Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Asasi za Tanzania tumeendelea kufuatilia mchakato wa uchaguzi mkuu 2015 tangu uandikishaji wapiga kura, uhamasishaji hadi kampeni zinazoendelea kwa umakini mkubwa. AZAKI tumefanya hivyo tukiamini kuwa uchaguzi  ni sehemu kuu ya michakato ya kidemokrasia hapa nchini kama ilivyo duniani kote. Sisi asasi za kiraia Tanzania, tukiwa watetezi na wasimamizi wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu, hatumuungi mkono mgombea yeyote wala chama chochote cha kisiasa kinachotafuta kuingia madarakani wala hatulengi kuchukua dola.

Kwa ujumla wake, uchaguzi hufanikishwa na wadau wengi tukiwemo sisi AZAKI, Vyombo vya usalama, viongozi wa Dini, Taasisi za Umma kama Tume na Vyombo vya habari. Lakini makundi makuu mawili ya wahusika wakuu ni wapiga kura na wapigiwa kura.  Ili wapiga kura waweze kuchagua kiongozi atakayeweza kusimamia maendeleo ya nchi na kuhakikisha amani ya nchi inazidi  kudumu  ni lazima viashiria vyote vya uvunjifu wa amani na mazingira ya vitisho kwa wapiga kura  vijadiliwe na wadau na vidhibitiwe mapema. 

Usalama na amani wakati wote wa uchaguzi ni suala la muhimu sana na ndio maana Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 unakuwa wa kidemokrasia, wa haki  na wa amani.  Tanzania ni Taifa lenye amani kwa muda mrefu sasa, lakini tusipokuwa makini katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya haki na usawa huenda tukalitumbukiza taifa hili katika machafuko. Angalizo hili ni muhimu zaidi kwa mwaka huu ambapo hamasa na mashindano vimekuwa kwa kiwango cha juu kuliko miaka mingine yoyote ya nyuma.

Ili kuweza kuhakikisha uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 unafanyika kwa  usalama na amani AZAKI   zimeona ni vyema kuanisha masuala mbalimbali yanayoweza kupelekea uvunjifu wa
amani nchini  kama angalizo kwa  sekta na taasisi husika kuchukua hatua stahiki mapema. Mchakato huu umejaa changamoto mbalimbali ambazo kama hakutakuwa na jitahada za ziada basi ni wazi kuwa tutakwenda kufanya uchaguzi tukiwa katika hali tete zaidi. Kati ya hizo changamoto nyingi zinazojitokeza, sisi wana AZAKI tumeanisha mambo sita makubwa yanayohitaji ufumbuzi wa haraka kabla ya tarehe 25 oktoba. Mambo hayo ni kama yafuatayo;  


(i) Matumizi Makubwa ya nguvu ya Vyombo vya Usalama  
AZAKI  zimegundua kuwa vyombo vya usalama kama Jeshi la Polisi na makundi mengine ya usalama Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa zikilalamikiwa sana kwa kuona kuwa tishio kwa wananchi badala ya kuwa msaada kwa wananchi. Kwa mfano, majeshi haya  yamekuwa yakifanya mazoezi waziwazi  na karibu na makazi ya watu  suala linalopelekea kujenga  uoga na hofu kwa wananchi . Pia baadhi yao  wameonekana wakitapakaa kwenye makazi ya wananchi huku wakiwa wamevaa sare zao. AZAKI zinatambua umuhimu wa vyombo hivi kipindi cha uchaguzi,  AZAKI tunataka vyombo hivi kufanya kazi zao bila kujenga hofu kwa wananchi na kwa mujibu wa Sheria.  


Wito Wetu kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama  
- Vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zake kwa uweledi na tahadhari ya kutowatia hofu wananchi na wapiga kura. Vyombo vya ulinzi visitumie vitisho, nguvu, na silaha za kivita wakati wa mikutano ya kampeni na siku ya kupiga kura.  

- Vyombo vya usalama  kwa namna yoyote   visiegemee  upande wowote wa chama cha siasa bali vitende haki kwa vyama vyote na wananchi wote wakiwemo wagombea mmoja mmoja na wala visikubali kuyumbishwa na mamlaka yoyote nje ya sheria inayovipa mamlaka kutekeleza wajibu wao.  

-  Tunalishauri Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutojihusisha na mchakato wa uchaguzi kuanzia kipindi cha maandalizi,  cha kampeni,  upigaji kura  na baada ya upigaji kura.  


(ii) Daftari la Wapiga Kura na Taarifa za Msingi
 Kwa mujibu wa Katiba na Sheria, Uchaguzi wa Tanzania unasimamiwa na Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar( ZEC).  AZAKI zimebaini pia pamoja na kufanya vizuri katika hatua zingine Tume za Uchaguzi kwa sasa zimeonyesha udhaifu mkubwa katika eneo la utoaji wa taarifa za msingi kwa wadau na umma kwa ujumla.   
Tumeshudia ukinzani wa taarifa mbalimbali zinazotolewa na Tume kama taarifa za idadi halisi ya wapiga kura walioandikishwa pamoja na idadi ya vituo vya kupigia kura. Ukinzani wa
takwimu za muhimu kama hizi ni jambo linaloweza kupelekea uvunjifu wa amani kama lisipo simamiwa vyema. Mambo haya pamoja na mengine yanawaweka wananchi katika hofu kubwa kwa kutokujua kama watapiga kura ama la na endapo idadi halisi ya wapiga kura ni ipi. Hofu inaongezwa na ukweli kuwa Sheria za uchaguzi Tanzania haziruhusu kulalamikia matokeo ya uchaguzi hususani katika ngazi ya urais.


Wito wetu kwa Tume za Uchaguzi
- Tume ya Taifa ya uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar zitimize  majukumu yao kisheria  kwa kutangaza rasmi takwimu za mwisho  za idadi ya vituo vya kupigia kura na kujibu hoja zinazaoibuliwa na wanasiasa badala ya kuwabeza na kuwapuuza.  

-  Tume Itoe Daftari la wapiga kura  lenye vigezo vyote  kwa wadau wote na wanachi kwa ujumla mapema iwezekanavyo ili kutoa fursa ya kurekebisha makosa yatakayobainika.

-  Tume ibandike majina ya wapiga kura kwenye vituo vyote wiki moja kabla ya siku ya kupiga kura kama ilivyoahidi kwa ajili ya wapiga kura kujua vituo watakavyopigia kura. 

- Tume za uchaguzi zifanye kazi kwa uhuru, kufuata sheria, kusimamia kanuni walizokubaliana na vyama vya siasa na kujiepusha kwa namna yoyote kukipendelea chama chochote wakati wote wa mchakato wa uchaguzi. 

- Tume zinapaswa kuhakikisha kuwa zimewapa mafunzo ya uhakika maofisa na wasidizi wa uchaguzi na kuchunguza mienendo yao kabla hawajawakabidhi vituo vya kazi ili kuepusha makosa yaliojitokeza wakati wa kuandikisha wapiga kura. 

- Tume za Uchaguzi zinapaswa kufanya maandalizi mapema, pia kusambaza vitendea kazi vinavyotakiwa kwa wakati ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza siku ya upigaji kura pamoja na hisia kuwa baadhi ya maeneo yanacheleweshewa vifaa kwa makusudi.

- Tume zihakikishe kuwa watu wote wenye sifa na kustahili kupiga kura ambao hawakuandikishwa katika vituo waliko siku ya upigaji kura wanawezeshwa kufaidi haki yao ya kupiga kura kwa mujibu wa sheria. 

- Tume zitangaze matokeo sahihi bila ya kuchelewesha ili kuepusha kutokea kwa vurugu zinazoweza kujitokeza.  


(iii) Mgogoro wa Kusubiri Matokeo katika umbali usiopungua Mita 200
AZAKI tumebaini kuwa jambo lingine linaloweza kuchangia uvunjifu wa amani ni  mgogoro uliobuka kuhusu uhuru wa wapiga kura kubaki vituoni katika umbali usiopungua mita 200.  Kwa mujibu wa  sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 sura ya 343 ya sheria za Tanzania kama zilivyopitiwa mwaka 2010  mpiga kura anapewa haki ya kupiga kura na kuondoka kuendelea na shughuli nyinginezo au kubaki kituoni kusubiri matokeo ili mradi anafanya hivyo katika umbali usiopungua mita 200 toka kituoni na kwamba hafanyi mkutano. Kwa tafsiri hii, mpiga kura
hajalazimishwa kurudi nyumbani baada ya kupiga kura wala hajakatazwa kuwepo nje ya eneo la katazo la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 104 (1).
Sheria inamtaka mpiga kura asionekane ndani ya eneo la  kituo cha kupiga kura baada ya kumaliza kupiga kura(within the vicinity) na haimlazimishi mwananchi arudi nyumbani mara baada ya kupiga kura au asogee umbali wa mita 200 bali sheria ya uchaguzi inaweka bayana kwa wananchi/mpiga kura kutokupiga kampeni au kuvaa nguo zenye alama au nembo ya chama chochote katika siku hiyo.


Wito Wetu kwa Tume za Uchaguzi na Jeshi la Polisi
- Kwa kuwa hili limekuwa  kawaida sasa katika chaguzi zilizopita hapa  Tanzania wananchi kubaki vituoni na  kusubiri matokeo karibu na vituo kwa umbali wa mita 200, na  kutokana na ufinyu wa muda usioweza kutoa mwanya wa kurekebisha sheria hii, Tunazitaka Tume za  uchaguzi  zitumie busara  katika kuamua  suala hili kwa kupima faida na hasara za kuzuia wananchi kubaki vituoni kwa umbali wa mita 200 kama walivyozoea katika  chaguzi zilizopita.

-   Pia, Tume zitoe maelekezo yenye kuangalia zaidi maslahi ya Taifa kwa wananchi  badala ya kusikiliza upande wowote kati ya wanaovutana kuhusu suala hili.  Ushauri wetu kuhusu jambo hili ni kuwa wapiga Kura waamue kuendelea na shughuli zao baada ya kupiga kura lakini wanaotaka waweze kubaki vituoni kwa umbali wa mita 200 kwa kadri ya mapenzi yao huku wakiepuka kufanya kinachofanana na mikutano.

-  Mahakama isadie kutatua mgogoro huu wa tafsiri ya kisheria ili kuepusha  machafuko katika Taifa hili yanayoweza kutokana na imani kuwa kukatazwa kubaki vituoni kuna nia ya kutaka kufanya ujanja Fulani kuhusu kura zao ikiwemo kuziiba.

- Pia tunataka Jeshi la Polisi wasitumie nguvu yoyote kwa wananchi endapo itafika siku ya kupiga kura bila suala hili kupatiwa ufumbuzi. Hii ni kwa sababu kwa jinsi Sheria ilivyo, imeruhusiwa wananchi kubaki umbali wa mita 200 kutoka vituoni.


- Pia tunawataka wapiga kura endapo wataona umuhimu wa kukaa umbali wa mita 200  kusubiri matokeo, basi wafanye hivyo kwa unyenyekevu mkubwa ili kulinda amani na pia kuepuka kuzuia wananchi wengine kutumia haki zao.


(iv) Suala la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na watumishi waliohamishwa vituo vya kazi
Ni kwa mara nyingine sasa katika uchaguzi mkuu wanafunzi wa vyuo vikuu wanakoseshwa haki yao ya kupiga kura  kwa sababu zisizoridhisha. Wanafunzi wengi walijiandikisha katika maeneo ambayo hawatakuwepo siku ya kupiga kura na hawataweza kupiga kura zote tatu kutokana na kwamba vyuo vitakuwa vimefungwa siku hadi tarehe ya upigaji kura. Aidha, baadhi ya watumishi wa umma waliohamishwa vituo vya kazi katika miezi na siku za karibuni nao wamejikuta katika hali ya ugumu waliyonayo wanafunzi na wanavyuo.


Wito Wetu kwa Tume za Uchaguzi
- Asasi za kiraia zinasisitiza watanzania walio katika makundi hayo mawili wapewe  fursa ya kuwezeshwa kufanya taratibu za kisheria kuwawezesha kupiga kura ya Rais siku ya tarehe 25 Oktoba. Aidha, katika miaka ijayo, Tume zihakikishe kuwa technolojia ya habari inawezesha upigaji kuwa wa waliojiandikisha popote nchini bila matatizo yoyote kwa kuwa mfumo ni wa kielektroniki.


- Asasi za Kiraia hazioni ulazima wa Tamko la Tanzania Commission for Universities (TCU) kwamba vyuo vikuu visifunguliwe mpaka baada ya uchaguzi  kwani amri hii inanyima wanafunzi wa vyuo hasa wale wachache walijiandikisha vyuoni  haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kinaweza kuwa ni kichocheo cha uvunjifu wa amani.  Suala hili linapaswa liangaliwe upya kwa miaka ijayo.  


(v) Kauli za Vitisho na Lugha Chafu
Kwa muda huu mchache uliobaki, vyama vya siasa na wanasiasa  vinapaswa kuendesha kampeni za kistaarabu zinazoheshimu misingi ya sheria na siasa za ushindani ambazo zinatambua kuwa kuna kushinda na kushindwa.  Kwa hivyo, kusiwepo na kampeni za vitisho, matusi na ubaguzi wa aina yoyote na badala yake kuwepo kampeni za kistaarabu zinazoheshimu na zinazozingatia maadili ambayo vyama vyote vya siasa vimesaini ili kuliepusha Taifa hili na Machafuko.   

Tunazitaka Tume zote mbili kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kwa wale watakaotoa vitisho kwa wananchi ama kwa wagombea. Tumesikitishwa na kitendo cha Tume kuacha kuchukulia hatua baadhi ya wanasiasa wanaotumia lugha za vitisho kwa wananchi au vyama vinavyokiuka muda wa kumaliza kampeni za uchaguzi.  

Aidha, tunavitaka vyombo vya habari vya umma kuacha mara moja kutoa fursa kwa chama kimoja tu wakati tunafanya uchaguzi wa vyama vingi. Taarifa za kila wiki za Baraza la Habari na  Taarifa ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu zinaonyesha   kuwa toka kampeni zianze vyombo vya Umma hasa TBC na Habari leo vimekuwa zikionesha wazi wazi kukipendelea zaidi chama Tawala katika habari zake na kuziacha ama kuzipa uzito mdogo taarifa za vyama vingine.  Tunakemea na kuvitaka pia baadhi ya vyombo vya habari vya binafsi kuacha kutoa taarifa za kichochezi na za uongo kwa wiki moja hii kuelekea siku ya kupiga kura ili kulinda amani ya Taifa. Kipekee, tunapenda kuvipongeza vyombo vya habari ambavyo vimefuatilia na kutoa taarifa za kampeni za uchaguzi wa Tanzania 2015 kwa uhuru na haki wakati wote wa mchakato huu. Kwetu, tunaona kuwa vyombo hivyo vimechangia kudumisha amani na vinastahili tuzo maalum.

Pia kwa umoja wetu tunatoa tahadhari kwa AZAKI  na viongozi wake kutokushiriki katika shughulizi za kampeni za vyma na wagombea ili waweze kutimiza wajibu wa uwaanngalizi bila kukiuka maadili ya AZAKI.


Mwisho
Sisi ni Asasi za Kiraia (AZAKI) za nchini Tanzania zilizoundwa na kutambulika kisheria na  zinazofanya kazi katika masuala mbalimbali ya kisheria, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Kwa umoja wetu tunasimamia na kuhimiza utawala wa sheria na haki za binadamu na masuala yote ya kimaendeleo ili kuhakikisha maisha ya watanzania yanakuwa bora katika nyanja zote. Kwa sababu hiyo, tunajiona tukiwa na jukumu kubwa la kukemea na kuvitaka vyombo husika kufanyia kazi viashiria vyote vya uvunjifu wa amani ili kulinusuru Taifa letu. Kamwe hatuwezi kunyamazia uovu wala kunyamazishwa!

Imetolewa kwa niaba ya asasi miavuli zilizofanya mikutano mikuu ya mashirika wanachama kati ya tarehe 14 na 17 Oktoba 2015,  
Dar es Salaam
Tarehe 17/10/2015 na:

 
Ismail SuleimanKatibu Mkuu
Baraza la Taifa la Asasi za Kiraia     

Onesmo Ole Ngurumwa
Mratibu wa Kitaifa
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania   

Deus M Kibamba
Mwenyekiti Taifa
JUKWAA LA KATIBA TANZANIA