Tamko Rasmi:-Bajeti 2015/2016

Categories

Bajeti ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2015/16 kwa sasa inajadiliwa Bungeni. Bajeti nzima ya Serikali itawasilishwa na Waziri wa Fedha mara baada ya uwasilishaji na mjadala wa bajeti za wizara kukamilika. Kwa kuzingatia umuhimu wa tukio hili kitaifa, wajumbe wa  Kikundi Kazi cha  Bajeti cha Policy Forum, tunapenda kutoa mchango wetu katika mchakato huu muhimu kwa kuchangia uchambuzi wetu. 

Bajeti ya taifa ya  mwaka huu inaashiria mwisho wa mfumo wa utawala uliopo wa Ubunge na Uraisi, pia mwisho wa kipindi cha mpango wa sasa wa maendeleo ya miaka mitano. Mwaka wa fedha 2014/15 (kama ilivyokuwa kwa mwaka 2013/14) umeshuhudia upungufu wa mapato jambo linalomaanisha kwamba bajeti iliyopitishwa haikukidhi  matumizi yaliyopangwa; na kuathiri miradi ya miundo mbinu na uwekezaji katika shughuli za kijamii. Pia imeshuhudia kwamba kumekuwa na upungufu katika mchango wa serikali kwa huduma za kijamii, kama vile elimu, maji na afya. Kwa mara nyingine tena kumekuwa na ucheleweshaji katika upelekaji wa fedha toka Serikalini na  kutoka kwa Washirika  wa Maendeleo kwa mwaka 2014-15, na kwa mwaka 2013-14.  Kwa kutambua athari mbaya zinazotokana na masuala haya muhimu, tunawasilisha mapendekezo ya Policy Forum kama ifuatavyo:

Ukusanyaji wa Rasilimali za Ndani

Tunakubali kwamba kumekuwa na jitihada kwa upande wa Serikali kuhakikisha kuwa bajeti yetu ya taifa haitegemei sana fedha toka kwa wafadhili wa nje.  Kufikishwa bungeni kwa miswada ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)na  Usimamizi wa Kodi mwaka jana ni kwa sehemu, ushahidi wa juhudi za serikali katika kuhakikisha ukusanyaji na usimamizi (menejimenti) unaopasa wa rasilimali fedha kutoka ndani.   

Hivi karibuni, wakati Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya alipowasilisha mapendekezo ya awali kuhusu bajeti kwa Wabunge jijini Dar es Salaam, alisema kuwa bajeti ya 2015/16 ni Sh. trilioni 22.48 toka Sh. trilioni 19.8  kwa mwaka 2014/15: ongezeko la 15%.  Katika hizo Sh. Trilioni 22.48, bajeti ya kawaida ni Sh. trilioni 16.7 wakati  bajeti ya maendeleo  ilitengewa Sh. trilioni 5.7  (kama 26%)  ya bajeti yote.

Kuhusu vyanzo vya hii bajeti, Waziri aliainisha kuwa kati ya hizi Sh. trilioni 22.48 za bajeti, Sh. trilioni 14.82 zitakusanywa kutoka ndani ya nchi. Mchanganuo wa kiasi kitakachokusanywa kutoka ndani unaonyesha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania inategemewa kukusanya Sh. trilioni 13.35 ikilinganishwa na Sh. trilioni 11.297 zilizotegemewa kukusanywa na mamlaka  hiyo mwaka 2014/15. Mapato yasiyo na kodi yanategemewa kuwa Sh. bilioni 949.2  wakati mamlaka ya Serikali za Mitaa yanategemewa kuchangia Sh. bilioni 521.9  kwenye bajeti. Licha ya kukopa kutoka wakopeshaji wa ndani na wa nje ya nchi, serikali inategemea kupokea kiasi cha kama Sh. trilioni 2 kutoka kwa washirika wa maendeleo. 

Hii hatua ya Serikali inapokelewa na inapongezwa. Changamoto kubwa inayotokana na hatua hii  hata hivyo, ni kama serikali itaweza kukusanya mapato haya kwa kiasi cha kutosha.   Policy Forum inaona  - kwa kuwa huu  ni mwaka wa uchaguzi pamoja na kura ya maoni– juhudi kubwa zaidi zinahitajika  ili kuongeza mapato; kwa kuwa rasilimali nyingi  zitatumika katika mchakato wa uchaguzi.

Je  Bajeti Hii Inazingatia Hali Halisi?

Utekelezaji wa bajeti iliyopita, hauleti matumaini kuhusu bajeti mpya inayokuja. Kutokana na taarifa ya Waziri, ucheleweshaji katika  utoaji wa fedha bado ni tatizo kubwa. Kwa mfano, hadi Machi 2015 ni 38% ya bajeti ya maendeleo iliyotolewa.   Hii inamaanisha kuwa  zaidi ya 50%  ya miradi ya maendeleo iliyokusudiwa haijatekelezwa, wakati imebaki chini ya miezi 3 kabla ya mwisho wa mwaka.   Hii ndiyo hali ilivyokuwa pia kwa kwa bajeti ya kawaida, kama taarifa zilizotolewa kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa hazijapokea bajeti iliyoidhinishwa kwa matumizi ya uendeshaji.

Kutokana na hayo yaliyotajwa juu, kuna mashaka kuhusu ongezeko la bajeti bila tamko  wazi la jinsi fedha hizo zitakavyopatikana tofauti na mwaka uliopita; ili tuwe na uhakika kuhusu upatikanaji wa fedha. Matumizi yasiyo ya kipaumbele ni vyema yakaainishwa ili Serikali iweze kutumia busara zaidi katika matumizi kwa mwaka 2015/16

Je Kumekuwepo Usimamizi wa Kutosha kwenye Mchakato wa Kupanga?

Kama Asasi za Kiraia (Azaki) tumejifunza kuwa utayarishaji wa makadirio ya bajeti, kwa bahati mbaya haukushirikisha Kamati ya Bunge ya Bajeti. Hili linafanya tujiulize maswali  kwani tunaelewa kuwa kamati hii inawajibika kisheria kusimamia na kushauri serikali    kuhusu njia mbali mbali za kuongeza mapato, pamoja na jinsi ya kugawa / kutenga hizi rasilimali.  Itambulike kuwa kamati hujishughulisha na wadau mbali mbali, ikiwa ni pamoja na Azaki kujadili ni kwa jinsi gani mipango iwe. Maoni ya  wadau hufikia serikali kwa kupitia kamati hii. Kwa hiyo tunasisitiza Wizara ya Fedha  ifanye  mashauriano  na Kamati ya Bunge ya Bajeti.  

Wito wa kupitia upya vipaumbele vya Bajeti ya Elimu ya mwaka  2015/2016

Wakati tunajali kwamba sekta ya elimu inapewa kipaumbele cha kwanza katika mgawo wa fedha;  msisitizo wetu kwa bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka 2015/2016  ni  kwa jinsi gani huo mgawanyo unatilia maanani mahitaji ya kimafunzo na changamoto zilizopo. Changamoto hizi ni pamoja na upungufu wa muda mrefu wa ruzuku maalum kwa kila mwanafunzi, masuala kuhusu sera ambazo hazijatekelezwa, na malalamishi ya wadau wa sekta hii ambayo bado hayajapatiwa suluhu.   Kwa hiyo kiasi cho chote cha bajeti ya mwaka 2015/16 kitakachotengwa kwa ajili ya sekta hii  lazima kitoe majibu  kwa  masuala yafuatayo:

Kuelezea mpango wa elimu bure:   Sera mpya ya elimu ya mwaka 2014, inasema kwamba ‘ Serikali itahakikisha kuwa elimu ya msingi inatolewa bure bila kulipiwa ada kupitia mfumo wa elimu kwa umma’. Tunaamini kwamba huu ni mpango mzuri, lakini tunapenda jambo hili liakisiwe katika uwasilishaji wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka 2015/2016.  Serikali itamke kwa uwazi kabisa jinsi inavyopanga kuhakikisha kuwa tamko hili la kisera kuhusu kutolipa ada litakavyotekelezwa.  Ni muhimu kwamba Serikali ieleze waziwazi suala hili wakati wa mchakato wa upangaji wa bajeti ya mwaka huu, kwani tamko hilo la kisera tayari limeshaanza kuleta misuguano kati ya wazazi/walezi na wakuu wa shule wanaotegemewa kutekeleza sera hiyo. Baadhi ya wanajamii wamevunja  ahadi zao za kutoa michango ya shule, kutokana na tamko hili la kisera.   

Serikali imeweka kiwango cha ruzuku kuwa ni  Sh.10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh.25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari. Lakini, ikumbukwe kuwa kiwango cha sasa cha ruzuku kwa kila mwanafunzi kiliwekwa mwaka 2002 (msingi) na mwaka 2004 (sekondari). Kwa aina zote mbili, ni zaidi ya miaka 10. Gharama za maisha zimepanda, uchumi umedorora, thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kushuka. Itabaki kuwa nadharia ikiwa serikali itaendelea kutumia kiwango hicho hicho cha ruzuku kwa kila mwanafunzi wakati thamani yake (kwa kipimo cha uwezo wa ununuzi) imeshuka. Hivyo basi, ni matarajio yetu kuwa  Serikali itatamka wazi wakati wa mipango ya bajeti hii ya mwaka 2015/2016 ni kwa vipi itarekebisha kiwango cha ruzuku kwa kila mwanafunzi ili iendane na hali halisi ya gharama za maisha.

Zaidi ya hayo, hali halisi ya MMEM na MMES kuhusiana na kutolewa kwa ruzuku kwa kila mwanafunzi imekuwa  kwa kiwango cha chini kwa miaka 10 iliyopita. Ruzuku kwa kila mwanafunzi hazikufika katika shule kwa muda uliotakiwa au kwa kiwango kilichotakiwa. Pamoja na hayo, sera mpya ya elimu imeongeza uondoaji wa ada juu ya hii changamoto ya kirasilimali. Utoaji wa ruzuku kwa kila mwanafunzi kwenda katika shule tangu kuanzishwa kwa MMEM na MMES haujawa wa kuridhisha.

Kufuatana na taarifa ya utekelezaji wa kauli mbiu ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa mwaka wa fedha 2013/2014, serikali iliweza kutoa wastani wa sh. 4,200 badala ya sh 10,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sh. 12,000 badala ya sh. 25,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari.

Hii hali imeendelea hata katika mgawo wa bajeti ya mwaka 2014/15,  wakati ambapo hadi kufikia tarehe 30 Machi 2015, wastani  wa sh. 865tu badala ya  sh. 10,000 zilikuwa zimefika shule  za msingi,  wakati wastani wa sh. 5,516 tu badala ya sh. 25,000 zilikuwa zimefika shule za sekondari. Ni ombi letu kuwa, bajeti ya mwaka huu sharti itoe utatuzi kwa suala la pengo la kirasilimali linalotokana na kutokutosheleza na mara nyingi ucheleweshaji wa ruzuku kwa kila mwanafunzi na uondoaji wa ada.  

Ili kuboresha usimamizi na ufanisi shuleni, ni muhimu taasisi hizi zikakaguliwa mara kwa mara. Bunge lihakikishe kuwa kwenye bajeti ya 2015/16 linaishauri Serikali kuupitia  Mpango Wa Matokeo Makubwa Sasa ili kuzifanyia kazi changamoto kwenye maeneo kama ukaguzi wa shule na kuwatia moyo walimu waweze kufundisha na wanafunzi waweze kujifunza.

Jinsia

Mapungufu katika bajeti (ikiwa ni pamoja na uwekaji wa vipaumbele usiofaa, ucheleweshaji katika utoaji / upelekaji  fedha, fedha zisizotosheleza, nk) vinaathiri makundi mbalimbali katika jamii kwa namna tofauti.

Makundi ambayo yako pembezoni, kwa mfano yanapata mzigo mzito zaidi kuliko makundi mengine. Ucheleweshaji katika utoaji / upelekaji wa fedha ambao umetokea   (ukichangiwa na fedha kutotolewa kabisa wakati mwingine) kumepelekea kwa viwango vya huduma zilizotakiwa  kutokufikiwa. Hili  linapotokea, kuna watu ambao hawana mbadala wa kupata huduma kwingine, bali wanabaki katika hali hiyo na kukumbana na athari kadiri zinavyokuja.

Mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2015/2016 yanaonesha kwamba serikali inapanga kuongeza mtaji katika Benki ya Kilimo; ili itakapoanza iweze kutoa mikopo kwa wakulima. Nchini  Tanzania, 98%  ya wanawake wa vijijini wenye nguvu ya   kufanya kazi wanajishughulisha na kilimo; na wanazalisha  kiwango kikubwa cha mazao ya chakula  kwa ajili ya matumizi ya nyumbani  na kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Wito tunatoa  kwa bajeti ya kilimo kuzizingatia jinsia ili kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi.   Benki tarajiwa sharti ikusudie na ipange kwa uwazi  ili kuhakikisha kuwa wanawake wa vijijini na wakulima wadogo wanaweza kupata hiyo mikopo.

Policy Forum inapenda kusisitiza tena kuwa  uzingatiaji wa masuala ya jinsia hakuna budi kujitokeze kwa nguvu zaidi katika sekta za  elimu, afya, na maji  ili  maisha ya wanawake yastawi.  

Katika miradi iliyopewa vipaumbele katika bajeti  ya mwaka 2014/15   zilihusu uwekezaji ambapomiradi mikubwa iliyo mingi inamilikiwa na wanaume;  yenye   matokeo ya muda mrefu kwa wakulima kama vile mashamba makubwa ya umwagiliaji maji; badala ya masuala ya pembejeo kama vile  mbegu bora, au benki za kijamii vijijini, ambayo yanaweza kuwa na matokeo yanayofanana (na hiyo miradi mikubwa)  lakini kwa kutumia rasilimali kidogo.  Tunahamasisha kwamba makundi   yaliyoko pembezoni  katika jamii yapewe vipaumbele.  

Hitimisho

Mchakato wa bajeti hauna mwisho.  Kwa hiyo tunajifunza  tunaposhiriki katika huo mchakato; na hayo mafunzo yachangie katika kuboresha bajeti ijayo. Kuna umuhimu wa Wizara ya Fedha  kupokea mchango wa mawazo kutoka kwa wadau mbali mbalikuhusu mbinu bora za kupanga kwa kutumia rasilimali tulizo nazo.  Kamati ya Bunge ya Bajeti pia ishirikishwe, ili kuweza kutoa utaalamu wake katika mchakato huu. Serikali inapoanza kuchukua hatua za kukusanya rasilimali, ni muhimu pia kuhakikisha  kuwa uwajibikaji kwa matumizi ya hizo rasilimali unaimarishwa.  Hilo linaendana na hitaji la kuboresha uwazi kwenye matumizi ya fedha katika utoaji wa huduma za umma. Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali iliyotolewa kwa mwaka ulioishia Juni 2014 inaonesha kwamba bado kuna tatizo kwenye matumizi ya rasilimali ya umma. Lakini pia kuna udhaifu katika utekelezaji wa maoni ambayo yamekuwa yakitolewa kwenye ripoti za ukaguzi. Kwa mfano, ni asilimia 38 tu ya maoni yaliyotolewa mwaka uliopita yametekelezwa ipasavyo. Hii inaonesha utendaji usioridhisha. Ufuatiliaji makini wa mapendekezo ya ukaguzi ni muhimu ili kuipa tija kazi ya ukaguzi.

Masuala ya kisera tunayoainisha hapa, hata hivyo yanahitaji moyo wa kujitoa ili yaweze kufanyiwa kazi. Kuendelea kuzorota kwa mifumo ya maji, afya, elimu na sekta ya kilimo  hakutakiwi kuendelee. Jamii iliyo na afya, yenye lishe bora, elimu  na ujuzi ni  muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ni kwa sababu hii tunaihimiza serikali itilie maanani haya mapendekezo machache  tunapoendelea kufanya kazi pamoja ili kufanya sera zitende kazi kwa ajili ya watu wa Tanzania.

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter