasilimali ya Gesi inawanufaisha watanzania wote na kuchangia maendeleo katika nchi yetu.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizi, sisi Asasi za kiraia baada ya kufanya uchambuzi wa awali wa rasimu iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia akaunti yake ya twitter, Jumatatu ya Mei 20, 2013 tumebaini mapungufu katika maeneo yafuatayo:
- Kutokuwepo kwa masuala kuhusu utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi na mafuta
- Kutokuwepo kwa masuala ya jinsia, mfuko wa kuhifadhi mazingira, fidia ya ardhi kupisha miradi nchi kavu, ushiriki wa sekta binafsi na masuala ya uwazi
- Masuala ya kuimarisha uwajibikaji hayajawekwa wazi
- Utata kuhusu raundi ya nne ya utoaji wa leseni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia
- Kutokuwepo kwa maelezo ya wazi kuhusu ushiriki wa serikali
- Sera haipo katika uhalisia – haioneshi ni jinsi gani mikataba/makubaliano yaliyopo hivi sasa kuhusu usafirishaji nje wa gesi asilia iliyosindikwa (Liquified Natural Gas – LNG) itahusishwa kwenye sera mpya au muda unaohitajika ili kuanzisha miradi ya uchakataji wa LNG.
Suala la Utafutaji
Kuhusu suala la utafutaji, tumebaini kuwa Sera haijataja chochote kuhusiana na utaratibu wa utoaji wa haki za kutafuta gesi asilia, kanuni ambazo zitasimamia masuala ya mikataba ya uzalishaji na ugawanyaji wa mapato na mfumo wa mitakaba inayopaswa kutumika, jinsi serikali/taifa litakavyoshiriki au kuwepo kwa utaratibu wa udhibiti katika suala la utafutaji gesi asilia. Kwa mfano ukurasa wa 7 wa rasimu unasema“Sera hii inahusisha tu suala la uchuuzi wa gesi. Wakati masuala kuhusu utafutaji yanaongozwa na sera nyingine, sera hii inatambua umuhimu wa kuungansiaha masuala yote yanayohusu mchakato wa gesi asilia.”
Pia tumebaini kuwa sera haijataja chochote kuhusiana na utaratibu wa utaoaji wa haki za kutafuta gesi asilia, kanuni ambazo zitasimamia masuala ya mikataba ya uzalishaji na ugawanyaji wa mapato na mfumo wa mitakaba inaopaswa kutumika, jinsi serikali/taifa litakavyoshiriki au kuwepo kwa utaratibu wa udhibiti katika suala la utafutaji gesi asilia.
Sera pia haisemi haswa ni lini hiyo sera nyingine kuhusiana na masuala ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia itakuwa tayari.
Masuala ya utafutaji yaliingizwa kwenye rasimu ya sera ya kwanza, ikihusisha jinsi serikali itakavyoshiriki katika uendelezaji wa sekta, masuala ya ushindani katika kandarasi na uwekezaji, kwa kutaja masuala machache tu. Lakini masuala hayo yote yameondolewa kwenye rasimu ya sasa. Tunaomba masuala haya yarudishwe.
Iwapo masuala ya utafutaji wa gesi asilia hayatakiwi kuwemo kwenye sera hii, basi inafaa kuwe na dokezo la lini hasa hiyo sera nyingine itakuwa tayari kutumika, ikihusisha na mchakato wa upatikanaji wa sera hiyo.
Kutokuwepo kwa masuala ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika rasimu ya sera hii kunaleta mkanganyiko kuhusiana na utaratibu wa utoaji wa leseni kwa ajili ya raundi ya nne ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo ya Bahari Kuu na Ziwa Tanganyika.
Tumefahamishwa kuwa wakati zabuni kwa ajili ya kuomba utafutaji wa mafuta na gesi asilia zitakapokuwa zinafunguliwa mnamo Oktoba 25, sera hii itakuwa tayari. Lakini tuna wasi wasi iwapo hili litawezekana kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa imechukua miaka kadhaa kuandaa sera ya Gesi Asilia, je, tuna uhakika gani iwapo sera ya kuongoza masuala ya utafutaji itaandaliwa na kuwa tayari ndani ya kipindi kifupi ifikapo Oktoba 25 kama inavyoahidiwa?
Masuala muhimu yameachwa
Katika uchambuzi wetu tumebaini kuwa masuala muhimu yameachwa, na yale yaliyowekwa yameingizwa kwa namna ambayo yanashusha umuhimu wake. Kwa mfano, masuala kuhusu jinsia na taasisi za kijamii hayamo kabisa kwenye sera inayopendekezwa. Pia masuala kuhusiana na ushiriki wa sekta binafsi katika mchakato wa gesi asilia nayo hayamo. Pia, sera haitaji kwa uzito unaostahili matakwa ya uwazi katika Mkakati wa Uwazi wa tasnia ya Uziduaji (EITI).
Masuala ya jinsia ambayo sisi kama Asasi tunaamini kuwa yanapaswa kuwa sehemu ya masuala muhimu ya kuingizwa kwenye sera hii inayopendekezwa. Serikali hivi sasa imekuwa na ahadi ya kuhakikisha kuwa masuala ya jinsia yanapewa kipaumbele katika sekta nyingi, kwa mfano katika sekta ya Ardhi, sheria na Kilimo. Hivyo basi litakuwa jambo la busara sera hii iendane na ahadi hizi za serikali.
Suala la kulinda mazingira na ugharamiaji wa kurudisha mazingira katika hali ya kawaida endapo yataharibiwa halijapewa uzito stahiki licha ya sera kukiri kuwa suala la kuhakikisha mazingira hayaharibiki ni changamoto. Ni ushauri wetu kuwa sera iweke wazi kuwa best practices and technology pekee ndio itatumika na kuwataka wawekezaji kutoa fedha itakayoingia kwenye mfuko wa mazingira ulioanzishwa na sera/sheria ya madini ya 2009 na 2010. Sera iweke wazi mamlaka zitakazo simamia masuala ya mazingira kwani uzoefu katika madini unaonyesha taasisi zaidi ya moja husika - TMAA na NEMC
Pia, ni muhimu sera ikahakikisha kuwa masuala hasi na chanya yatakayotokana na shughuli za utafutaji na biashara ya gesi asilia yanafafanuliwa ipasavyo na yanaenelezwa kwa mtazamo wa jinsia.
Masuala muhimu hapa ni pamoja na: Haki kuhusu ardhi – masuala kuhusu ulipaji wa fidia na utoaji wa ardhi kwa wawekezaji pamoja na kuhakikisha kuwa masuala yanayowahusu wajasiriamali wanawake na jinsi watakavyopewa kipaumbele katika mipango hii.
Vurugu zilizotokea hivi karibuni huko Mtwara ni kielelezo kuwa kuna umuhimu mkubwa wa taasisi za kijamii kushirikishwa ipasavyo ili kuziba ufa uliopo kati ya jamii na serikali. Taasisi hizi zinaweza kuifanya kwa ufanisi kazi ya kutoa elimu na kuwaelewesha wananchi na viongozi wao kuhusiana na sekta hii inayoibuka kwa kasi hapa nchini. Elimu hii itawapa fursa wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato unaohusu rasilimali hii muhimu kwa uchumi wao na wa nchi.
Pamoja na mambo mengine, elimu hii itawawezesha wananchi pia kushiriki katika kupanga mipango na pia kudhibiti mchakato.
Ushiriki wa sekta binafsi
Kuhusu sekta binafsi, ni muhimu kuainisha kwa kina umuhimu wa sekta binafsi na jinsi gani itashiriki au kushirikishwa katika mchakato mzima. Umuhimu wa sekta binafsi nchini umetajwa katika aya moja tu katika sera yote. Ingawa maneno ‘sekta binafsi’ yanaonekana katika maeneo mbalimbali ya sera hii, ni muhimu kuainisha kwa kina umuhimu wa sekta binafsi na jinsi gani itashiriki au kushirikishwa katika mchakato mzima.
Masuala ambayo sekta binafsi inaweza kushiriki au kushirikishwa ni pamoja na kuainisha taasisi za nyumbani zinazoweza kufanya kazi pamoja na makampuni ya kimataifa; misamaha ya kodi; kutenga zabuni fulani fulani kwa kampuni za ndani pekee; masuala hukusu udhibiti; ushauri na uwezeshwaji kifedha na kiutendaji kwa makampuni ya ndani yatakayotaka kujiingiza kwenye biashara hii na kadhalika.
Ahadi za serikali kuhusu EITI, ambazo zitapewa mkazo baada ya mkutano wa Sydney, nazo hazitajwi sana. Ilitarajiwa kuwa sera hii ingekuwa moja ya nafasi za kuhakikisha kuwa serikali inatoa maelezo ya jinsi inavyopanga kutimiza masharti kama hayo.
Kukosekana kwa maelezo kuhusu Uwajibikaji na Uwazi
Ahadi zinazotolewa na serikali kupitia sera kuhusiana na utekelezaji wa masharti ya EITI ni dhaifu sana. Sehemu kuhusu Uwazi na Uwajibikaji ilipaswa ielezewe kwa kauli thabiti ili kuonesha uzito na umuhimu wa suala hilo. Ilitarajiwa kuwa sehemu hii pia ingehusisha masharti mapya yaliyokubaliwa wakati wa mkutano wa Sydney uliofanyika hivi karibuni.
Kubwa zaidi, sera inapendekeza mabadiliko kadhaa ya taasisi zinazohusika na usimamizi na udhibiti. Lakini haiwekwi wazi iwapo Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa za Maji na Nishati (EWURA) itaimarishwa na kuwezeshwa kusimamia shughuli za utafutaji wa gesi au iwapo itaanzishwa mamlaka nyingine kwa ajili ya kazi hiyo.
Kutokana na hilo, wajibu wa wachakataji wa gesi, wataohusika na masuala ya kusafirisha kwa kutumia mabomba, vifaa vya uchakataji, na upangaji wa bei – ni muhimu pia kwani masuala hayo yatahusisha uwekezaji mkubwa na hivyo litahitaji mdhibiti ambaye naye atakuwa na nguvu ya kiteknolojia kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi na mwenye uwezo wa kuhakikisha sekta inasimamiwa ipasavyo.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), ambalo mpaka sasa ndilo linaonekana kama mdhibiti katika sekta hii, tayari linakabiliwa na changamoto za kiuwezo kudhibiti sekta hiyo. Imedhihirika kuwa TPDC haina uwezo wa kutosha kusimamia mikataba ya uzalishaji pamoja na kudhibiti utendaji wa kampuni zinazohusika na kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi. Kuiwezesha EWURA au kuanzisha taasisi nyingine ili kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa ni changamoto kubwa sana katika mazingira tuliyomo lakini ni suala muhimu la kupewa kipaumbele.
Sera ingeonesha umuhimu kwa kuelezea jinsi ambavyo suala hilo litakavyoshughulikiwa kwa kuonesha jinsi uwezo wa kufanya kazi hiyo utakavyotafutwa na utatafutwa wapi?
Kutokuwepo kwa masuala ya utafutaji katika sera hii kunamaanisha kuwa masuala muhimu ya uwajibikaji bado hayajapatiwa ufumbuzi.
Kuna kazi ya kufanya marekebisho katika muundo wa TPDC na kazi zake ambayo inaendelea, lakini hilo linapaswa kufanywa kwa kuzingatia umuhimu wa kutenganisha majukumu ya mzalishaji na mdhibiti. Kama masuala haya yangekuwepo kwenye sera kungeongeza umuhimu wa nyaraka hii.
Mkanganyiko katika utoaji wa leseni mpya
Katika sera hii, suala la kuondolewa kwa masuala ya utafutaji kunaleta mashaka makubwa sana kuhusiana na mchakato unaoendelea wa kutoa leseni mpya kwa watafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu vipya. Kuna vitalu vipya saba katika Bahari Kuu na kimoja katika eneo la Ziwa Tanganyika. Zabuni za waombaji zitafunguliwa Oktoba 25, baada ya zoezi hilo kuahirishwa mara mbili tangu ilipotangazwa mara ya kwanza Aprili 2011.
Tangu kutolewa kwa tangazo la kwanza kukaribisha waombaji wa leseni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia mwaka 2011, yametokea mabadiliko makubwa sana. Kitalu kimoja (Kitalu namba 4/1B) katika eneo la Bahari Kuu ambacho kimeondolewa katika mchakato huo na kimechanganywa na kitalu namba 41/C. Vitalu hivi sasa vimepangwa katika zabuni ambayo bado haijapangiwa tarehe ya kutangazwa.
Hivi sasa vitalu hivi viwili “vimetengwa rasmi kwa ajili ya serikali ambapo TPDC itaruhusiwa kufanya shughuli maalum za utafutaji kwa kumtumia mbia atakayepatikana kwa njia ya ushindani[1]”.
Pia ifahamike kuwa zabuni hizi zilikuwa zitangazwe Aprili 2011 na mchakato umeahirishwa mara mbili. Mchakato ulipoahirishwa Septemba 2012, notisi ya kuahirishwa kwake ilisema kuwa taarifa kuhusu takwimu (Bid Round Data Package – ikihusisha takwimu za ki-seismic) zitakuwa tayari mwishoni mwa mwezi huo. Hii inamaanisha kuwa, zabuni za kuomba leseni kwa ajili ya raundi ya nne, zilikuwa wazi tangu wakati huo.
Tunasikitika kuona Serikali ile ile iliyoahirisha zabuni za vitalu ili kupisha utengenezwaji wa sera na sheria leo hii inatangaza zabuni kabla ya sera na sheria. Aidha katika hali ya kushangaza serikali iliahirisha zabuni kupisha upatikanaji wa kanuni na muongozo wa utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi ila katika utangulizi wa rasimu ya sera ya 2013 serikali inasema masuala haya yanashughulikiwa na sera ya nishati ya 2003. Tungependa serikali ieleze kama sera ya nishati inatosheleza kwanini iliahirisha zabuni?
Utata kuhusu ushiriki wa serikali
Suala jingine katika rasimu hii ya sera ambalo haliyatolewa maelezo ya kutosha na ya kina ni ushiriki wa serikali katika shughuli hizi. Sera haina budi isipokuwa kuhakikisha, kwa maneno ya dhati kabisa, ushiriki wa serikali. Lakini rasimu hii ya sera haielezei suala hilo kinagaubaga. Rasimu haielezi, mathalani, ni taasisi gani zitahusika, zitawezeshwa vipi kushiriki na kufanya kazi zao kwa ufanisi, jinsi gani ambavyo taasisi hizo hazitakwamisha ushiriki wa sekta binafsi na kadhalika.
Rasimu ya sera ina dhana ya majukumu na wajibu mkubwa wa serikali katika karibu kila hatua. Lakini, hakuna maelezo yanayoainisha ni taasisi zipi hasa zitahisika. Kwa mfano, sera inatamka kuwa serikali, pamoja na mambo mengie:
“kimkakati, kupitia makampuni ya kitaifa (kwa pitia PPP – ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi) itaendeleza na kuendesha miundombinu muhimu ya usambazaji wa uhakika wa gesi”
“itaanzisha mchakataji wa gesi ili kuhakikisha ufanisi na kuhakikisha usambazaji wa gesi asilia”
“itawekeza kimkakati, kupitia taasisi zake, katika mnyororo wa thamani wa GTL na LNG na miradi mingine ya gesi asilia”
“itaimarisha uwezo wa kampuni za kitaifa kushiriki kimkakati katika sekta ya gesi asilia”
Hapa, inaweza kuonekana kuwa inamaanisha kampuni zinamilikiwa na serikali. Lakini pia inaweza kuwa inamaanisha kampuni tanzu za kampuni ya mafuta ya taifa. Maneno ‘taasisi zake’ ni tata wakati maneno ya mwishoni yanayosema ‘kampuni za kitaifa’ yanaweza kumaanisha pia hata kampuni binafsi za Kitanzania au zinazomilikiwa na serikali. Hakuna uhakika wa tafsiri hizo zinamaanisha nini hasa.
Sera pia inataja “Kampuni ya Taifa ya Mafuta na Gesi (haitaji TPDC isipokuwa kwenye ufupisho) na pia inataja “Kampuni ya Gesi ya taifa ya matawi yake”, zinazotajwa kama wazalishaji na wasambazaji.
Hapa pia kuna utata mkubwa kuhusiana na nini kiinamaanishwa haswa, hasa ukizingatia kuwa majina haya yanatajwa bila mpangilio maalum ambao ungeweza kutoa mwanga wa nini kinamaanishwa iwapo ungefuatwa. Hii inafanya iwe vigumu kuelewa na kuutathmini mpango huu wa serikali.
Ukosefu huu wa maelezo yanayoeleweka unaleta mashaka na unaweza kuyatisha makampuni ya mafuta na kuyafanya yachelewe kufanya maamuzi ya kuja kuwekeza nchini.
Haina uhalisia
Sera haina uhalisia kwani haioanishi yanayotokea hivi sasa katika sekta ya gesi asilia na kilichoandikwa kwenye nyaraka;
Haipangi muda maalum kwa kila shughuli, haizungumzii jinsi ya kukabiliana na majanga (tukumbuke vurugu za Mtwara) na haizungumzii masuala mengine yanayofahamika kuhusiana na sekta hii.
Inafahamika kuwa asilimia 86 ya gesi itakayozalishwa itasafirishwa nje ya nchi baada ya kuchakatwa. Mkataba wa biashara ya gesi ulishasainiwa na kampuni ya Ophir ambao umerithiwa na kampuni ya BG miaka kadhaa iliyopita. Mkataba huo bado unafanya kazi na kauli za waziri zinaonyesha suala hili.
Hata hivyo, sera haielezi lolote kuhusiana na suala hilo. Inakuwa vigumu kuelewa iwapo hilo limetokea kutokana na mabadiliko makubwa ya msimamo wa serikali, kisera au ni muendelezo wa ile hali ya masuala muhimu kama haya kutogusia uhalisia wa hali iliyopo.
Muda wa kuendeleza viwanda vya kuchakata gesi unafahamika. Kampuni ya BG imeshasema kuwa itafikia uamuzi wa mwisho wa kuwekeza nchini au la katika kipindi cha miaka mitatu au minne ijayo. Iwapo itaamua kuwekeza, itachukua miaka mingine kadhaa kujenga viwanda vya kuchakata gesi asilia na kuzalisha LNG na pia kujenga miundombinu yake.
Inapaswa dhamira inayoonesha kupitia nyaraka muhimu kama hizi ioanishwe na hali halisi, ikiwamo muda wa kufanya shughuli fulani, ili kuwawezesha wadau kupanga mambo yao kwa uhakika. Pia hii inasaidia wapanga mipango wenyewe na wale watakaoathirika na miradi hiyo, zikiwamo jamii, sekta binafsi na kadhalika.
Hii itawezesha kupanga mipango yenye uhalisia na ambayo inatabirika kwa urahisi na kuwezesha masuala mengine kuendelea kwa ufanisi kama vile utoaji wa ardhi, upangaji wa miundombinu, utoaji wa mafunzo ya ufundi, kuandaa sera nyingine, kuimarisha uwezo wa wadau wa ndani na kadhalika.
Haya ni baadhi ya mambo ambayo yangeweza kuwaelimisha watu wa Mtwara na kupunguza wasiwasi wao.
04/6/2013
The Extractives Industry Working Group:
1. Agenda Participation 2000
2. Interfaith Standing Committee on Economic Justice and the Integrity of Creation
3. HakiMadini
4. Policy Forum
5. Oxfam
6. TACOSODE
7. Tanzania Natural Resource Forum (TNRF)
8. Oil, Natural Gas and Environment Alliance (ONGEA)
9. International Alliance on Natural Resources in Africa (IANRA) Tanzania chapter