Skip to main content
Imechapishwa na Policy Forum

Wakati Taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Jumapili tarehe 14 Disemba 2014, Kikundi Kazi cha Policy Forum cha Serikali za Mitaa (LGWG) kimeona ni vema kutoa kitabu hiki ili kuwawezesha wananchi wa kawaida kufuatilia na kuelewa jinsi uchaguzi wa serikali za mitaa unavyoendeshwa.
Kitabu hiki ni ufupisho wa yaliyomo kwenye kanuni za uchaguzi kama zilivyotangazwa kwenye matangazo ya serikali namba GN 321, 322 na 323 ya tarehe 5/9/2014 kwa mujibu wa sura ya 287 ya sheria inayohusu mamlaka za wilaya na sura 288 inayohusu mamlaka za miji. Kwenye kitabu hiki pia tumeweka mambo muhimu yaliyomo kwenye kanuni hizi zilizotolewa na TAMISEMI kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2014. Matangazo haya yalitolewa na Waziri wa TAMISEMI siku 90 kabla ya uchaguzi kama sheria inavyoelekeza.


Kitabu hiki kina sehemu kuu nne, sehemu ya kwanza ni utangulizi wakati sehemu ya pili inahusu mambo muhimu ya uchaguzi yaliyomo kwenye kanuni, sehemu ya tatu inahusu baadhi ya kasoro zilizomo kwenye kanuni na sehemu ya nne ni kalenda tarajiwa ya uchaguzi.


Kwenye utangulizi kitabu kinaelezea chimbuko lake ambalo ni muhtasari wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa na kutaja lengo kuu la kijitabu hiki kuwa ni kumwezesha mwananchi wa kawaida kuelewa kirahisi masuala na mchakato wa uchaguzi tarajiwa.


Sehemu ya pili ambayo inaelezea kanuni imetaja sifa za mpiga kura,mchakato wa uandikishaji wa wapiga kura, sifa za wagombea, namna ya kuwasilisha pingamizi baada ya uteuzi, masuala ya kampeni na wahusika watakaotakiwa kuwepo siku ya uchaguzi. Katika sehemu hii pia tumeelezea makosa ya uchaguzi na adhabu ambazo mtu anaweza kupata akitenda makosa hayo.


Kama tulivyosema awali, kwenye kitabu hiki pia (sehemu ya tatu) tumegundua kasoro kadhaa ambazo zisiporekebishwa zitaleta matatizo kwenye uchaguzi huu nazo ni:-


•    Ikitokea mgombea uwenyekiti wa kitongoji, kijiji au mtaa kuwa ndiye mgombea pekee, kanuni hazijaelekeza utaratibu wa kufuata ili kumpata mshindi.  

•    Kanuni haiainishi muda halisi wa wapiga kura kujiandikisha, kilichoelezwa katika kanuni kifungu cha 8 (1) katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji na kifungu cha 9 (1) katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mitaa na Vijiji ni kwamba uandikishaji utafanyika siku 21 kabla ya siku ya uchaguzi.  Hii inapelekea kutoelewa uandikishaji unaanzia lini unakwisha lini.

•    Kanuni zimeambatanisha fomu zinazowapa ugumu wapiga kura. Fomu hizi zinamtaka mpiga kura kuandika jina kamili la mgombea anayemtaka na chama chake. Wananchi waliowengi wataona ni usumbufu na hivyo kutoshiriki na kukosa haki yao ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.

•    Katika fomu za maombi ya kugombea uwenyekiti wa mtaa fomu Na. I. Katika fomu hiyo kifungu namba 9 mgombea anatakiwa ajaze nembo ya chama cha Siasa na nembo ya halmashauri. Katika kifungu cha 10 mgombea anatakiwa ajaze nembo ya halmashauri. Mgombea anajazaje hii fomu katika maeneo haya?

•    Kanuni imetoa adhabu tofauti hasa faini kwa mtu atakayetenda kosa kwenye uchaguzi. Mtu akitenda kosa kwenye mamlaka ya mji faini yake ni shilingi elfu hamsini, kosa hilo hilo likitendwa kwenye mamlaka za wilaya faini yake ni shilingi laki tatu. Pamoja na kwamba huu ni uonevu kwa wanavijiji, hakuna mantiki kosa moja kuwa na adhabu mbili tofauti.   

•    Ukiipitia kalenda ya uchaguzi kwa makini yote yaliyopangwa hayatekelezeki kwa muda unaokusudiwa wa siku 28 kuanzia Msimamizi wa Uchaguzi alipotoa maelekezo ya uchaguzi na ratiba yake hadi kufikia siku ya uchaguzi, kutokana na siku zilizopangiwa utekelezaji wa kila jukumu kuwa ni nyingi zaidi na majukumu hayo hayawezi kufanyika sambamba kwa pamoja ni lazima yapishane ili kupisha jukumu jingine kuchukua nafasi.

MWISHO
Tunapenda kuwaangaliza wanasiasa wetu hapa nchini hasa wakati huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa na tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu kuwa pale wanapokuwa wamekubaliana mambo kikanuni basi wayatimize ili kuongeza imani kwa wananchi wanaowaongoza.
Pia tunavitaka vyombo vinavyosimamia chaguzi hususan TAMISEMI na tume ya uchaguzi watimize majukumu yao kwa weledi, uadilifu na mujibu wa sheria wakizingatia misingi ya demokrasia ikiwemo kujiepusha na upendeleo wa aina yeyote.

……………………………………………………
Israel Ilunde
Makamu Mwenyekiti – Bodi ya Policy Forum

Taarifa kwa waandishi:
Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana na wafuatao:
•    Israel Ilunde: +255 754 772 212, ypcyouth@yahoo.com.au
•    Alex Ruchyahinduru   +255 757716333, policy2@policyforum.or.tz

To read the booklet please click here