Skip to main content
Submitted by Web Master on 10 February 2012

Mtandao wa Watetezi wa  Haki za Binadamu Tanzania (THRD-Coalition) unaoratibiwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Pamoja na mtandao wa asasi za kiraia wa Policy Forum wanatoa wito kwa Serikali kuwaachia mara moja Watetezi wa  haki za binadamu 16 ambao waliwekwa chini ya ulinzi mnano tarehe 9/2/2012 katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.  Tukio hilo  limekuja siku moja baada ya wanaharakati kuungana na  kuishinikiza serikali irejee mezani kufanya mazungumzo na madaktari  ambao kwa takribani mwezi mmoja sasa wameingia kwenye mgomo na kusitisha huduma za afya katika hospitali kuu zote za umma nchini.

Waliowekwa chini ya ulinzi ni pamoja na wakurugenzi watendaji Dr. Helen Kijo Bisimba wa LHRC, Mama Ananilea Nkya wa TAMWA, na Irenei Kiria wa SIKIKA.  Wengine  ni pamoja na wafanyakazi watano wa  TGNP,   wafanyakazi wa LHRC  Marcossy Albanie, Anna Migila, Wakili Godfrey Mpandikizi na Mwanasheria toka  Chama cha Mawakili Kanada Erin Riley, pamoja na wanaharakati wengine ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja. Mtandao unaamini kuwa kamata hiyo imetokana na msimamo wa wanaharakati katika swala hilo ambao kwa takribani mwezi mmoja sasa wamekuwa wakitoa matamko kwa umma kupitia vyombo vya habari, na kuitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika katika sakata hilo. 

Siku moja kabla ya kushikiliwa, wanaharakati hao walitoa tamko la pamoja kutokana na kusikitishwa na vifo vya watanzania katika hospitali za umma.  Wanaharakati wanaoshikiliwa wanaamini kuwa haki ya kuishi ni haki ya msingi ambayo bila hiyo hakuna haki nyingine zinazoweza kutekelezeka.  Tunaamini kamata kamata hiyo ina nia mbaya na haikuwa ya lazima kwani wanaharakati hao walikwenda Muhimbili kuangalia mambo yalivyokuwa yakiendelea.

Ni vyema tukakumbuka pia kuwa nchi nyingi duniani zimekuwa na tabia ya kuwashikilia watetezi wa haki za binadamu kwa tuhuma zisizo na msingi.  Mtandao unaomba mshikamano na umoja kutoka kwa vyombo vya Habari, wasanii na jumuia zote za kitaifa na kimataifa zinazotetea haki za binadamu.
             
 
Onesmo Olengurumwa,
Mratibu wa Mtandao
Mtandao wa watetezi  Haki za Binadamu Tanzania-THRD-Coalition
P. O. Box 75254 Dar es Salaam, TANZANIA Telephone: +255-22-2773038/48, Fax: +255-22-2773037, Mob: +255 783 172394 E-mail: thrddefenders@gmail.com