TAMKO LA POLICY FORUM : BAJETI YA 2017/18: MAMLAKA NA UFANISI WA SERIKALI ZA MITAA

Categories

Sisi wanachama wa Policy Forum, Mtandao wa Asasi za Kiraia;

Kufuatia kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2017/18 na Bunge la Bajeti la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) Juni 2017;

Kwa kuzingatia juhudi dhahiri za Serikali ya JMT katika kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za mandeleo kwa Watanzania;

Baada ya kuchambua Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, Hotuba ya Bajeti ya Wizara Fedha na Mipango, Hotuba ya Waziri OR-TAMISEMI, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano II, Taarifa ya Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali 2015/16, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; 

Tukiwa na ufahamu kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 145 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na majukumu yake kuainishwa katika Ibara ya 146, na kwamba mamlaka hizi zimetambuliwa na Agenda ya Maendeleo Endelevu Duniani ya 2030 (Sustainable Development Goals 2030) kuwa vyombo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu na kuondoa umaskini, na kwamba;

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 katika kifungu namba 3 cha Utawala Bora na Utawala wa Sheria kinachozungumzia demokrasia na ushiriki wa wananchi inatambua umuhimu wa kuziwezesha Serikali za Mitaa  katika kuwahudumia wananchi ndani ya mamlaka hizo.

Tunatambua juhudi kubwa za Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa malengo haya na kwamba, Serikali Kuu kupitia Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi ya Mwaka 1998 imeazimia kuzipa Serikali za Mitaa uhuru na mamlaka ya kutoa huduma na kuleta maendeleo katika maeneo yao. Hii ni pamoja na kuzipa mamlaka ya kupanga kukusanya na kutumia mapato yake ya ndani katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kwa kuwa  Mpango  wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17-2020/21 umejielekeza  katika kuongeza mapato ya ndani kutoka vyanzo vipya. Serikali kupitia mpango huu imetambua umuhimu wa kodi ya majengo kama chanzo kikuu cha mapato ya ndani ya Serikali za Mitaa na kusisitiza kuwa itaziwezesha Mamlaka hizi katika ukusanyaji wa kodi.Hata hivyo uzoefu wa miaka ya hivi karibuni umedhihirisha kuendelea kuongezeka kwa hali ya utegemezi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Serikali Kuu, jambo ambalo hata mwelekeo wa bajeti ya mwaka ya Mwaka 2016/17 na ya Mwaka huu 2017/18 umeziacha Serikali za Mitaa kwenye njia panda pale ambapo imeamua  kuziondolea baadhi ya vyanzo vyake vya mapato. Mfano, tathmini iliyofanyika mwaka 2012  na TACINE (Mtandao wa Majiji na Miji Tanzania) ilionyesha miji imekuwa tegemezi kwa Serikali Kuu kwa 73% kinyume na Sheria ya Mipango Miji ambayo inataka Manispaa zijitegemee kwa 70% na Majiji 95%;

Mtandao wa Policy Forum kupitia kikundi kazi cha Serikali za Mitaa tunapenda kutoa taarifa hii yenye maoni yetu kwa umma na mapendekezo kwa Serikali ili yazingatiwe katika kuboresha utendaji na ufanisi wa Serikali za Mitaa.

Maoni Yetu

Pamoja na sera nzuri ya ubia wa Serikali na sekta binafsi kama ambavyo imeelezwa vyema na Waziri wa Fedha na Mipango, miradi mingi ya ubia inayoonekana kufanikiwa ni ile inayotekelezwa na  Serikali Kuu. Nafasi ya Serikali za Mitaa kupata miradi hiyo inakuwa ngumu kwa kuwa inahitaji uwezo mkubwa wa kifedha wakati Halmashauri nyingi hazina na kuna ushahidi kuwa tayari zimenyang’anywa baadhi ya vyanzo vya mapato.

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti  ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dk. Philip Mpango (Mb) ya 2017/18, Serikali za Mitaa zimeondolewa mamlaka ya kukusanya baadhi ya vyanzo vyake muhimu vya mapato ya ndani ikiwemo Kodi ya Majengo na Kodi ya Mabango.  Jambo hili linaenda kinyume na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano II, ambao umetambua Kodi ya Majengo yaani “Property Tax” kama chanzo kikuu na muhimu cha mapato ya ndani ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwani inachangia  kati ya 30% hadi 60% ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Miji.

Kuondolewa kwa kodi hizi yaani kodi ya majengo na ile ya mabango, kutapelekea athari zifuatazo;

Serikali za Mitaa kuwa na upungufu mkubwa wa mapato ya ndani jambo ambalo litapelekea ufifishaji na ucheleweshaji wa utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo;

Kuzilemaza na kuongeza utegemezi wa Serikali za Mitaa kwa Serikali Kuu na hivyo kuendelea kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo;

Kuendeleza urasimu wa mgawanyo wa rasilimali zinazopaswa kuwafikia wananchi kwa wakati;

Kupunguza kasi na ari ya Serikali katika kutunza na kuboresha miundombinu katika halmashauri ambazo hutegemea zaidi vyanzo vyake vya ndani. Hii pia ingepunguza utegemezi kwa wafadhili na wawekezaji wa kimataifa badala ya kuwategemea wao kufadhili miradi ya Halmashauri zetu.

MAPENDEKEZO

Serikali ifikirie upya maamuzi ya kuzinyang’anya Mamlaka ya Serikali za Mitaa baadhi ya vyanzo vya mapato, badala yake itekeleze kikamilifu nia yake ya kuziimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kiutawala, kifedha na kisiasa ili ziwe huru kimapato na kimaamuzi kama ilivyoazimia katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano II.

Serikali ipeleke ruzuku ya kutosha na kwa wakati kwa Serikali za Mitaa ili kuwezeshautekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi kwa wakati.

Serikali za Mitaa ziongeze juhudi za kubuni vyanzo vipya vya mapato yake ya ndani ambavyo sio kero kwa wananchi ili kuziwezesha kutekeleza mipango yake kikamilifu.

Kwa kuwa Mwaka 2007 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipewa jukumu la kukusanya mapato ya Kodi ya Majengo kwenye Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke. Utekelezaji wa jukumu hilo ulikuwa duni na kurejeshwa kwenye Halmashauri husika. Mtandao wa PF unaishauri Serikali kuwa na msimamo kuhusiana na sera, sheria, mipango , kanuni na miongozo juu ya ukusanyaji wa kodi za majengo

Ili kuimarisha ushiriki wa wananchi kwenye mipango na bajeti ni vema mfumo wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo uliyoboreshwa (Improved O&OD) uhamasishwe nchi nzima.

Imeandaliwa na;

Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa - Mtandao wa Policy Forum.

Na Kuwasilishwa na;

Israel Ilunde,

Mwenyekiti - Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa

Policy Forum (PF)

1, August, 2017.

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter