TAMKO: Ufisadi katika sekta ya umeme unapima uadilifu na uwajibikaji wa serikali ya Tanzania

Categories

Kufuatia kutolewa na kujadiliwa kwa taarifa ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuhusu Independent Power Tanzania Limited (IPTL)  Akaunti  ya Tegeta  ya Escrow (TEA) bungeni  na kilio cha umma kilichofuatia  kuhusu kufichuliwa kwa  ufisadi ambao haujawahi kuwapo wa aina  hiyo, Sisi, Asasi za Kiraia (AZAKI) tajwa hapo chini , tunapenda kuwasilisha msimamo wetu wa pamoja kuhusu utata wa suala hili.

 

Tumefanya mapitio ya taarifa ya  Ofisi yaTaifa ya  Ukaguzi (NAO)  kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali  (PAC), pia taarifa ya PAC  ya tarehe 26 Novemba 2014 Bungeni, pamoja na machapisho mengine mengi kuhusiana na suala hili, na TUMEBAINI yafuatayo kuhusu mapungufu ya taasisi zetu katika kuendesha shughuli zao kwa uwazi na uwajibikaji:

1. Ya kwamba  jinsi Pan Africa Power Solutions Tanzania (PAP) ilivyochukua hisa za Mechmar ambazo ni  asilimia 70 ya hisa za IPTL kwa uwizi wa ujanja na uhawilishaji wa fedha za TEA zisizopungua Dola za Kimarekani milioni 120 kwa IPTL/PAP uliofanywa  ulikuwa kinyume cha sheria  na ulihusisha  njama  baina ya   maafisa wa serikali wa ngazi ya juu, Wakurugenzi wa Bodi ya Tanesco,  Shirika la Uandikishaji na Utoaji Leseni  za Biashara (BRELA) na Benki binafsi.

2.Ya kwamba utoaji wa fedha  toka TEA mwaka 2013  ulikuwa ndiyo kilele cha miongo miwili ya utekwaji  wa sera ya nishati  kwa faida binafsi  na rushwa iliyohusisha  IPTL, Tanesco  na Wizara ya Nishati na Madini (MEM).

3. Ya kwamba mchakato wa usuluhishi kupitia Kituo  cha Kimataifa cha Uamuzi wa Migogoro  ya Kiuwekezaji  (International Centre for the Settlement of Investment Disputes (ICSID)  ulioanzishwa na TANESCO mwaka 2008 ili kupata suluhisho juu ya malipo yanayosemekana kupitiliza tozo la uwezo (capacity charges) kwa kipindi chote  cha mkataba  (mwaka 2002 hadi leo)   ulihujumiwa  na PAP pamoja  na wamiliki wadogo wa zamani wa hisa  za IPTL , VIP Engineering and Marketing (VIP) kwa  kutumia kijanja mfumo wa kisheria wa Tanzania, na kuacha  suala la gharama za umeme wa IPTL bila utatuzi.

4. Dhana ya kwamba “TEA siyo fedha za umma” ni hoja inayotolewa na  watetezi wa IPTL/PAP/VIP   ili kukanganya mjadala mweledi wa masuala ya msingi yaliyopo.

TUNAWAPONGEZA CAG na  PAC  kwa wajibu wao  muhimu wa kufuatilia  na kuwawajibisha maofisa wa serikali kwa vitendo  na  maamuzi yao  kuhusu  IPTL/TEA  kujipatia fedha isivyo halali  kwa kukagua taarifa husika za  mahesabu ya fedha  na kutaka maelezo  na uhalali  kutoka kwa wahusika.  Katika mfumo wa kidemokrasia,  hata hivyo, hii haitoshi.  Wakati maelezo na uhalali  kutoka kwa wenye wajibu huo yanapoonekana hayaridhishi, bunge linawajibu wa  kuhakikisha hatua za marekebisho zinachukuliwa kwa kutumia uwezo wake wa kisheria na kikatiba .

TUNASIKITISHWA    na  jinsi ambavyo fedha za TEA zilihawilishwa (hamishwa) kirahisi kutoka Benki kuu ya Tanzania (BOT) kwenda  benki binafsi, na hatimaye kwenda kwenye  akaunti za watu binafsi. Vitendo hivi vinadhihirisha ukosefu wa  uangalifu unaotakiwa kwa upande wa wahusika. Tunamashaka na mambo mengine yafuatayo yanayohusiana na hili:

 

·        BRELA:Taarifa ya CAG inaonyesha  wazi kuwa kulikuwa na nyakati ambapo ukosefu wa uangalifu unaotakiwa  ulijitokeza katika michakato  ya  Mamlaka ya Uandikaji na Utoaji Leseni za Biashara (BRELA)   kuhusu  uhawilishaji wa kinachofikiriwa kuwa ni fedha  zinazomilikiwa na Mechma ambazo ni 70 % za hisa za IPTL.  Wamiliki wa  chombo kisichofahamika  cha Piper Link, PAP  na mmliki hisa wake  asiyefahamika, Simba Trust, wote  wakiwa washiriki katika hujuma hii, walitakiwa wawe wamegundulika katika uchunguzi wa awali au kusita kufanya waliyoyafanya wangejua kuwa majina yao yanaweza wekwa wazi hadharani.   

 

·       Uangalifu unaotakiwa na mabenki na mashaka  kuhusu utakatishaji  fedha:  Chini yaSheria ya  Uzuiaji wa Utakatishaji Fedha (Anti-Money Laundering Act)  ya mwaka 2006,  benki zote na taasisi zote za fedha lazima zichukue hatua za uangalifu unaotakiwa za kuwatambua watu walio na nafasi kubwa kisiasa na kubaini vyanzo vya fedha zao na kuwafuatilia.  Ukweli wa kwamba viongozi wa ngazi za juu kisiasa, baadhi yao wakiwa wamehusika dhahiri katika kashfa za rushwa katika kipindi kilichopita,  walifungua akaunti katika Benki ya Mkombozi na kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kunaonyesha kwamba taratibu za kawaida za kuwafuatilia wateja ikijumuisha hatari ya utakatishaji fedha hazikuzingatiwa.  

 

Muamala wa dola milioni 65 za Marekani kutoka Benki ya Mkombozi  kwenda benki ya huko Uholanzi kunaonyesha ukiukaji wa taratibu za kawaida za “kumjua mteja wako”.  Benki ya  Stanbic  kwa upande wake inatuhumika kwa kula njama katika ulipaji wa kiasi kikubwa cha fedha taslimu kwa wanufaika wa PAP/IPTL katka muda wa siku moja.   Ukweli wa kwamba PAC haikuweza kuhakiki majina ya wengine ambao akaunti zao za benki zimeingiziwa kiasi kikubwa cha fedha kinacholeta mashaka  na ya kwamba Kitengo cha Kiintelijensia  cha Fedha  (FIU) hakikujulishwa kuhusu miamala hiyo, pia kunaonyesha ukiukaji wa kanuni  na taratibu za kibenki. Ingawaje Benki Kuu ya Tanzania  ilichukua hatua za kujisafisha  dhidi ya changamoto za kisheria zinazoweza kujitokeza kuhusiana na TEA, ilishindwa kuchukua uangalifu wake binafsi juu ya kesi hii ikitegemea dhamana ya wahusika wakuu.  

 

·       Uwazi wa mikataba: Msukumo uliopo hivi sasa wa kufanya mikataba ya sekta zote za nishati kuwa wazi ni lazima  ijumuishe mikataba kati ya serikali na wazalishaji binafsi wa nishati  ikiwa ubia  baina ya Serikali Na Wazalishaji Binafsi (PPP) hautafedheheshwa. Hivi sasa kuna ongezeko la sababu siyo tu za kuweka wazi mikataba bali ushiriki kamilifu wa bunge katika mchakato wa mikataba ,  kuanzia utoaji wa zabuni, utendaji na ukamilishaji pale panapokuwa na mikataba ya pamoja  ya aina hii (joint venture agreements). Ushiriki kamili wa  umma na bunge katika kuchunguza na kujadili mikataba ya PPP na utekelezaji wa mikataba hiyo kungelifanya  hali iwe ngumu kwa PAP na VIP kutumia mwanya wa udhaifu wa kimfumo  ndani ya BRELA, Tanesco  na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujinufaisha.

 

·       Utamaduni wa kuepuka adhabu: Ikiwa wale waliohusika katika kashfa hii hawatawajibishwa  kwa kutumia mamlaka yao vibaya na kwa uwizi wa fedha za umma, itakuwa ni mwendelezo wa udhaifu wetu wa kimfumo kuhusiana na kuwafungulia mashitaka viongozi walioonekana kuhusika na vitendo vya rushwa, baadhi yao wakiwa  wamerudia makosa hayo hayo. Umma unazidi  kuumizwa na vitendo hivi vya rushwa ya viwango vikubwa,  na jinsi ambavyo watuhumiwa wa rushwa wanavyojitetea pia na kile kinachojitokeza kama uwezo wao wa kuepuka adhabu.

 

Kuna hatari kwamba mwendelezo wa kuepuka adhabu kutawasilisha jumbe zisizo sahihi kwamba: 1) Hakuna hatari kutumia kiwango kikubwa cha fedha za umma kwa ubadhirifu,  na 2) dola haina  mamlaka  ya kuwashughulikia watenda maovu.

Kwa mwanga wa hayo hapo juu, TUNATOA WITO kwa Serikali  kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika katika uporaji wa TEA kwa matumizi mabaya ya mamlaka na uwizi wa fedha za umma.   Hasa, tunataka Serikali iagize  mara moja na kwa uwazi urejeshaji wa fedha zote za escrow zilizolipwa kwa  ulaghai  kwa PAP, pamoja na faida  na itekeleze mapendekezo ya Bunge  na kutatua  suala hili la IPTL kwa manufaa ya umma. Hatua hizo ni:  

1. TAKUKURU, polisi  na vyombo vingine vya usalama wachukue hatua dhidi ya wale wote waliotajwa na PAC  kwenye taarifa yake na wengine watakaobainika kuhusika baada ya uchunguzi zaidi;

2. Wenyeviti na wajumbe wa Kamati za Bunge waliohusishwa katika sakata  hilo waadhibiwe;

3. Benki ya Stanbic, Benki ya Mkombozi na taasisi nyingine za fedha zichunguzwe kwa kushindwa kuwa na uangalifu unaotakiwa na kwa utakatishaji fedha;

4. Mapitio ya Sheria ya TAKUKURU (PCCB Act) yafanyike ili kukabiliana  na viwango vikubwa vya rushwa  na uhujumu wa uchumi;

5. Serikali iangalie uwezekano wa kuumiliki mtambo wa IPTL;

6. Serikali  ifanye mapitio ya mikataba yote ya uzalishaji wa umeme.

Kashfa hii ya IPTL inaleta hali ya wasiwasi kuhusu uadilifu wa Serikali ya Tanzania  ambayo inaweza kutatuliwa tu kwa  uongozi imara wenye  maamuzi  thabiti ili kumaliza kwa mara ya mwisho kashfa hii iliyodumu kwa muda mrefu.

 

Imetiwa sahihi na:

1.      Policy Forum

2.      Tanzania Coalition on Debt and Development

3.      ACTIVISTA

4.      Tanzania Youth Vision Association

5.      SIKIKA

6.      Action Aid Tanzania

7.      HakiElimu

8.      Youth Partnership Countrywide

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter