Habari Za Hivi Karibuni

Siku chache zilizopita, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliunda kamati mbili za wataalamu kwa ajili ya kuchunguza taarifa za kuwapo kwa udanganyifu wa kiwango cha madini katika mchanga wa dhahabu (makinikia), ambao umekuwa ukisafirishwa kupelekwa nje ya nchi. Mchanga huo ni ule unaotoka katika migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi ambayo kwa pamoja inamilikiwa na Kampuni ya Acacia.

Kamati hizo pia zilipewa kazi ya kutoa mapendekezo kuhusu namna bora ya kusimamia sekta ndogo ya madini ya dhahabu. Zaidi ya hapo, kamati hizo pia zilitakiwa kuchunguza na kuchambua masuala ya fedha katika shughuli za uchimbaji wa madini nchini. Matokeo ya uchunguzi wa kamati hizo, yalizaa kikao baina ya Rais Magufuli na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick (ambao ni wamiliki wa sehemu kubwa ya Acacia), Profesa John P. Thornton, hatua ambayo imefungua milango ya majadiliano baina ya wawekezaji hao na serikali ya Tanzania.

Baada ya kufuatilia kwa umakini mkubwa matukio haya pamoja na mwitikio wa jamii kuhusu hatua zilizochukuliwa, Jukwaa la Asasi za Kiraia la HakiRasilimali – PWYP tunaofanya kazi ya utetezi katika sekta ya madini, yenye wanachama tajwa hapo chini tunapenda kueleza msimamo wetu.

Tumefanya mapitio ya mihtasari ya taarifa zote mbili tunaunga mkono baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kamati ambayo yanajenga msingi wa hoja zilizokuwapo tangu mwanzo, hivyo tutapenda kueleza mtazamo wetu kama ifuatavyo:

TUNAMPONGEZA Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake, uthubutu na msimamo wa kuuhisha mjadala wa kitaifa kuhusu usimamizi wa rasilimali za nchi na manufaa yake kwa umma pamoja na dhamira aliyoonyesha ya kuanisha mchakato wa mapitio ya sheria zote zinazosimamia sekta ya madini.

TUNASISITIZA kuwa wananchi wanayo haki ya msingi ya kupata ufafanuzi na maelezo kutoka kwa waliopewa dhamana na wajibu wa kusimamia rasilimali za nchi. Haki hii ni wajibu wa kijamii hivyo kinyume chake ni wahusika kutakiwa kutetea uamuzi waliowahi kuufanya katika mfumo mzima wa uvunaji wa madini dhidi ya thamani halisi ya rasilimali husika. Suala hili linapaswa kwenda sambamba na hatua ya kuwekwa bayana kwa mikataba yote ya uchimbaji wa madini ambayo inapaswa kuwa wazi kwa umma kupitia tovuti ya Wizara ya Nishati na Madini. Ikiwa tunataka kuondoa mashaka na kukosolewa kwa mikaba katika siku zijazo, lazima usiri katika masuala haya ukome kwani unazidisha hali ya wananchi kutowaamini viogozi wenye dhamana ya kusimamia rasilimali hizi.

TUNATAMBUA kwamba uamuzi wa uziduaji wa rasilimali hufanywa kwa kuzingatia mawanda mapana yakiwamo masuala ya kibiashara, huku manufaa yakitarajiwa kupatikana baada ya muda mrefu. Hata hivyo uamuzi wenye sura ya aina hii unaweza kuaminika, kuelewekana kuwa wa maana, ikiwa wananchi wanafahamu mantiki yake kiuchumi na matarajio ya uwekezaji husika, hivyo kuepusha hatari ya kuwapo kwa mkanganyiko wa fikra miongoni mwao.

TUNATOA WITO wa kufanyika kwa mageuzi yenye tija na ufanisi katika mifumo ya sheria, udhibiti wa fedha na usimamizi wa sekta ya madini kwa kuzingatia mambo yafuatayo;

Kuwepo kwa mpango thabiti na huru wa Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi (TEITA), ambao unashirikisha wadau mbalimbali, pia kutambuliwa na kuheshimiwa kwa Asasi za Kiraia (CSO) ambazo watendaji wake wana mchango mkubwa katika kukuza uelewa wa umma kuhusu mapato ya serikali yatokanayo na sekta ya madini pamoja na uhalisia wa kufikiwa kwa matarajio.

Kuhusu wito wa Rais wa kupitiwa upya kwa sheria za madini, tunapenda kutoa hadhari kwamba marekebisho ya sheria zilizopo yasifanywe kwa ‘dharura’ (ikizingatiwa kuwa udharura ambao ulianza kutumika tangu 2010 wakati wa utunzi wa Sheria ya Madini, umesababisha kupitishwa kwa sheria kadhaa pasipo kulipa Bunge na wananchi fursa ya kufanya uhakiki na kujiridhisha kuhusu ubora wake).

Katika mazingira ya sasa kuna kila sababu kuongeza uwazi katika kusaini au kuingia mikataba ya uvunaji / uziduaji wa rasilimali, siyo tu kwa umma bali ushiriki kamilifu wa Bunge katika mchakato huo.  Kwa maana hiyo, sheria lazima zitoe fursa kwa Bunge kuisoma na kuijadili mikataba ijayo baada ya kuwa imepita katika hatua za rasimu na majadiliano katika ngazi ya serikali. Hatua hii itasaidia kupunguza uwezekano kutumika kwa udhaifu wowote unaoweza kuwapo katika mfumo wa serikali wakati wa kuingia katika mikataba hiyo ya madini. Uidhinishaji wa mikataba unaoweza kufanywa na wizara, idara na wakala wa serikali (MDAs) pamoja na makubaliano husika kupitiwa na Bunge ni uthibitisho kwamba wawakilishi wa wananchi wanakuwa wamepata muda wa kutosha wa kujadili uhalali wa mikataba kabla ya kuanza kutekelezwa. Pia ni njia mojawapo ya kuyafanya makubaliano husika kuwa chini ya miliki ya umma.

Uhamishaji fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia uuzaji na uagizaji bidhaa nje ya nchi (transfer mispricing) ni suala linaloingilia na kuathiri sera za kodi, ikizingatiwa kuwa linawiana na ushindani wa malengo ya pande tatu katika mfumo wa ulipaji na utozaji wa kodi: kwanza ni lengo la kuongeza mapato kwa mamlaka ya kodi ya ndani, pili ni lengo la kuongeza mapato kwa mamlaka ya kodi ya nje na tatu ni lengo la kupunguza kodi kwa mlipakodi. Kwa maana hiyo, tunaishauri serikali ichunguze ili kubaini iwapo kulikuwa na mchezo wa uhamishaji fedha (transfer mispricing) miongoni mwa kamuni za Barrick, Acacia na kampuni zake zote tanzu. Na ikiwa itabainika kuwapo kwa ‘mchezo’ unaohusisha kampuni hiyo, basi fedha zilizotoroshwa nje zirejeshwe kwa kampuni za Barrick na Acacia kutakiwa kulipa.

HakiRasilimali – PWYP tunaamini kwamba usimamizi wa rasilimali za nchi siyo tu kukusanya mapato, bali pia lazima tuwe na mtazamo mpana wa kuona umuhimu wa kuziongezea thamani rasilimali hizo. Mfumo mzima wa uongezaji wa thamani ya madini unaweza kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na kukuza ajira. Hata hivyo hayo yanawezekana ikiwa mambo hayo yatazingatiwa katika maboresho yanayokusudia kufanywa. Kwa maana hiyo, tunaukaribisha uamuzi wa serikali wa kujenga kiwanda cha uchenjuaji wa madini ambacho kitakuwa na manufaa ya kiuchumi na kusitisha usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) kwenda nje ya nchi.

Pamoja na kwamba uamuzi muhimu uliofanywa na Rais umechelewa, unajenga msingi wa kuwa na majadiliano yenye tija kuhusu sekta ya madini katika siku zijazo. Katika kutekeleza maazimio ya timu za wataalamu, HakiRasilimali – PWYP tunaishauri serikali  urges governments to be kuzingatia mambo yafuatayo ambayo yanaweza kuwa na matatizo ya kisheria siku zijazo:

Wajibu wa kimataifa wa kisheria ambao serikali imejifunga kuusimamia, kama vile kuzihakikishia kampuni za uwekezaji kwamba mali zao zitakuwa salama na hakutakuwa na utaifishaji;

Umuhimu wa kuendelea kuwa nchi rafiki kwa uwekezaji katika mazingira ambayo yanazinufaisha pande mbili; mwekezaji na serikali; na

Umuhimu wa kuwapo kwa uwazi wa mashauriano wakati wa mchakato wa kubadili mifumo ya sasa ya kisheria na masuala ya fedha katika sekta ya madini.

 

Imeandaliwa na:

Sekretarieti ya HakiRasilimali – PWYP

Muhimu: HakiRasilimali ni jukwaa la Asasi za Kijamii (CSOs) ambazo zimesajiliwa kama kampuni zisizotengeneza faida chini ya Sheria ya Kampuni ya 2002 ambazo zinafanya kazi mahususi kuhusu masuala ya madini, mafuta na gesi nchini Tanzania. HakiRasilimali ni taasisi mshirika wa Publish What You Pay (PWYP), ambayo inaundwa na wanachama ambao ni muungano wa asasi za kiraia katika nchi zaidi ya 40 duniani kote. Lengo la asasi hizo ni kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya rasilimali za madini, mafuta na gesi.

(Wanachama: Action for Democracy and Local Governance, Governance Links, Governance and Economic Policy Centre, Interfaith Standing committee, ONGEA, HakiMadini, Policy Forum, Tanganyika Law Society).

 

PDF

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UZINDUZI WA RIPOTI YA HALI YA UTEKELEZAJI WA DIRA YA MADINI YA AFRIKA

Policy Forum kwa kushirikiana na Tax Justice Network – Africa (TNJ-A), Tanzania Tax Justice Coalition (TTJC) na HakiRasilimali wameandaa uzinduzi wa kitaifa wa Ripoti ya Hali ya Utekelezaji wa Dira ya Madini ya Afrika (AMV) utakaofanyika katika ukumbi wa Bunge (Old Dispensary Hall), Dodoma  tarehe 15 Mei, 2017.  Uzinduzi  huo utaanza saa 6:30 mchana.

Dira ya Madini Afrika iliasisiwa 2009 na wakuu wa nchi za kiafrika (ikiwemo Tanzania) zenye madini kwa lengo la kuboresha uwazi, usawa na matumizi bora ya madini kwa lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo. Dira ya Madini ya Afrika (AMV) inasisitiza mabadiliko katika usimamizi wa rasilimali za madini ili kuleta tija katika kukuza uchumi na viwanda barani Afrika. 

Kuasisiwa kwa AMV kulizua mijadala mbalimbali kutoka kwa wananchi wakihoji ni  kwa namna gani faida zitokanazo na madini zitaleta mageuzi ya kiuchumi  na madhara yatokanayo na shughuli za uchimbaji madini yanawezaje kutatuliwa. Mijadala ya aina hii ilianzia kwenye jamii ambazo shughuli za uchimbaji wa madini zilianza kati ya miaka ya 1980 na 1990.

Baada ya miaka saba ya kuasisiwa kwa AMV, Tax Justice Network-Africa (TJN-A) imefanya utafiti wa kisayansi katika nchi tatu - Ghana, Tanzania na Zambia kuangalia hali ya utekelezaji wa mojawapo ya nguzo saba muhimu za AMV ambayo ni Usimamizi wa Mapato na Mifumo ya Usimamizi wa Fedha.

Utafiti huo umelenga zaidi kupima maendeleo ya utekelezaji wa AMV katika nchi zilizoazimia dira hiyo ikiwemo Tanzania. Pia, utafiti umepima ulinganifu wa mifumo ya usimamizi wa fedha pamoja na mapato katika ngazi ya kitaifa na kikanda. Ripoti ya utafiti huo imetoa mapendekezo kwa lengo la kuboresha usimamizi wa fedha na mapato yatokanayo na madini.

Mojawapo ya mapendekezo, ni kuimarisha uwezo wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ili kukabiliana na tatizo la uhamishaji haramu wa fedha kutoka kwenye sekta ya madini.

Ripoti imependekeza kuanzishwa kwa sera ambayo itanufaisha jamii zilizoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini. Mapato yatokanayo na shughuli za madini yawezesha jamii hizo kupata maji safi na salama, huduma bora za afya, elimu bora na miundombinu madhubuti.

Ripoti hiyo itazinduliwa mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na wawakilishi mbalimbali kutoka taasisi za kiserikali na wanahabari na itapatikana mara baada ya kuzinduliwa. ________________________________________________________________________

Kwa taarifa zaidi, wasiliana nasi: info@policyforum.or.tz / 0782317434

Toleo la Bajeti ya Wananchi 2016/2017 kama ilivyokuwa kwa matoleo yaliyotangulia1, linakusudia kutoa maelezo rahisi na wazi kuhusu Bajeti ya Serikali ya 2016/17. Kimsingi, Bajeti ya Serikali ni makadirio ya mapato na matumizi yanayoandaliwa na Serikali kwa mwaka. Ni chombo muhimu kinachotumiwa na Serikali kutekeleza maamuzi yake ya sera kwa vitendo kisiasa, kijamii na kiuchumi. Aidha, ni andiko ambalo linaonesha jinsi Serikali inavyopanga kukusanya mapato kupitia vyanzo mbalimbali na jinsi inavyotarajia kutumia kulingana na vipaumbele vilivyopangwa katika mwaka husika wa fedha.Kusoma zaidi bofya hapa.

Februari 2015 Jopo la Ngazi ya Juu Kuhusu Uhamishaji Haramu wa Fedha kutoka Barani Afrika, likiongozwa na Mwenyekiti wake Rais Thabo Mbeki, liliwasilisha ripoti yake kwa Tume ya Umoja wa Afrika/Tume ya Umoja wa Kimataifa ya Kiuchumi Barani Afrika (AUC/ECA). Ripoti ilionesha kuwa nchi za Kiafrika hupoteza kwa wastani dola bilioni 50 kwa mwaka kutokana na uhamishaji haramu wa fedha. Shughuli za kibiashara za sekta binafsi ndizo zinazochangia kwa kiwango kikubwa uhamishaji haramu wa fedha (IFFs), zikifuatiliwa na uhalifu uliopangwa, kisha shughuli za sekta ya umma. Vitendo vya rushwa vinachukua nafasi kubwa katika kuwezesha
uhamishaji huu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Makampuni ya Kimataifa huhamisha faida kwa makampuni tanzu yenye kodi ndogo au mamlaka za kisiri ambapo mara nyingi hayo makampuni tanzu ni makampuni hewa, mengi yakiwa na mwajiriwa mmoja au wawili tu, wakati shughuli zilizo nyingi hufanyika katika nchi nyingine. kusoma zaidi bofya hapa.


Ndugu msomaji wetu na mtumiaji wa kitabu hiki tunakuletea kitabu hiki cha “Mwelekeo wa Katiba Mpya Tanzania: Tulikotoka,Tulipo na Tuendako” likiwa ni chapisho maalum katika awamu ya pili ya mchakato wa kuandika katiba mpya nchini Tanzania.Kusoma zaidi bofya hapa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Omary Mchengerwa (MB)

Waheshimiwa Wabunge

Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya PF Bw Bakari Khamis Bakari

Ndugu Wajumbe wa Bodi ya PF

Ndugu Viongozi na watendaji wa AZAKI hasa wajumbe wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum

Ndugu Mratibu wa Policy Forum, Bw Semkae Kilonzo

Ndugu waandishi wa habari,

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kwa ajili ya kutafakari mchakato wa Katiba mpya na kuzindua kitabu tulichokiandaa wana PF kwa kushirikiana na JUKATA chini ya uhariri wa mwanazuoni Prof Chriss Peter Maina. Sisi wana AZAKI tuliofika hapa mbele ya waheshimiwa Wabunge tunajisikia wenye bahati  kwa kupata fursa ya kusikika mbele yao  na waandishi wa habari.

Mheshimiwa Mgeni rasmi mimi nimepewa jukumu na wanachama wenzangu kukukaribisha wewe utufanyie mambo mawili muhimu, kwanza utufungulie rasmi hafla hii fupi kwa nasaha zako na pili utuzindulie Kitabu chetu. Kama muda utaruhusu ,tutafurahi pia kwa ruhusa yako kama utatoa nafasi japo fupi ili waheshimiwa wabunge na waandishi wa habari waweze kuichangia hotuba yako na maudhui ya kitabu  chetu  ‘MWELEKEO WA KATIBA MPYA TANZANIA: Tulikotoka, Tulipo  na Tuendako’

Hivyo kabla sijakukaribisha, naomba nitumie muda mfupi kusema machache ili uweze kukielewa kikundi kazi cha serikali za mitaa cha Policy Forum, madhumuni ya kukutana hapa na kutoa muhtasari wa maudhui ya kitabu ambacho tunategemea utakizindua leo.

Mheshimiwa mgeni rasmi na waheshimiwa Wabunge, sisi tunatambua kuwa ninyi ni wawakilishi wa watu na mnayo majukumu mengi na watu wengi wa kuwasikiliza, kitendo chenu cha kujumuika nasi leo ni ishara ya wazi kuwa mnatambua nafasi ya AZAKI katika kusukuma mbele maendeleo hasa kwenye ushawishi wa sera, sheria na upatikanaji wa Katiba mpya iliyo bora.

Mheshimiwa Mgeni rasmi, walioko mbele yako ni wajumbe  wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum(PF), wanaowakilisha Asasi  wanachama zisizopungua 74 ambao tumeunganisha nguvu za asasi zetu  ili kuchangia ubora wa michakato na maudhui ya sera kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi Taifa ili kupata sera zenye  uwazi zaidi, za kidemokrasia, shirikishi  na  zinazozingatia uwajibikaji.

Kwa kuzingatia azma hii, na kwa kuwa majukumu makuu ya PF yamejikita kwenye Utawala bora, Rasilimali za umma, na Sauti za wananchi, Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa  hutumia mbinu za uongozi shirikishi kwa kuwahusisha wanachama na wadau wake kwenye mipango na utekelezaji ambazo zimepelekea kuwa na Dira iliyozaa Mpango mkakati wenye kusheheni yafuatayo;

  1. Kuendeleza Utawala bora ngazi ya serikali za mitaa kwa kuhamasisha uimarishaji wa demokrasia na  kutetea uhuru wa kimaamuzi na kiutendaji wa mamlaka hizo

 

  1. Kuongeza uelewa wa wanachama kuhusu masuala ya mamlaka za Serikali za mitaa na Sekta ya AZAKI kwa ujumla kwa kuendesha mafunzo na kuzalisha machapisho kwa lugha rahisi.

 

  1. Kuimarisha uhusiano wetu na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) na BUNGE, kwa njia ya mikutano ya mashauriano  baina yetu na Waheshimiwa Wabunge, jambo ambalo tunalitekeleza leo.

 

  1. Kufuatilia uwajibikaji wa Kijamii ikiwemo matumizi ya fedha za umma  kwa kutoa mafunzo kwa wananchi na Waheshimiwa Madiwani (Public Expenditure Tracking) 

 

  1. Kuinua Sauti za wananchi kwa kuwasambazia taarifa sahihi katika mfumo rahisi na kuwaelimisha juu ya haki zao na wajibu wao ili kuwa na ushawishi kwenye maamuzi ya umma na ubora wa taasisi za umma kwenye kutimiza wajibu wao wa kuhudumia wananchi

Tukio la leo ni sehemu tu ya juhudi zetu katika kutoa  mchango kwenye mchakato wa kutengeneza sheria mama yaani Katiba ya nchi tukiangazia mchakato wa Katiba mpya ili kutoa mapendekezo ya mwelekeo wa namna  ya kuendesha awamu ya pili ya kukamilisha zoezi la uwandishi wa Katiba.

Kutokana na ukweli kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania ulikwama tena bila muafaka wa mwelekeo wake, sisi kama wadau katika sera na maendeleo ya serikali za mitaa tunaona ni muhimu kurejesha mchakato wa Katiba mpya ili kuukamilisha ukizingatia muafaka wa kisiasa  na kijamii.

Sisi tunaungana na Rais Daktari Mhe. John Pombe Magufuli kwa nia yake ya kuendeleza mchakato wa Katiba mpya alipozungumza Jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 23 Juni 2016 akipokea taarifa ya uchaguzi wa mwaka 2015 kutoka Tume ya Uchaguzi. Alisema;

“Mchakato wa Katiba ulifikia mahali pazuri sana

... Haya mengine yatakapofikishwa serikalini

Tutayafanyia kazi na wakati tutakapokuwa

Tunafanyia kazi inawezekana yakajitokeza

Mengine ambayo yanaweza kuwa added katika huo mchakato.

Katiba ni ya waTanzania lengo letu ni kuipeleka Tanzania mahali pazuri … hiyo ndiyo ahadi yangu”

 

Kwa maoni yetu, kauli hii ya Rais Magufuli ni ahadi na ndoto muhimu sana katika kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. Inawataka wadau mbalimbali wa mchakato huu watumie fursa hii kujitokeza kushiriki kikamilifu kwenye hatua zinazofuata.

Hata hivyo tunasikitika kusikia kwamba,wakati Rais alipoongea na waandishi wa habari tarehe 4/11/2016 Jijini Dar es Salaam, alitamka kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya sio kipa umbele kwa sasa. Kauli yake imetukatisha tamaa kwani yaweza kuwa ndio mwanzo wa kuangusha juhudi zote alizozianzisha mtangulizi wake Mhe Jakaya Mrisho Kikwete.

Sisi tunamsihi Mheshimiwa Rais kukumbuka ahadi yake ya mwezi Juni 2016 ili aongoze kumalizia mchakato wa kuandika Katiba mpya kwani wananchi tunatambua uwezo wake wa kufanya maamuzi na kuyatekeleza kwa maslahi ya walio wengi.

Mheshimiwa mgeni rasmi, Pamoja na yote hayo, tunaomba kutumia fursa hii kuleta muhtasari wa maudhui ya Kitabu chetu cha MWELEKEO WA KATIBA MPYA TANZANIA: Tulikotoka, Tulipo  na Tuendako

Kitabu hiki kimegawanyika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inaeleza historia ya mchakato tangu ulipoanzishwa hadi ulipofikia. Sehemu ya pili inaelekeza tuendako na kupendekeza hatua na masuala muhimu ya kuzingatiwa katika kukamilisha mchakato.

Kitabu kimerahisisha jinsi ya kuelewa namna mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba ulivyoanza na ulipokwamia na ni nini cha kufanya. Malengo yetu ni kuwapa hamasa wananchi kudai katiba mpya ambayo itakuwa imejumuisha mawazo yao.

Pia wafanya maamuzi wanachokozwa na kuhimizwa kuendelea au kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya. Kupitia tukio hili la leo tunapenda kutoa wito kwa viongozi na wananchi kusoma kitabu chetu na kuzingatia mapendekezo yetu ili tuweze kumaliza vyema mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania.

Mhehimiwa Mgeni rasmi ,Tunaomba sasa kwa heshima utuzindulie na useme nasaha zako kwa umma kupitia hadhira hii.

Karibu sana na asanteni kwa kutusikiliza

 

Israel Ilunde-Mwenyekiti, Kikundi kazi cha Serikali za mitaa cha Policy Forum (PF)

 

Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana na wafuatao:

·         Mwenyekiti KikundiKazi cha Serikali za Mitaa: Israel Ilunde:  ilunde@yahoo.com, +255 754772212

·         Elinami John   +255 785 932 298, policy2@policyforum.or.tz

 

 

Pages