Mkurugenzi wa TAKUKURU Afurahishwa na Kampeni ya Kudhibiti Upotevu wa Fedha za Umma

Categories

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema imefurahishwa na kampeni ya Policy Forum iitwayo Stop the Bleeding ambayo inahusu udhibiti wa upotevu wa fedha za Umma kupitia njia haramu zikiwemo utakatishaji wa fedha na ukwepaji kodi. Hayo yamesemwa Novemba 11, 2018 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Diwani Athumani alipokuwa akiongea na Wabunge wa Bunge Tanzania Wanaopamba na Rushwa (APNAC).

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika kampeni ya Policy Forum inaelezea vizuri namna rushwa inavyochangia utakatishaji wa fedha pamoja na ukwepiji wa kodi ambapo inaonekana kuwa Afrika inapoteza takribani Dola za Kimarekani Bilioni 80 kwa mwaka kutokana na utakatishaji wa fedha. Alieleza kuwa mikakati mingi ya kukomesha biashara hiyo haramamu inahusisha utungaji wa sheria imara na ushirikiano lakini vitendo vya rushwa vinaweza kuwafanya baadhi ya Wabunge kutumiwa na baadhi ya vikundi ili kupitisha sheria mbovu kwa maslahi yao binafsi. Alisisitiza kuwa  “Wabunge wanapaswa kuwa mabalozi katika kuzuia na kupambana na rushwa ili kusimamia vizuri bajeti inayopitishwa na Bunge pamoja na mapato ya nchi”.

Katika hotuba yake mkurugenozi wa TAKUKURU alitilia mkazo kuwa mapambano dhidi ya rushwa nchini siyo agenda ngeni; ni tatizo la kihistoria na kidunia ambapo mikakati inabadilika kutokana na mabadiliko ya mbinu zinazotumika kuomba na kutoa rushwa. Mfano katika semina hii ya Policy Forum mnaona jinsi makampuni au watu binafsi wanavyotakatisha na kutorosha fedha kwenda nchi zingine kwa njia haramu, sheria na mikakati nayo inapaswa kuboreshwa ili kubaini wahalifu.

Kutokana na kubadilika mbinu na teknolojia, ndiyo maana hata nyie Waheshimiwa Wabunge kila mara mnatunga sheria; Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 na Sheria ya Uhujumu Uchumi. Sheria hii ilitungwa kuendana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mapambano dhidi ya rushwa wa mwaka 2003, kwa vile tatizo la rushwa ni la kikanda na kidunia ndiyo maana mmekuwa na mtandao huu wa APNAC, alisisitiza Athumani.

Katika kuelezea uhusiano baina ya TAKUKURU, APNAC na Policy Forum, Diwani Athumani alieleza kuwa  “tumekuwa na uhusiano wa muda mrefu na tunaomba muendelee kuipigania TAKUKURU na Serikali eneo la mapambano dhidi ya rushwa. Ushirikiano si wa bahati mbaya, hata Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa Awamu ya Tatu (NACSAP III) 2017/2022 umesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali katika vita dhidi ya rushwa”.

Akitaja mafanikio ya TAKUKURU katika kupambana na Rushwa, Mkurugenzi huyo alifafanua kwamba tathmini ya tafiti mbalimbali za kupima kiwango cha rushwa zilizofanywa na vyombo vya ndani na nje ya nchi zinaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua ifuatavyo:- Mo Ibrahim Index on African Governance, 2016 imeiweka Tanzania kwenye nafasi ya 17 kati ya nchi 54 barani Afrika kwa utawala ulio bora kwa kupata maksi 57.5% ikilinganishwa na nafasi ya 18 na maksi 56.7% ya mwaka 2014. Transparency International Corruption Preception Index, 2017 imeiweka Tanzania kwenye nafasi ya 103 kati ya nchi 180 duniani kwa kiwango cha rushwa na kupata maksi 36% ikilinganishwa na nafasi ya 119 na maksi 31% za mwaka 2014. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya ndani ya nchi wa TWAWEZA, 2017 umeonesha zaidi ya asilimia 80 (80%) ya wananchi wa Tanzania waliohojiwa na watafiti wanamaoni kwamba rushwa nchini mwetu imepungua. Utafiti mwingine wa Taasisi ya ndani ya nchi ya REPOA,2017 umeonesha wananchi 7 kati ya 10 (71%) ya waliohojiwa walisema ushiriki wa Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa ni mzuri, imani hiyo ikiongezeka kutoka asilimia 37 ya kwenye matokeo yaliyotolewa mwaka 2014/15.

Bosi huyo wa TAKUKURU alisisitiza kwamba kwa kuwa kampeni ya Policy Forum ina lengo la kudhibiti upotevu wa fedha za umma zinazotoroshwa nje ya nchi, ni vizuri pia tujue kuwa, hata ndani ya nchi kuna wizi mkubwa unafanyika kutokana na vitendo vya rushwa. Nina mfano hai ambapo TAKUKURU imefanya na inaendelea kufanya uchunguzi wa wizi wa Tshs. 5,876,680,677.74 uliofanyika mwaka 2008 katika makampuni (yamehifadhiwa kwa sababu maalumu) yanayofanya kazi Tanzania.

Tanzania imesaini mikataba mingi ya kupambana na rushwa na ni mwanachama wa Jumuiya kama vile Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Rushwa (United Nations Convention Against Corruption-UNCAC), Mkataba wa Mapambano dhidi ya Rushwa Afrika (African Union Convention on Preventing and Combating Corruption), Nchi Zilizoko Chini ya Jumuiya ya Madola, Nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern African Forum Against Corruption (SAFAC) na Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (East African Association of Anti-Corruption Authorities- EAAACA).

 

Marejeo ya Mkukuta

Social Media

We are on Facebook!


drupal hit counter