Skip to main content
Submitted by Web Master on 14 October 2020

Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017-2020/21), pamoja na malengo mengine, unakusudia kuweka mazingira wezeshi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujiajiri na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kama vile uvuvi, kilimo, ufugaji na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Serikali ya kutimiza lengo la kusaidia makundi hayo ni utoaji wa mikopo isiyo na riba.

Mwaka 2018, Serikali ilirekebisha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa (Sura 290) ambapo Halmashauri zote nchini zilitakiwa kutenga fedha kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Marekebisho hayo ya sheria yalifuatiwa na utungaji wa kanuni zinazoainisha masharti, vigezo vya utoaji na usimamizi wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi hivyo.

Katika kikao kilichofanyika Oktoba 13, 2020 kati ya Uongozi wa Idara ya Serikali za Mitaa (Tamisemi), Policy Forum na UNA Tanzania, ilibainishwa kwamba kuna changamoto kadhaa zinazokabili mfumo na utaratibu wa utoaji na usimamiaji wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini.

Akielezea kuhusu changamoto hizo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa, Angelista Kihaga, alieleza kuwa licha ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 90 kutolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, bado kuna  tatizo la usimamizi. Alieleza kuwa wasimamizi wengi hawana ujuzi wa kutosha wa kusimamia vikundi ili viweze kutekeleza shughuli zake za maendeleo ziwe endelevu na pia ziweze kuzalisha fedha ambazo zitarejeshwa katika Halmashauri husika. Alisisitiza kuwa kuna haja ya kuwajengea uwezo wasimamizi hao ili kuleta tija za mikopo wanayopatiwa wanavikundi.

Ukosefu wa fedha na ujuzi wa kufanya ufuatiliaji kwa vikundi vilivyopata mikopo ilielezwa kama moja ya changamoto zinazokabili Halmashauri nchini. Changamoto hii inaenda sambamba na ukosefu wa vitendea kazi vya kitaalamu hasa ngamizi (computer) kwa ajili ya kuweka kumbumbuku ya utoaji na ulipwaji wa mikopo iliyotolewa. Kiaga alitanabaisha kuwa pia, kunahitajika ushirikiano wa pamoja na AZAKI ili kuweza kutoa mafunzo kwa vikundi vidogovidogo jinsi ya kufanya shughuli za kijasiriamali ili vikundi hivyo viwe na mafanikio katika miradi yao na pia viweze kurejesha mikopo inayotolewa kwa wakati na kwa ufanisi.

Akizungumzia kuhusu namna ya kutatua changamoto zilizopo katika kusimamia shughuli na mfumo wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo, Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa Dk. Charles Mhina alisema kuwa kunahitajika marekebisho katika miongozo iliyopo ili kupata mwongozo bora ambao utawezesha  zoezi la utoaji na urudishaji wa mikopo kuwa rahisi na lenye tija kwa vikundi na Serikali.

Dk Mhina alisisitiza kwamba Serikali imeandaa rasimu ya kurekebisha kanuni zilizopo zinazoratibu utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Alisema kuwa “ili tuweze kuwa na mwongozo bora lazima tuwe na kanuni ambazo zipo imara”

Mojawapo ya maazimio ya kikao hicho ni kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kitajumuisha wataalamu kutoka Tamisemi, Policy Forum na UNA Tanzania, ambao watakaa pamoja ndani ya siku thelathini (30) na kuandaa mwongozo ambao utajumuisha mawazo ya wadau wengine. Mwongozo huo utakapokamilika, utasambazwa katika ngazi husika ili kurahisisha na kuweka ufanisi zaidi katika mfumo wa utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini.