Tamko la Kikundi Kazi cha Bajeti Kuhusiana na Bajeti ya Mwaka 2014/15

Categories

Wakati Waziri wa Fedha  anapowasilisha  Bajeti ya Taifa  kwa mwaka wa Fedha 2014/15  Bungeni  kesho, sisi  Wajumbe wa  Kikundi Kazi cha Bajeti  cha  Policy Forum, tunaowakilisha zaidi ya Asasi  70 za Kiraia tuliounganisha nguvu zetu  ili kuongeza uelewa na  ushiriki wa jamii katika uandaaji wa sera, tunapenda kutoa  mchango wetu katika mchakato huu  muhimu.   

Bajeti  hii ya Taifa inawasilishwa baada ya mwaka  wa fedha uliokuwa mgumu  ulioshuhudia upungufu  wa mapato  kwa mwaka 2013/14 ikiwa na maana kwamba matumizi yaliyopangwa  yalizidi bajeti iliyopitishwa, hali ambayo iliathiri  miradi ya  miundo mbinu  na huduma za kijamii, ikipunguza pia mchango wa Serikali kwa sekta za afya  na maji, pia kulikuwa na ucheleweshaji katika upelekaji  wa fedha za serikali na za wabia wengine wa maendeleo  kwa mwaka wa fedha 2013/14. Tukizingatia masuala haya nyeti, tunaleta mapendekezo yetu  muhimu ya kisera  kama ifuatavyo:

Ukusanyaji wa Rasilimali (Mapato) za Ndani

Kabla ya kuwasilishwa  kwa Bajeti ya Taifa ya mwaka  2012/13  miaka miwili iliyopita,  Kikundi Kazi cha Bajeti cha  Policy Forum kiliona kwamba Tanzania  ina uwezo wa kukusanya kodi kufikia kiwango cha 20.9% ya Zao Ghafi la Ndani (GDP), kulingana na makadirio ya  Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF) lakini imekuwa ikikusanya  kiasi kinachozidi kidogo 14% (kwa makadirio ya  2009/10). Ingawa  mapato ya kodi kama sehemu ya Zao Ghafi la Ndani (GDP)  yamekuwa yakiongezeka  taratibu (15.2%  kwa mwaka 2010/11 na yanategemewa  kufikia 16.2%  kwa mwaka 2013/14),  hii bado ni pungufu ya uwezo uliopo uliothibitishwa.  Sheria  ya mabadiliko ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) itakayoanza  kutumika hivi karibuni  izingatie suala la upunguzaji  wa misamaha ya kodi ambazo zinafikiriwa kimakosa kuvutia na kudumisha Uwekezaji wa  Nje ndani ya nchi wakati zinasababisha upotevu mkubwa wa mapato.  Tunapongeza serikali kwa kuonesha nia ya kupunguza changamoto za  upotevu wa mapato na  kuanzishwa kwa sheria ya mabadiliko ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kunadhihirisha nia hii.  Hata hivyo,  Policy Forum inaona kwamba,  nguvu zaidi zielekezwe katika kufikia lengo la serikali la kupunguza kiwango cha misamaha ya kodi ikilinganishwa na Zao Ghafi la Ndani (GDP) hadi  1.2%.  Kiwango cha sasa hivi ni 4.3% ya Zao Ghafi la Ndani.

Afya

Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatarajiwa kupunguzwa  kwa kiwango cha 17.4% toka  shilingi  za Tanzania 754 billioni  kwa mwaka 2013/14 hadi  shilingi 623 billioni  kwa mwaka  2014/15. Sababu kuu ya upungufu huu  ni mchango mdogo zaidi toka kwa Wabia wa Maendeleo  ambao utapunguzwa kwa kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 182.  Hali hii itaathiri  zaidi  upatikanaji wa fedha kwa ajili madawa muhimu na vifaa vya matibabu . Wakati misaada toka nje inakatwa kwa kiwango cha  bilioni 17.7,  Serikali inasita kuziba pengo lililopo ambalo sasa linazidi  shilingi  za Tanzania bilioni 200.

Ikiwa Bunge litapitisha bajeti hii kama  ilivyowasilishwa,  itasababisha  kuisha  kila mara kwa madawa muhimu  katika vituo vya afya  vya serikali  katika mwaka ujao wa fedha. Katika muktadha wa  Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi,  Kijamii na Kitamaduni ambayo serikali ya Tanzania iliridhia mwaka 1976,  serikali inashindwa kwa kiasi kikubwa katika wajibu wake wa kuhakikisha kuwa kila mtu anafikia huduma ya matibabu ambayo inajumuisha uwepo wa madawa muhimu kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kugharimia madawa hayo.  

Pia kuna masuala ya uwajibikaji ambayo  yanahitaji uchunguzi  wa kina. Baada ya kutolewa kwa maoni rasmi ya kiukaguzi  ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  (CAG) ,  Wizara  ya Afya  na Ustawi wa Jamii  inahitaji  kuboresha mtiririko wa taarifa zake za ukaguzi  na kuamua kuchukua hatua.  Inapaswa kuimarisha  Kitengo chake cha ukaguzi wa ndani  na kufanya kazi kwa karibu na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  (CAG) pamoja  na Bunge kufanya marekebisho stahiki ili kuzuia hoja nzito zingine za kiukaguzi .  Ikiwa na maoni safi ya kiukaguzi, Wizara itakuwa katika nafasi nzuri zaidi  kupata msaada wa kisiasa na wa kifedha kwa changamoto zinazokuja siku za mbeleni.   

Elimu

Bajeti ya Wizara  ya Elimu  na Mafunzo ya Ufundi imeongezeka  kutoka shilingi  za Tanzania bilioni 689.7  kwa mwaka 2013/2014 hadi  shilingi  794 bilioni kwa mwaka 2014/15.   Cha kuvutia, Bajeti ya Maendeleo ya Wizara imeongezeka toka shilingi  bilioni  72  kwa mwaka 2013/14 hadi shilingi bilioni  454 mwaka 2014/15.  Kuhusu matumizi ya kawaida,   yamepungua toka shilingi  bilioni 612  mwaka uliopita hadi shilingi bilioni 340 mwaka 2014/15.

Pamoja na hayo, hizi takwimu zilizopitishwa zinazua masuala mbalimbali  mbele yetu. Ingawaje bajeti inaonekana imeongezeka kitakwimu, bajeti ya Maendeleo ya Wizara  imepunguzwa.  Hii ni kwa sababu kiasi kidogo kilichoongezeka mwaka huu  kimetokana na mpangilio  mpya wa kifungu cha 7001 kutoka Elimu ya Juu  - 270900 ambacho mwaka 2013/14  kiliwekwa kama bajeti ya kawaida cha kifungu cha 1003 (Sera na Mipango)  ambacho kiko chini ya  matumizi ya Maendeleo  kwa mwaka 2014/15.

Hii inamaanisha kuwa sehemu kubwa ya kinachoitwa bajeti ya maendeleo haitumiki kweli kama bajeti halisi ya maendeleo bali inaelekezwa kwenye Elimu ya Juu kama mikopo kwa wanachuo  kwa matumizi yao ya kawaida.  Suala la kama mikopo ya wanachuo ichukuliwe kama uwekezaji linahitaji mjadala kwa sababu mikopo  hiyo haina faida  na  urejeshaji umekuwa ni changamoto. Kwa hiyo   ukiangalia takwimu kwa makini, utaona kuwa Wizara bado inatumia  fedha kidogo  katika miradi ya elimu.  Hii ni kweli kwa kuwa kati ya shilingi  bilioni 454  iliyopangwa  kwa matumizi ya maendeleo,  shilingi  bilioni 307  zimepangwa  kwa Bodi ya Mikopo ya Wanachuo wa Elimu ya Juu   kwa ajili ya mikopo ya wanachuo. Hii ni  68%  ya jumla ya bajeti ya Maendeleo ya  Wizara.

Kilimo

Sekta ya Kilimo ni mojawapo ya sekta muhimu Tanzania  kwa sababu kadhaa.  Kati ya hizo ni pamoja na ukweli kwamba sekta hii inaajiri zaidi ya nusu ya wakazi wa Tanzania  (74%) na ilichangia 24.8%  kwa mwaka 2012 na 24.7%  kwa mwaka  2013 ya Zao Ghafi la Ndani (GDP).  

Pamoja  na huu wajibu muhimu ambao sekta hii inayo katika uchumi, inakumbana na changamoto  kadhaa kuanzia  ndani hadi nje  ya sekta.  Ndani ya sekta, kuna uthibitisho wa matumizi mabaya ya fedha za umma zilizopangiwa sekta hii, na kutokana na hili  miradi ya maendeleo imeshindwa kutekelezwa  vizuri.  Nje ya sekta, utoaji wa fedha kwa sekta hii haujawa mzuri. Kumekuwa na ucheleweshaji wa upelekaji wa fedha ambao umethibitishwa pamoja na  uwasilishaji wa fedha zisizotosheleza. 

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG)  kwa mwaka 2012 inaonesha kuwa miongoni mwa makosa ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika iliyopelekea Wizara kupewa hati isiyoridhisha na CAG ni ukosefu wa nyaraka za kuthibitisha matumizi ya kiasi cha shilingi  2, 162,343,978. Tunahimiza  Wizara izingatie mapendekezo ya CAG  ili kuboresha nidhamu  ya fedha.

Kwa upande wa  utoaji,  ucheleweshaji umekuwa kawaida.  Wakati  haifiki hata miezi mitatu hadi mwaka wa fedha 2013/14 kuisha,  hadi  31 Machi, 2014,  Hazina ilikuwa imetoa 50.4%  tu ya bajeti ya maendeleo  ya Sekta ya Kilimo.

Kinachofurahisha  kuhusu bajeti ya mwaka huu  ya Kilimo  ni ongezeko  la uwajibikaji wa   serikali  kutoa fedha za kuendesha  miradi ya maendeleo.  Hili ni jambo la kupongezwa, lakini  inabakia changamoto kama serikali itaweza  kweli  kupata kiasi hicho cha fedha  na kuzipeleka kwa miradi iliyopangwa.  Kwa mfano,  kwa mwaka 2013/14  serikali ilipanga  kukusanya shilingi bilioni 3.2  lakini hadi Machi 31, 2014  iliweza kukusanya shilingi  bilioni 1.7  (53.7%) tu.

Pamoja na kwamba tunaipongeza Serikali  kwa ahadi  yake ya kutoa fedha  kwa sehemu kubwa ya miradi yake ya  maendeleo,  ni wakati sasa  wa makusanyo ya mapato kuboreshwa  ili kuendana na dhamira hiyo.    Zaidi ya hayo, bajeti ya kilimo bado  iko mbali kufikia lengo la  Azimio la Maputo la mwaka 2003  kuhusu  Kilimo na Chakula  inayosema kwamba  walau 10%  ya Bajeti  yote ya Taifa ipangiwe sekta ya Kilimo. 

Maji

Programu ya Sekta ya Maendeleo ya Maji  (WSDP) iliyozinduliwa mwaka 2006 ilionesha kuwa ni moja kati ya mbinu pana za Kisekta  katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.  Imevutia  ahadi zinazofikia  Dola za Marekani bilioni 1.7  kwa kipindi cha April 2014.  Fedha zimeelekezwa katika Menejimenti ya Rasilimali Maji, Usambazaji Maji Vijijini,  Usambazaji Maji Mijini, na Menejimenti  ya Rasilimali Maji, Upatikanaji wa Maji Vijijini,  Upatikanaji wa Maji Mijini,  na Ujenzi wa  Uwezo wa Kitaasisi.

Kwa ujumla sekta imeshuhudia ongezeko katika utoaji wa fedha hasa katika kitengo cha vijijini kati ya mwaka 2012/13 na 2013/14.  Kwa mara ya kwanza, tumeshuhudia ongezeko kubwa la kipengele cha bajeti ya vijijini  toka shilingi 120,787,537,924  mwaka 2012/13 hadi shilingi 345,805,362,000 mwaka 2013/14. Hili linastahili pongezi.

Licha ya ongezeko la fedha zilizopitishwa kwa ajili ya sekta, awamu ya kwanza ya mpango ilikabiliana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na uchelewaji katika utoaji wa fedha  toka serikalini na pia toka kwa Wabia wa Maendeleo kwa mwaka 2013/14. Jambo lingine linaloleta mashaka ni kwamba  sekta ya maji bado ni tegemezi kwa hisani ya wafadhili, hilo linazua maswali kuhusu uendelevu wa miradi ya maji kote Tanzania. 

Licha ya changamoto za utoaji, uchunguzi wa kile kidogo kinachotolewa unaibua maswali kama tunapata thamani ya fedha kama ilivyokusudiwa.  Mapitio ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji   (WSDP I) ulionesha ukosefu wa kijumla  wa ukaguzi wa kiufundi ili kufahamu kama fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo na kama taratibu za manunuzi zimefuatwa. Kwa  kigezo cha utendaji kazi wa  matoleo ya maji (water point) ya 54%  tutawezaje kuhakikisha  kuwa maji yanatumika ipasavyo? 

Wakati mwaka mpya wa fedha unakaribia kuanza,  tunatoa wito wa kufanyika kwa Mapitio ya sekta ili kuboresha uendelevu wa matoleo ya maji na upatikanaji wa fedha.

 Jinsia

Masuala ya maji, kilimo, afya na elimu yote  yana uhusiano mkubwa na Wanawake . Nchini Tanzania, 98%  ya wanawake wa vijijini walio na nguvu za kufanya kazi  wanajishughulisha na kilimo na wanazalisha kiwango kikubwa cha mazao ya chakula kwa matumizi ya kaya na pia kwa mauzo  nje ya nchi.  Kwa hiyo ingelifaa ionekane dhahiri kuwa bajeti  ya kilimo inazingatia suala la usawa wa jinsia, kwa mfano zitengwe fedha kiasi fulani kwa ajili ya kupanua wigo wa  wanawake  kufikia huduma rasmi za kifedha ili kuimarisha miradi yao ya kilimo, pia kuwezesha wanawake wakulima kufikiwa na huduma za ugani.    Hali kadhalika, uingizwaji wa masuala ya jinsia kunapaswa kudhihirika  katika sekta za elimu, afya na maji ili maisha ya wanawake yaboreke.

Vipaumbele  vingi  vya bajeti  ya mwaka 2014/15  vinahusu  uwekezaji katika miradi mikubwa ambayo kwa sehemu kubwa inamilikiwa na wanaume na ina matarajio ya  matokeo  ya muda mrefu kwa wakulima kama vile  miradi ya umwagiliaji maji na kilimo cha mashamba makubwa. Hata hivyo, masuala ya  pembejeo kama vile mbegu bora au upatikanaji wa fedha vijijini  (mikopo) ambayo yanaweza kuleta matokeo yanayofanana na hayo lakini kwa kutumia rasilimali ndogo zaidi hayaonekani kutiliwa mkazo.  

Hitimisho

Kwa uelewa kwamba miradi yetu mingi ni tegemezi kwa wafadhili wa nje,  tunahimiza serikali kupanua wigo wake wa kodi kutuwezesha kukusanya rasilimali za kutosha  kuendesha miradi yetu mbalimbali ya maendeleo.  Hili ni  jambo muhimu sana hasa katika muktadha wa upunguzwaji wa fedha kutoka kwa wafadhili .

Wakati serikali inaanza hatua za kukusanya rasilimali,  ni muhimu pia uwajibikaji kwa upande wa matumizi ya rasilimali kuimarishwa. Sambamba na hili  ni uboreshaji wa uwazi katika matumizi ya fedha zinazotumika katika utoaji  wa huduma za umma.

Masuala ya kisera tuliyozungumza hapa yanahitaji  kujitoa kwa kiwango kikubwa ili kuyatekeleza.  Mifumo ya maji, afya na elimu pamoja na sekta ya kilimo haiwezi kuachwa kuendelea kushindwa.  Jamii yenye lishe nzuri, iliyoelimika na yenye stadi  ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.  Kwa sababu hii, tunahimiza serikali  itilie maanani haya mapendekezo  machache,  tunapofanya kazi pamoja katika kuzifanya sera zitende kazi kwa watu wa Tanzania.

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter