Elimu Ya Mpiga Kura Kwa Wananchi ili Kuongeza Ushiriki Wa Vijana Na Wanawake
Na Jansi Sinkamba
Tushiriki ni mwanachama wa Policy Forum (PF) na ni asasi inayojikita katika kuleta maendeleo ya jamii masikini nchini Tanzania. Kazi zinazofanywa na Tushiriki zimejikita katika masuala ya utawala bora, jinsia, sera ya elimu, kilimo, PET, SAM, uharibifu wa mazingira, afya, lishe, usafi, haki za binadamu, na maji safi.
Tangu mwaka 2015, Tushiriki imekuwa kitoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi na kuongeza ushiriki wa vijana pamoja na wanawake katika masuala ya utawala bora. Kwa mwaka 2015 Tushiriki ilitekeleza mradii wa kutoa elimu kwa wananchi katika kata mbili kata ya Igoma na kata ya Tembela Mbeya Vijijini malengo yakiwa ni kutoa elimu ya mpiga kura pamoja na utawala bora.
Mategemeo ya mradi huo ilikuwa ni kuongeza ushiriki wa wananchi kwenda kupiga kura ili kupata viongozi bora wenye kuleta maendeleo katika maeneo yao, ngazi ya kata pamoja na Serikali ya Mtaa na Vitongoji. Pia, ilitegemewa kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kuingia kwenye mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya Kata, Mtaa na Vitongoji.
Katika Mradi huo kazi kubwa zilizofanywa ilikuwa ni kuhamasisha vijana na wanawake kuingia kwenye michakato ya kuomba nafasi za uongozi kwa nafasi mbalimbali, kuhamasisha jamii kushiriki na kuhudhuria mikutano mbalimbali ya wagombea na kampeni ili kupima hoja zenye uhitaji wa wananchi, kutoa elimu ya namna ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kutambua usiri wa kupiga kura, kutoa vipeperushi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujua majukumu ya viongozi na kuhamasisha vijana kushiriki mijadala ya redio katika kutoa elimu ya uchaguzi.
Imeandaliwa na kuandikwa na Jansi Sinkamba, Mkurugenzi Mtendaji wa Tushiriki