Skip to main content
Submitted by Web Master on 16 July 2008

KAULI YA FEMACT  (15/07/2008) JUU YA

KIFO CHA MWANAMKE MJAMZITO MWANANYAMALA HOSPITALI

Tumepokea na kufuatilia mkanganyiko wa sababu za kifo cha mama mjamzito (Tedy Dimoso) na kichanga wake wakati wa kujifungua kwa masikitiko makubwa sana. Kwa mujibu wa barua kutoka kwa msimamizi wa mirathi kifo hiki kilitokea tarehe 01/06/2008 katika hospitali ya Mwananyamala. Barua hiyo ya tarehe 06/06/2008 kwenda kwa Waziri wa Afya inatoa maelezo kwa kina jinsi kifo hicho kinavyoweza kuwa kimetokea kwa uzembe.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliamua kuunda tume tarehe 18/06/08. Hatupiganii kifo cha Tedy Dimoso peke yake bali tunapigania vifo vya wanawake wajawazito katika mkoa wa Dar es Salaam na nchini kote. Wanawake wajawazito 578 kati ya 100,000 hufariki kila mwaka hapa Tanzania, hii ni sawa na mwanamke mmoja kila siku! Mkuu wa Mkoa anaonekana kutetea uzembe uliofanywa na Hospitali ya Mwananyamala na hivyo kuleta wasiwasi kama matatizo haya ya vifo vya wanawake wakati wa kujifungua yatatutuliwa. FemAct bado tunadai usahihi wa kilichotokea na kutaka haki itendeke pande zote mbili: upande wa marehemu na upande wa hospitali. Kwa mujibu wa mazungumzo ya simu na Mkuu wa Mkoa leo tarehe 15/07/2008 saa tatu asubuhi, Mkuu wa Mkoa anakiri kwamba taarifa ya Tume yake ilikuwa na jukumu la kumtafutia taarifa yeye mwenyewe kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa. Mkuu wa Mkoa amekubali kwamba mtu yeyote anaweza kuunda tume ya uchunguzi ili tupate majibu ya kina zaidi.

Kwa mtazamo wetu tume hii ilikuwa na mapungufu yafuatayo; Wajumbe wake hawakujulikana hadi tarehe 11/07/2008 Kandoro alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ripoti yao. Wananchi hawakutangaziwa hadidu rejea za tume hii. Wananchi hawakutangaziwa tume itafanya kazi kwa muda gani na katika ofisi gani ili walio na maoni au ushahidi wapate kupeleka. Wajumbe wa tume hii wote ni watendaji wa serikali, hivyo kulikuwepo mgongano wa maslahi. Taarifa ya tume imetoa maelezo yale yale ambayo Mkuu wa Mkoa alikuwa akitoa kila siku, hivyo kutia shaka kama watu wote waliohusika na kushuhudia tatizo hilo wanafikiri kama Mkuu wa Mkoa.

Kwa mujibu wa nakala ya taarifa kwa vyombo vya habari tarehe 11/07/2008 toka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bado usahihi wa sababu za kifo cha marehemu Tedy Dimoso haujapatikana. Pia taarifa hiyo haioneshi kama inalifahamu tatizo sugu la vifo vya akina wanawake wakati wa kujifungua na sababu zake. Tungependa kujua tume ilihoji watu gani na hao watu walitoa maoni/mawazo gani. Kwenye taarifa hiyo hakuna kabisa maelezo kutoka kwa ndugu wa marehemu na wala wagonjwa wengine wambao walikuwa wodini na marehemu kabla hajafa. Pia inasemakana kwamba Mkuu wa Mkoa hajawahi kuwasiliana na ndugu wa marehemu tangu kifo hicho kitokee.

Tunahitaji Mkuu wa Mkoa atoe ufafanuzi wa haya yafuatayo;
• Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hospitali ya Mwananyamala ilipangiwa pesa za dawa peke yake shilingi 174,502,463 katika mwaka wa fedha 2007/08. Ni kiasi gani cha pesa hizi zilitumika? Kwa nini Tedy Dimoso alifariki kwa kukosa dawa?
• Kwa mujibu wa Mpango wa Utoaji huduma za Afya (CCHP) wa Manispaa ya Kinondoni mwaka wa fedha 2007/08, Hospitali ya Mwananyamala ilipanga kutumia shilingi 22,000,000 kugharamia dawa na vifaa vingine kwa kitengo cha Uzazi hospitalini Mwananyamala. Ni kiasi gani cha fedha hizi zilitumika mwaka wa fedha 2007/08?
• Pia Hospitali ya Mwananyamala ilitengewa shilingi 210,000,000 kujenga jengo la ghorofa moja kwa ajili ya huduma za mama na mtoto katika hospitali ya Mwananyamala. Ujenzi wa jengo hili umefikia wapi? Kwa nini Tedy Dimoso alifanyiwa upasuaji wodini?
• Kwa mujibu wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Sera ya Wananchi Kuchangia Gharama za Huduma za Afya katika Hospitali ya mwaka 1994, mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanastahili kupata huduma za afya bure bila malipo. Kwa nini ndugu wa marehemu Tedy Dimoso waliambiwa wakanunue dawa?
• Bado tunahitaji maelezo sahihi sababu gani dizeli lita 120 zilitolewa kuchangia kusafirisha maiti. Sababu zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa kwamba ilikuwa ni utu siyo sahihi. Tunahitaji kujua kama kuna bajeti ya kuchangia misiba ambayo marehemu wamefia hospitali za serikali ili watu wengine wote waweze kuipata. Vingenevyo ni vigezo gani vilivyotumika kwa marehemu huyu peke yake, na pesa hizo zilitoka mfuko gani, na ziliidhinishwa katika kikao gani cha Baraza la Madiwani?
• Kwa mujibu wa kifungu namba 14 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 toleo la 2005, kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake. Kwa nini serikali haikutimiza wajibu wake wa kutunza na kuhakikisha uhai wa Tedy Dimoso?

Tunahitaji kuona Mkuu wa Mkoa anafanya yafuatayo;
• Anatupilia mbali ripoti ya tume yake bubu na kuunda tume huru kuchunguza matatizo na vifo vya wanawake wakati wa kujifungua na watoto chini ya miaka 5 katika Jiji la Dar es Salaam. Wanawake wote waliojifungua tangu Januari 2007 (au ndugu wa marehemu) ni vizuri wakahusika kuhojiwa.
• Mkuu wa Mkoa anaomba radhi kwa wananchi wa Manispaa ya Kinondoni kwa dharau aliyoonesha wananchi wanaolijua tatizo hili kwa kina pamoja na ndugu wa marehemu
• Mbunge wa Kinondoni Idd Azzan anaomba radhi wapiga kura wake kwa kutoa kauli potofu Bungeni kuhusu tatizo hili.
• Mkuu wa Mkoa anawajibisha wote watakaobainika kuhusika na uzembe huo
• Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Kinondoni hawatumii vitisho na propaganda kutisha wananchi wanaojaribu kutetea haki na uhai wa wananchi
• Kubandika taarifa ya kiasi gani cha pesa kilipokelewa na muda gani katika Hospitali zote na vituo vya afya na zahanati. Nakala za mpango kazi na bajeti ya utoaji huduma kwa kila Hospitali, Kituo cha Afya, na Zahanati zibandikwe sehemu ya wazi wananchi na wahudumu wa afya waweze kufuatilie, kutathmini na kuwajibisha watendaji husika.

Imetolewa na Wanaharakati wa mtandao wa haki za binadamu na jinsia (FEMACT) na kusainiwa na

Ms. Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
Kwa niaba ya FEMACT
15 Julai 2008