TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba uandikwe upya.
Mtandao wa Jinsia Tanzania tumeupokea uamuzi wa Bunge wa kusogeza mbele muda wa kuujadili muswada wa sheria ya mapitio ya Katiba wa 2011 kwa masikitiko makubwa.Uamuzi wa Bunge unaoitaka serikali kuufanyia marekebisho muswada huo na kuutafsiri kwa Kiswahili ni wamsingi ingawa una mapungufu. Tulitarajia kwamba Bunge lingeishauri waziwazi serikali kuuondoa muswada huo Bungeni na kuanzisha mchakato shirikishi wa kutunga muswada mpya.
Kwa hiyo, tunaunga mkono msimamo wa wananchi wanaoitaka serikali kuandaa muswada mpya unaozingatia maoni ya makundi mbalimbali ya wananchi.
Tunapenda kusisistiza msimamo wetu kwamba wananchi hawapaswi kutungiwa sheria ya kuanzisha mchakato na mfumo wa kutunga katiba mpya na chombo chochote kabla hawajajadiliana na kukubaliana juu ya dira, tunu na maadili ya Taifa lao. Msingi wa madai yetu ni mapungufu makubwa yaliyomo kwenye muswada wa marejeo ya katiba wa 2011 uliowasilishwa na serikali Bungeni kwa hati ya dharura. Muswada huu ulitungwa na serikali kabla ya kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa na ndio maana ulikuwa na kasoro nyingi zisizokubalika na watu wengi waliopata wafursa ya kuusoma na kutoa maoni yao.
Tunasisitiza kwamba, mjadala wa kujenga muafaka wa kitaifa unapaswa kuutangulia mchakato wa kisheria wa kutunga katiba mpya. Mjadala wa Kitaifa ndio utakaoainisha: wigo wa uwakilishi wa makundi mbalimbali; sifa za wajumbe wa mkutano wa kitaifa wa katiba na kazi zake; sifa za wajumbe wa tume huru ya katiba na hadidu za rejea za tume hiyo; sifa za wajumbe wa Bunge la Katiba, muundo na kazi zake; na utaratibu wa kuandaa na kusimamia kura ya maoni.
Ili mjadala huo uwe na tija, wananchi wanahitaji muda wa kutosha wa kujadiliana na kukubaliana kwanza juu ya dira, misingi ya kisiasa na kiuchumi na maadili ya taifa lao. Vilevile serikali inahitaji muda wa kutosha wa kukusanya maoni ya wananchi na kuyachambua kabla ya kuandaa sheria ya kusimamia mchakato wa kutunga katiba mpya.
Kazi ya kuandaa na kuratibu mjadala wa kitaifa inapaswa kufanywa na chombo huru kinachoundwa na wataalamu wenye misimamo thabiti na sio vyombo au taasisi za dola. Tunaitaka Serikali kuheshimu maamuzi ya wananchi yatakayotolewa wakati wa mjadala huo. Tunasisitiza kwamba maamuzi ya wananchi ndiyo yatakayozaa sheria nzuri ya mchakato na mfumo wa kutunga katiba mpya.
Tunalitaka Bunge kutimiza wajibu wake wakikatiba kwa kuishauri Serikali juu ya namna bora ya kuandaa na kuratibu mjadala wa kitaifa ili wananchi wote waweze kushiriki kwa amani,utulivu na kuvumiliana. Bunge linapaswa pia kushirikiana na serikali katika kuweka mazingira muafaka ya kisiasa na kisheria ili mchakato wa kutunga katiba ukamilike kwa mujibu wa matarajio ya watanzania wote.
Tunawataka wanasiasa wote kutambua wajibu wao wa kutetea maslahi ya taifa na kuepuke kuweka mbele maslahi ya vyama vyao wanapowasilisha hoja zao ndani na nje ya Bunge. Ili kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia haki na wajibu wao wa kuunda katiba mpya, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa na wadau wote wa siasa nchini:
a) Kuafikiana juu ya mfumo wa kuratibu mjadala wa kitaifa utakaoweka misingi ya kisiasa na kisheria ya kutunga katiba mpya.
b) Kuafikiana juu ya sheria ya kuunda Bunge la katiba na sheria ya kuandaa na kusimamia kura ya maoni. Sheria hizi zitatungwa na Bunge kwa kuzingatia mapendekezo ya wananchi yatakayotokana na mjadala ya kitaifa ulioratibiwa na tume huru ya katiba.
c) Kushirikiana kuweka mazingira muafaka ya kisiasa yatakayowezesha wananchi wote kushiriki katika mchakato wa kutunga katiba mpya bila hofu au kuburuzwa na kundi la watu au taasisi yoyote.
d) Bunge kutotunga sheria yoyote yenye lengo au mwelekeo wa kuchakachua mchakato wa kutunga katiba mpya katika kipindi chote cha mchakato wa kutunga katiba mpya.
e) Kuafikiana juu ya muda wa mchakato wa kutunga katiba.
f) Kuafikiana juu ya namna ya kutoa elimu kwa wananchi wote ili waweze kushiriki ipasavyo katika mchakato wa kutunga katiba.
MJADALA KWANZA, SHERIA BAADAYE!
Imetolewa Dar es salaam na
Mary Rusimbi
Mwenyekiti wa Bodi TGNP