Risala ya Kumkaribisha Mgeni rasmi Mhe . Mohamed Omary Mchengerwa (MB), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Katika Hafla ya Uzinduzi wa Kitabu cha MWELEKEO WA KATIBA MPYA TANZANIA: Tulikotoka, Tulipo na Tuendako.

Categories

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Omary Mchengerwa (MB)

Waheshimiwa Wabunge

Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya PF Bw Bakari Khamis Bakari

Ndugu Wajumbe wa Bodi ya PF

Ndugu Viongozi na watendaji wa AZAKI hasa wajumbe wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum

Ndugu Mratibu wa Policy Forum, Bw Semkae Kilonzo

Ndugu waandishi wa habari,

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kwa ajili ya kutafakari mchakato wa Katiba mpya na kuzindua kitabu tulichokiandaa wana PF kwa kushirikiana na JUKATA chini ya uhariri wa mwanazuoni Prof Chriss Peter Maina. Sisi wana AZAKI tuliofika hapa mbele ya waheshimiwa Wabunge tunajisikia wenye bahati  kwa kupata fursa ya kusikika mbele yao  na waandishi wa habari.

Mheshimiwa Mgeni rasmi mimi nimepewa jukumu na wanachama wenzangu kukukaribisha wewe utufanyie mambo mawili muhimu, kwanza utufungulie rasmi hafla hii fupi kwa nasaha zako na pili utuzindulie Kitabu chetu. Kama muda utaruhusu ,tutafurahi pia kwa ruhusa yako kama utatoa nafasi japo fupi ili waheshimiwa wabunge na waandishi wa habari waweze kuichangia hotuba yako na maudhui ya kitabu  chetu  ‘MWELEKEO WA KATIBA MPYA TANZANIA: Tulikotoka, Tulipo  na Tuendako’

Hivyo kabla sijakukaribisha, naomba nitumie muda mfupi kusema machache ili uweze kukielewa kikundi kazi cha serikali za mitaa cha Policy Forum, madhumuni ya kukutana hapa na kutoa muhtasari wa maudhui ya kitabu ambacho tunategemea utakizindua leo.

Mheshimiwa mgeni rasmi na waheshimiwa Wabunge, sisi tunatambua kuwa ninyi ni wawakilishi wa watu na mnayo majukumu mengi na watu wengi wa kuwasikiliza, kitendo chenu cha kujumuika nasi leo ni ishara ya wazi kuwa mnatambua nafasi ya AZAKI katika kusukuma mbele maendeleo hasa kwenye ushawishi wa sera, sheria na upatikanaji wa Katiba mpya iliyo bora.

Mheshimiwa Mgeni rasmi, walioko mbele yako ni wajumbe  wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum(PF), wanaowakilisha Asasi  wanachama zisizopungua 74 ambao tumeunganisha nguvu za asasi zetu  ili kuchangia ubora wa michakato na maudhui ya sera kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi Taifa ili kupata sera zenye  uwazi zaidi, za kidemokrasia, shirikishi  na  zinazozingatia uwajibikaji.

Kwa kuzingatia azma hii, na kwa kuwa majukumu makuu ya PF yamejikita kwenye Utawala bora, Rasilimali za umma, na Sauti za wananchi, Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa  hutumia mbinu za uongozi shirikishi kwa kuwahusisha wanachama na wadau wake kwenye mipango na utekelezaji ambazo zimepelekea kuwa na Dira iliyozaa Mpango mkakati wenye kusheheni yafuatayo;

  1. Kuendeleza Utawala bora ngazi ya serikali za mitaa kwa kuhamasisha uimarishaji wa demokrasia na  kutetea uhuru wa kimaamuzi na kiutendaji wa mamlaka hizo

 

  1. Kuongeza uelewa wa wanachama kuhusu masuala ya mamlaka za Serikali za mitaa na Sekta ya AZAKI kwa ujumla kwa kuendesha mafunzo na kuzalisha machapisho kwa lugha rahisi.

 

  1. Kuimarisha uhusiano wetu na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) na BUNGE, kwa njia ya mikutano ya mashauriano  baina yetu na Waheshimiwa Wabunge, jambo ambalo tunalitekeleza leo.

 

  1. Kufuatilia uwajibikaji wa Kijamii ikiwemo matumizi ya fedha za umma  kwa kutoa mafunzo kwa wananchi na Waheshimiwa Madiwani (Public Expenditure Tracking) 

 

  1. Kuinua Sauti za wananchi kwa kuwasambazia taarifa sahihi katika mfumo rahisi na kuwaelimisha juu ya haki zao na wajibu wao ili kuwa na ushawishi kwenye maamuzi ya umma na ubora wa taasisi za umma kwenye kutimiza wajibu wao wa kuhudumia wananchi

Tukio la leo ni sehemu tu ya juhudi zetu katika kutoa  mchango kwenye mchakato wa kutengeneza sheria mama yaani Katiba ya nchi tukiangazia mchakato wa Katiba mpya ili kutoa mapendekezo ya mwelekeo wa namna  ya kuendesha awamu ya pili ya kukamilisha zoezi la uwandishi wa Katiba.

Kutokana na ukweli kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania ulikwama tena bila muafaka wa mwelekeo wake, sisi kama wadau katika sera na maendeleo ya serikali za mitaa tunaona ni muhimu kurejesha mchakato wa Katiba mpya ili kuukamilisha ukizingatia muafaka wa kisiasa  na kijamii.

Sisi tunaungana na Rais Daktari Mhe. John Pombe Magufuli kwa nia yake ya kuendeleza mchakato wa Katiba mpya alipozungumza Jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 23 Juni 2016 akipokea taarifa ya uchaguzi wa mwaka 2015 kutoka Tume ya Uchaguzi. Alisema;

“Mchakato wa Katiba ulifikia mahali pazuri sana

... Haya mengine yatakapofikishwa serikalini

Tutayafanyia kazi na wakati tutakapokuwa

Tunafanyia kazi inawezekana yakajitokeza

Mengine ambayo yanaweza kuwa added katika huo mchakato.

Katiba ni ya waTanzania lengo letu ni kuipeleka Tanzania mahali pazuri … hiyo ndiyo ahadi yangu”

 

Kwa maoni yetu, kauli hii ya Rais Magufuli ni ahadi na ndoto muhimu sana katika kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. Inawataka wadau mbalimbali wa mchakato huu watumie fursa hii kujitokeza kushiriki kikamilifu kwenye hatua zinazofuata.

Hata hivyo tunasikitika kusikia kwamba,wakati Rais alipoongea na waandishi wa habari tarehe 4/11/2016 Jijini Dar es Salaam, alitamka kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya sio kipa umbele kwa sasa. Kauli yake imetukatisha tamaa kwani yaweza kuwa ndio mwanzo wa kuangusha juhudi zote alizozianzisha mtangulizi wake Mhe Jakaya Mrisho Kikwete.

Sisi tunamsihi Mheshimiwa Rais kukumbuka ahadi yake ya mwezi Juni 2016 ili aongoze kumalizia mchakato wa kuandika Katiba mpya kwani wananchi tunatambua uwezo wake wa kufanya maamuzi na kuyatekeleza kwa maslahi ya walio wengi.

Mheshimiwa mgeni rasmi, Pamoja na yote hayo, tunaomba kutumia fursa hii kuleta muhtasari wa maudhui ya Kitabu chetu cha MWELEKEO WA KATIBA MPYA TANZANIA: Tulikotoka, Tulipo  na Tuendako

Kitabu hiki kimegawanyika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inaeleza historia ya mchakato tangu ulipoanzishwa hadi ulipofikia. Sehemu ya pili inaelekeza tuendako na kupendekeza hatua na masuala muhimu ya kuzingatiwa katika kukamilisha mchakato.

Kitabu kimerahisisha jinsi ya kuelewa namna mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba ulivyoanza na ulipokwamia na ni nini cha kufanya. Malengo yetu ni kuwapa hamasa wananchi kudai katiba mpya ambayo itakuwa imejumuisha mawazo yao.

Pia wafanya maamuzi wanachokozwa na kuhimizwa kuendelea au kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya. Kupitia tukio hili la leo tunapenda kutoa wito kwa viongozi na wananchi kusoma kitabu chetu na kuzingatia mapendekezo yetu ili tuweze kumaliza vyema mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania.

Mhehimiwa Mgeni rasmi ,Tunaomba sasa kwa heshima utuzindulie na useme nasaha zako kwa umma kupitia hadhira hii.

Karibu sana na asanteni kwa kutusikiliza

 

Israel Ilunde-Mwenyekiti, Kikundi kazi cha Serikali za mitaa cha Policy Forum (PF)

 

Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana na wafuatao:

·         Mwenyekiti KikundiKazi cha Serikali za Mitaa: Israel Ilunde:  ilunde@yahoo.com, +255 754772212

·         Elinami John   +255 785 932 298, policy2@policyforum.or.tz

 

 

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter