TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: MAONI YA KIKUNDI KAZI CHA BAJETI CHA POLICY FORUM KUHUSU BAJETI YA TAIFA 2018/2019

Categories

Dodoma, Julai 17 2018

Tarehe 14 mwezi wa Juni 2018 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Philip Mpango aliwasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge ili kuruhusu utekelezaji wake ifikapo Julai Mosi 2018. Hotuba hii ya Waziri ilitanguliwa na mawasilisho ya bajeti za Wizara mbalimbali pamoja na mijadala.

Sisi wanachama wa Kikundi Kazi cha Bajeti cha Policy Forum, tumeisikiliza vizuri hotuba ya Mhe. Waziri na tungependa kutoa maoni yetu juu ya bajeti hii ili kuwezesha utekelezaji mzuri utakaoleta tofauti chanya kwenye maisha ya wananchi. Hivyo basi, tunapenda kusema yafuatayo:

Tunaipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa juhudi kadhaa ambazo imezionesha hadi sasa katika kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi. Tumeshuhudia mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwa na lengo la kuhakikisha utekelezaji wa bajeti kwa kutumia zaidi rasilimali za ndani na kupunguza utegemezi kwa wahisani.

Pamoja na jitihada za Serikali za ukusanyaji mapato kutoka vyanzo vya ndani, bado mapato haya hayajaweza kukidhi mahitaji na hivyo kusababisha miradi mingi ya maendeleo inayotegemea kutekelezwa kwa fedha za ndani kushindwa kutekelezwa. Kuna baadhi ya Wizara hadi kufikia mwezi Aprili 2018 ama hazikuwa zimepokea kabisa fedha za maendeleo zilizopaswa kutoka kwenye vyanzo vyetu vya ndani au zilikuwa zimepokea kias kidogo sana cha fedha hizi.

Kwa mfano, Wizara ya Madini hadi kufikia mwezi Februari 2018, haikuwa imepokea fedha yoyote kutoka mapato ya ndani ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Kiasi kidogo kilichopokelewa na wizara hii (asilimia 3 ya bajeti yake) kilitokana na fedha za wahisani. Wakati huo huo, Wizara hii hadi kufikika mwezi Februari 2018 ilikuwa imevuka kiwango cha makusanyo kwa kukusanya zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 200 huku lengo likiwa ni kukusanya takribani shilingi za kitanzania bilioni 195. Hali hii inakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo ingeleta tija zaidi katika ukusanyaji wa mapato.

Katika bajeti ya mwaka 2017/18 Serikali ililenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 19,997 ikijumuisha mapato kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hata hivyo, hadi kufikia mwezi wa Aprili 2018, jumla ya makusanyo ilikuwa ni shilingi za kitanzania bilioni 14, 838.5 hii ikiwa ni asilimia 75 ya makadirio. Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi yalikuwa bilioni 12,611 sawa na asilimia 74 ya lengo (bilioni 17,106.4). Mapato yasiyo ya kodi yalifikia bilioni 1,789.9 sawa na asilimia 82 ya lengo (bilioni 2,183.4). Mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalifikia bilioni 437.6 ambayo ni sawa na asilimia 64 ya makadirio ya shilingi bilioni 687.3.

Kwa ujumla, hadi kufikia mwezi Aprili 2018, Serikali ilikuwa imekusanya kias cha shilingi za kitanzania trilioni 21.9 hii ikiwa ni asilimia 69 ya lengo la bajeti ambalo ni shilingi za kitanzania trilioni 32.

Tunawasihi Wabunge kupitia mjadala wa bajeti iliyowasilishwa na Mhe. Mpango kuendelea kuikumbusha Serikali umuhimu wa kupanga bajeti inayotekelezeka. Tunahitaji kuona mjadala mpana na wa kina kwenye maeneo yafuatayo:

Namna bora zaidi ya kuboresha ukusanyaji wa mapato. Ukusanyaji uwe wa haki na unaoboresha uhusiano kati ya mlipa kodi na Serikali yake. Tungependa kuona walipa kodi wakiongezeka huku na mapato yakiongezeka pia.

Matumizi sahihi ya rasilimali. Pamoja na ukweli kwamba bado ukusanyaji haukidhi mahitaji, taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali zinaonesha kwamba kuna fedha za Serikali zinazokusanywa ambazo hazitumiki ipasavyo. Tunasisitiza nidhamu zaidi ya matumizi ya kile kinachopatikana.

Uhusiano wa bayana wa kisekta katika kufikia Tanzania ya viwanda. Ni vyema kuainisha sekta ambazo ukuaji wake ni muhimu zaidi katika uchangiaji wa ukuaji wa viwanda vyetu na kuzipa kipaumbele cha bajeti ili kufanikisha malengo yake.

Tunaisihi Serikali yetu kuendelea kuona umuhimu wa kuwekeza kimkakati ili kuleta tija zaidi katika utoaji wa huduma. Zaidi tungependa kuona sekta za kijamii kama elimu na afya zikiendelea kupewa kipaumbele kwenye bajeti yetu.

Maoni yetu mahsusi kwa Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla kwa bajeti hii na zijazo:

Ukusanyaji wa mapato: Serikali izirudishie Mamlaka za Serikali za Mitaa vyanzo vyake vya mapato na kuziimarisha ili ziweze kukusanya kwa ufanisi zaidi. Hatua hii iende sambamba na urasimishaji wa walipa kodi ambao bado hawako kwenye mfumo ili kuongeza mapato.

Mamlaka ya Mapato: Serikali itengeneze mfumo wa kuisimamia Mamlaka ya Mapato ili kuboresha uhusiano mzuri na walipa kodi. Pia, Serikali kuongeza juhudi katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na mfumo wa makusanyo wa mapato yasiyo ya kodi (Government electronic Payment Gateway – GePG) kwa taasisi za Serikali zinazokusanya maduhuli.

Uboreshaji Elimu: Tunaiomba Serikali kuongeza bajeti kwenye sekta ya elimu haswa bajeti ya maendeleo. Hii iendane na kuifanyia kazi changamoto ya ucheleweshwaji wa fedha za maendeleo kwenye sekta hii.

Huduma za afya: Serikali iliangalie tatizo la upungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya kwa kuhakikisha mikakati mizuri zaidi ya kuajiri na kuwabakisha katika ajira watumishi wa afya. Hii iambatane na kuboresha fursa za masomo kwa ajili ya kupata madaktari bingwa kwenye hospitali za rufaa nchini.

Maendeleo ya Vijana: Kuwe na jitahada za pamoja kwa wizara zinazohusika na maendeleo ya vijana. Hizi ni pamoja na wizara zinazohusika na maendeleo ya elimu na mafunzo, ajira, biashara, viwanda, kilimo, na afya. Tunapendekeza kuweka kipaumbele katika kuwajengea vijana wetu uwezo na ujuzi wa kujiajiri na kuajirika.

Kilimo: Serikali kuhakikisha bajeti iliyopangwa kwa ajili ya sekta ya kilimo inatolewa kwa ukamilifu na kwa wakati ili kufanikisha shughuli katika sekta hii haswa za utafiti, umwagiliaji, huduma za ugani, pembejeo, uvunaji na kakabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi zifanyike kikamilifu kama ilivyopangwa katika bajeti.

Imeandaliwa na Kikundi Kazi cha Bajeti cha Policy Forum

Wanachama: Hakielimu, Sikika, Action Aid, Open Mind Tanzania (OMT), Oxfam, Tanzania Gender Networking Programmme (TGNP), Science, Technology, Innovation Policy Research Organization (STIPRO), Community Development for All (CODEFA), Save the Children na Children in Crossfire.

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter