Skip to main content
Submitted by Web Master on 5 December 2018

Kufuatia kupitishwa kwa sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2018,  Sisi wadau kutoka Asasi za Kiraia na watafutaji, watumiaji na wasambazaji wa taarifa za takwimu tumekutana kufanya uchambuzi wa kina wa sheria hii;

Pamoja na kutambua umuhimu wa sheria hii ambayo imelenga kuzuia usambazaji/ uchapishaji wa taarifa za kitakwimu zinazoweza kupotosha umma;

Sisi Wanachama wa Policy Forum, kushirikiana na Twaweza na TAMWA, tumegundua kwamba Sheria hii ina mapungufu yanayoweza kuathiri kazi za utafiti zinazofanywa na wadau na watafiti ambazo huchangia maendeleo ya Taifa;

Kwa kuzingatia Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu 1948 Ibara ya 19); Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia 1966 – Ibara ya 19; Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu (Banjul Charter 1981- Ibara 9); Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria mbalimbali zilizotungwa, tumegundua kuna mapungufu kadhaa kwenye Sheria ya Takwimu namba 9 ya mwaka 2015.

Hivyo basi, tumekubaliana kwa pamoja kuleta maoni na mapendekezo yetu kwa lengo la kuboresha sheria hii. Miongoni mwa maeneo yanayohitaji maboresho ni pamoja na;

1.1. Maana ya “Takwimu Rasmi”

Kifungu cha tatu (3) cha Sheria ya Takwimu kinatoa tafsiri mpya ya maana ya takwimu rasmi ikimaanisha takwimu zilizoandaliwa, kuthibitishwa, kukusanywa au kusambazwa kwa idhini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Tafsiri hiyo haijazingatia jukumu na wajibu wa wadau wengine ambao pia wanazalisha takwimu kama vile Asasi za Kiraia (AZAKI), wadau wa maendeleo, vyombo vya habari na watu binafsi.

Wadau hawana fursa ya kutoa taarifa za kitakwimu kutokana na kuunganishwa kwa tafsiri hizo mbili ambazo ni takwimu rasmi na taarifa za kitakwimu kama zinavyoainishwa chini ya kifungu cha 5, 6(2)(c) na (f), 19, 22(2), 23(1), 28 na 37(2)(4)(5)(6) kwa hiyo hulazimika kupata kibali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Hili litasababisha kukosekana kwa taarifa mbadala ili kuzilinganisha na kuzifanyia tathmini kwa ajili ya kujenga hoja.

1.2. Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhodhi mamlaka ya kuzalisha taarifa za kitakwimu

Kwa mujibu wa sheria ya takwimu kifungu cha 3 na cha 18, kimeipa NBS mamlaka ya makubwa ya kukusanya na kutoa takwimu rasmi.

  1. Vifungu hivi vinakwenda kinyume na Mkataba wa Afrika wa Takwimu wa Mwaka 2009 unaotafsiri mamlaka za takwimu kama taasisi za Kitaifa za kitakwimu au taasisi nyingine zinazosimamia uzalishaji na usambazaji katika ngazi ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
  2. Vifungu hivyo(cha 3 na cha 18) vimeongeza urasimu kwenye mchakato mzima wa kukusanya na kusambaza Takwimu na kuleta vikwazo visivyokuwa na ulazima katika kupata takwimu muhimu.
  3. Sheria hii haijaainisha kipindi maalumu kwa NBS kushughulikia maombi ya vibali vya kufanya tafiti kama inavyoainishwa. Kadhalika, haijaainisha utaratibu maalumu wa maombi ya vibali.
  4. Sheria hii imerundika majukumu kwa NBS ya kusimamia takwimu kutoka vitengo vyote vya Serikali pamoja na wadau wengine. Mzigo huu wa majukumu unaweza kuathiri uwezo wa NBS.
  5. Sheria haina utaratibu wa kukata rufaa endapo mwombaji akinyimwa kibali cha kuchakata na kusambaza taarifa za kitakwimu jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 13(6)(a) inayotoa haki ya kukata rufaa.

1.3. Usambazaji wa takwimu rasmi

Sheria inaipa NBS mamlaka ya kutoa vibali vya kufanya utafiti, kuusimamia na kuidhinisha matokeo ya utafiti kabla ya kusambazwa kwa mujibu wa kifungu cha 24 A na B.

i. Mahitaji haya ya vibali zaidi ya mara moja yanaongeza urasimu na gharama za uendeshaji ikiwemo muda na fedha.

ii. Utaratibu wa vibali zaidi ya mara moja pia unaminya uhuru na haki ya kutoa matokeo huru kwa kuwa Ofisi ya Takwimu kutokana na mamlaka iliyonayo, huenda ikasita kuidhinisha takwimu ambazo zitatofautiana na zile za Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

1.4. Makosa na adhabu

Kifungu cha 37(4) kinaainisha makosa na kutoa adhabu zisizokuwa na ukomo. Hii ni kinyume na nadharia ya misingi ya utoaji adhabu. Hata hivyo, ingawa sheria hii imetungwa kwa ajili ya takwimu rasmi zinazoandaliwa na kurasimishwa na NBS lakini sheria inatoa adhabu kwa takwimu zote rasmi na zisizo rasmi.

2. Mapendekezo

Kwa kuzingatia Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 inayowapa wananchi haki ya kutafuta, kupata na kusambaza taarifa, na umuhimu wa takwimu katika maendeleo ya nchi yetu, tunapendekeza sheria ya takwimu ifanyiwe marekebisho kama ifuatavyo;

2.1. Makosa na adhabu chini ya sheria hii yajikite katika kusimamia mchakato mzima wa upatikanaji na usambazaji wa takwimu rasmi na sio takwimu zote kwani makosa na adhabu zinazohusiana na upotoshaji wa taarifa nyingine unashughulikiwa na sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 na sheria nyingine.

2.2 Sheria itambue uwepo wa taasisi na wadau wanaoandaa takwimu huru ambazo ni mbadala wa takwimu rasmi ili kuwezesha kuwepo kwa mijadala hai na chanya kwa maendeleo ya taifa letu.

2.3 Kwakuwa sheria imetoa tafsiri ya “takwimu rasmi” ni vema pia, itoe tafsiri ya neno “takwimu zisizo rasmi” na kuweka mipaka iliyo wazi baina ya maneno hayo.

2.4 Sheria iondoe sharti la kuomba vibali zaidi ya mara moja kwenye kuandaa, kukusanya na kusambaza takwimu rasmi.

2.5 Kifungu cha 37(4) kinachohusu adhabu kinahitaji kufanyiwa marekebisho yafuatayo;

i. Sheria iweke ukomo wa adhabu ili iendane na nadharia ya misingi ya kutoa adhabu na kuepusha uwezekano wa utoaji wa adhabu kinyume na haki za binadamu.

ii. Kuondoa takwimu zisizo rasmi kwenye adhabu kwani sheria hii inahusu takwimu rasmi.

2.6Sheria iongeze kifungu kinachowawezesha wadau kukata rufaa pale ambapo maombi yao ya vibali yamekataliwa na hawakuridhika na maamuzi ya Ofisi ya Takwimu, sheria ielekeze NBS kutoa sababu za kutokutoa vibali kwa muombaji.

3. Hitimisho

Sisi tunaamini kuwa, uhuru wa kupata na kusambaza taarifa ni nguzo muhimu katika kuchochea ushiriki wa wananchi na wadau katika maendeleo ya nchi.

Katika hoja yetu tumeainisha maeneo yanayohitaji maboresho na kutoa mapendekezo yenye lengo la kuboresha Sheria ya Takwimu Namba 9 ya mwaka 2015 ambayo tunaamini Serikali itayashughulikia.

Ikumbukwe kwamba, sheria hii pamoja na umuhimu wake, inaathiri upatikanaji na usambazaji wa takwimu. Kuendelea kwake kutumika bila marekebisho, kunaathiri shughuli za maendeleo na kijamii hususan shughuli za AZAKI.

Kwa msingi huu, tunaiomba Serikali iyazingatie maoni yetu na kuchukua hatua stahiki katika kurekebisha sheria hii ili kuhakikisha misingi ya Utawala Bora inazingatiwa kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ni sheria mama.

Imeandaliwa na kutolewa na;Wanachama wa Policy Forum kwa kushirikiana na, Twaweza na TAMWA. Na Kuwasilishwa na;Japhet Makongo - Mwenyekiti wa Mtandao wa Policy Forum

5, Disemba, 2018.